Mar 15, 2022 02:39 UTC
  • Jumanne tarehe 15 Machi 2022

leo ni Jumanne tarehe 12 Shaabani 1443 Hijria sawa na tarehe 15 Machi mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 945 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Ghassani mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi. Kitabu cha Tamjidul Muhmal ni miongoni mwa athari muhimu za msomi huyo wa Kiislamu. 

Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Mwaka 1901 Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia. 

Emil Adolf von Behring

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo. Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4. Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.

Uchaguzi wa kwanza wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, vibaraka wa madola ya kigeni walilipua bomu katika hadhara kubwa ya waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada muhimu ya Sala ya Ijumaa  mjini Tehran na kuwaua shahidi waumini kadhaa pamoja na kuwajeruhi wengine wengi. Sambamba na kutekelezwa kwa kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia, ndege za kivita za Iraq ziliruka na kuingia katika anga ya mji mkuu Tehran kama tishio la kuonyesha kwamba, mji huu ulikuwa chini ya mashambulio.

Swala ya Ijumaa ya Tehran

Katika siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.

 

Tags