Alkhamisi tarehe 12 Mei 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 12 Mei mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1115 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la 'Ibn Muqlah', mwandishi, mchora hati na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji. Alizaliwa mjini Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo kipindi hicho. Akiwa kijana Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Ibn Abbas. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala hao, walipatwa na hasira na hivyo kumtia jela Ibn Muqlah. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi muda punde baadaye. Umashuhuri wake mwingi ulishuhudiwa katika sekta ya uchoraji. Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalat fi Mizaanul-Khat.'
Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia. Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba, alipofuka macho mwishoni mwa umri wake, na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya nchi nne zilizoikalia kwa mabavu Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ulizingirwa na Urusi ya zamani. Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro na udhibiti huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya mgogoro huo ilikuwa kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Ujerumani Magharibi na Mashariki.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilijitenga na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.
Na miaka 14 iliyopita, katika siku kama ya leo, tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha Rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Tukio hilo la kutisha liliwaacha mamilioni ya watu bila makazi.