Mar 19, 2022 02:50 UTC
  • Jumamosi, 19 Machi, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe 19 Machi 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Alifariki dunia mwaka 1950. ***

Sir Norman Haworth

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, mwanafizikia na mwanakemia wa Kifaransa alizaliwa huko Paris. Baada ya kusoma masomo yake ya Chuo Kikuu alifanikiwa kuwa msaidizi wa Marie Curie mwanafizikia na mvumbuzi wa radiamu. Baadaye alimuoa binti ya Marie Curie ambapo akishirikiana mkewe walifanikiwa kugundua mpangilio mpya wa radiactive. Frederic Joliot aliaga dunia mwaka 1958. ***

Frederic Joliot

Miaka 88 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ayatullah Mullah Muhammad Hashim Khorasani msomi, mwanafakihi na mwanahistoria mkubwa wa Kishia. Ayatullah Mullah Muhammad Hashim Khorasani ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Thiqatul-Islam alizaliwa mwaka 1280 Hijria katrika mji wa Mash'had Iran. Baada ya kusoma masomo ya msingi alifunga safari na kuelekea Najaf Iraq na kubakia huko kwa muda wa miaka 12 akinufaika na elimu ya wasomi na wanazoni mashuhuri wa zama hizo kama Akhund Khorasani na Sayyid Ismail Sadr. Mullah Muhammad Hashim Khorasani aliporejea kutoka Najaf alielekea Mash'had. Alimu huyu ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni Muintakhab Tawariikh, na Husnul Aqibat Fi Saadatil Khatimah.

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel. ***

Louis de Broglie