Feb 27, 2022 03:51 UTC
  • Jumapili tarehe 27 Februari 2022

Leo ni Jumapili tarehe 25 Rajab 1443 Hijria sawa na Februari 27 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1260 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo alipata malezi na elimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Ja'far as-Swadiq (as) kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa baba yake, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuongoza Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, na alikumbana na mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kulingania dini na kupambana na madhalimu. Hatimaye Haroun Rashid alimuua mjukuu huyo wa Mtume (saw) kwa kumpa sumu.

Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha Swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'

Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alizaliwa John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani. Steinbeck alizaliwa mwaka 1902, na katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi ambako alionesha kipawa kikubwa. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away na Cup of Gold.

John Steinbeck

Miaka 46 iliyopita katika siku kama hii ya leo Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara ilijitangazia uhuru. Jamhuri hiyo iko kaskazini magharibi mwa Afrika katika pwani ya Bahari ya Atlantic na ina ukubwa wa kilomita mraba laki mbili na 84 elfu na jamii ya watu karibu laki sita. Jamii ya Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara inaundwa na watu wa kaumu mbalimbali za kiarabu, Barbar, Hassaniya na Tuareg. Mwaka 1975 wakoloni wa kihispania waliikabidhi ardhi ya Sahara kwa Morocco baada ya mapambano ya miaka mingi ya watu wa eneo hilo. Baada ya kuondoka wakoloni wa Kihispania, harakati ya Polisario ilitangaza uhuru wa nchi hiyo kwa kuunda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu na kukataa utawala wa Morocco na Mauritania katika ardhi ya eneo hilo. Mwaka 1979 Mauritania pia ilitupia mbali madai ya kumiliki eneo hilo la Sahara lakini Morocco ingali inadai kuwa ni sehemu ya ardhi yake. Lugha rasmi ya watu wa Sahara ni Kiarabu na asilimia 99 ya wakazi wake ni Waislamu.  

amhuri ya Kiarabu ya Sahara

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.

Najmuddin Erbakan