Alkhamisi tarehe 10 Machi 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Shaabani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Machi 2022.
Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano.
Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.
Tarehe 10 Machi siku kama ya leo miaka 126 iliyopita jeshi la Italia lilishindwa vibaya katika jaribio lake la kutaka kuivamia na kuikalia kwa amabavu Uhabeshi au Ethiopia ya sasa. Lengo kuu la shambulizi hilo la Italia lilikuwa kuiungunisha Ethiopia na makoloni mengine mawili ya nchi hiyo, yaani Somalia na Eritrea. Katika vita hivyo jeshi la Italia lilipata kipigo na hasara kubwa ya hali na mali licha ya kuwa na silaha za kisasa na kulazimika kurudi nyuma.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia.

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari ambaye alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1314 Hijria Shamsia katika eneo la Lar nchini Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Mwaka 1332 alielekea Qum kwa ajili ya elimu ya juu ya Kiislamu. Huko Qum, Ayatullah Musavi Lari aliasisi Kituo cha Kueneza Maarifa ya Kiislamu Duniani ambacho kilikuwa kikisambaza vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha hai za dunia. Mwaka 1372 Hijria Shamsia Academia ya Sayansi ya Jamhuri ya Azarbaijan ilimtunuku shahada ya uzamivu kutokana na taathira kubwa ya vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha ya Kirusi. Ayatullah Mujtaba Lari aliaga dunia siku kama ya leo tarehe 19 Esfand katika Hospitali ya Imam Ridha (as) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa kipindi kirefu.