Iran yadungua ndege isiyo na rubani ya Marekani karibu na Bushehr
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138714-iran_yadungua_ndege_isiyo_na_rubani_ya_marekani_karibu_na_bushehr
Jeshi la Iran limedungua ndege isiyo na rubani ya Marekani iliyokiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu karibu na mji wa kusini wa Bushehr.
(last modified 2026-05-29T05:55:59+00:00 )
May 29, 2026 03:20 UTC
  • IRGC yatungua droni ya Marekani
    IRGC yatungua droni ya Marekani

Jeshi la Iran limedungua ndege isiyo na rubani ya Marekani iliyokiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu karibu na mji wa kusini wa Bushehr.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya jeshi la Iran kuizuia meli ya mafuta ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuvuka Mlango-Bahari wa Hormuz kinyume cha sheria.

Shirika la Habari la Tasnim lilichapisha ripoti hiyo jioni ya jana Alhamisi, likinukuu chanzo cha kijeshi.

Chanzo hicho "kimethibitisha kutunguliwa ndege isiyo na rubani ya Marekani iliyoingia bila ruhusa katika anga ya karibu na Bushehr," ripoti hiyo imesema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, operesheni hiyo imefanyika "kwa kombora la mfumo wa ulinzi wa anga wa taifa.

Wakati huo huo, Shirika la Habari la Fars, limeripoti kuwa mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran umekabiliana na ndege hiyo kupitia vifaa vya ulinzi wa anga vilivyowekwa karibu na miji ya Jam na Kangan katika Mkoa wa Bushehr.

Ripoti zinasema "shughuli za utafutaji ili kupata mabaki ya ndege hiyo zinaendelea katika maji ya Ghuba ya Uajemi."

Mkoa wa Bushehr, ambao una Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Bushehr, pia ulikumbwa na mashambulizi mengi katika vita vya hivi karibuni vya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuanzia Februari 28 hadi Aprili 7.