Jumapili, 3 Aprili, 2022
Leo ni Jumapili tarehe Mosi ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 3 Aprili 2022.
Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qur'ani Tukufu. Ni mwezi wa rehma na baraka za tele. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi wa Ramadhani ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za mwezi huu. Allah SWT anasema: "Hakika tumeiteremsha (Qur'ani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu." Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hassan AS, ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za mwezi huu na kutujaalia kuwa miongoni mwa wale wanaofadika na baraka zake.

Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhuf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbalimbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabdudu Mungu Mmoja. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Surat Maryam aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka na utawala mkubwa kama tunavyosoma katika Suratun Nisaa aya ya 54. Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhuf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Issa AS, na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 1015 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".

Katika siku kama ya leo miaka 711 iliyopita, alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu na sehemu ya kwanza aliitumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji na alifungwa jela kutokana na njama za maadui zake. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilipoanza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria.

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Zakir Hussein Rais Mwislamu wa India aliaga dunia. Zakir Husain alizaliwa 1897. Alisoma masomo yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh na baadaye kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Berlin nchini Ujerumani. Baada ya kuhitimu masomo kwa miaka mingi alijihusisha na harakati za kielimu na kisiasa. Mwaka 1962 akawa Makamu wa Rais wa India. Hatimaye mwaka 1967 alichaguliwa kuwa Rais kupitia uchaguzi. Zakir Husain alikuwa mpinzani mkubwa wa vitendo vya mabaرu vya Wahindu dhidi ya Waislamu na alikuwa akiafiki Pakistan kujitenga.

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.
