May 22, 2022 06:01 UTC
  • Jumapili tarehe 22 Mei mwaka 2022

Leo ni Jumapili tarehe 20 Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 22 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 626 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za Hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, alizaliwa Arthur Conan Doyle mwandishi wa Scotland. Awali Doyle alisomea elimu ya tiba, hata hivyo kutokana na kwamba hakufaulu katika uga huo ndipo akaamua kujiunga na taaluma ya uandishi. Licha ya kwamba Doyle aliandika visa vingi lakini kilichomletea umashuhuri ni majmui ya visa vya polisi vilivyoitwa Sherlock holmes. Arthur Conan Doyle alifariki dunia mwaka 1930.

Arthur Conan Doyle

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita yaani mwaka 1885 aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo. Victor Hugo alijitosa kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alijiengua kwenye uwanja huo na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu.

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita yaani mwaka 1912 alizaliwa Herbert Charles Brown mwanakemia wa Uingereza. Brown alizaliwa mwaka 1912 mjini London na familia yake ikahamia Marekani kabla ya hata kutimiza miaka miwili. Alijiunga na chuo kikuu cha Chicago mwaka 1935 na kusomea kozi ya Kemia na kuendelea na masomo hadi alipofanikiwa kuwa mhazili wa chuo kikuu. Mwaka 1979 alitunukiwa tunzo ya Nobel katika taaluma ya kemia kutokana na jitihada alizofanya katika ugunduzi wa michanganyiko mipya ya kemia kaboni au Organic Chemistry. Herbert Charles Brown alifariki dunia mwaka 2004.

Herbert Charles Brown

Miaka 42 iliyopita katika siku kama hii ya leo sawa na tarehe Mosi mwezi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsiya ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani ambayo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran ilianza kuiwekea Iran mzingiro wa kiuchumi lengo likiwa ni kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na vile vile kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kufikia mapatano. Baada ya uamuzi huo wa serikali ya Marekani; Imamu Khomeini (M.A) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kuwa uhai wa uchumi wa nchi mbalimbali hautegemei madola makubwa na kulihutubu taifa la Iran kuwa: Kamwe msiogope vikwazo vya kiuchumi; kama mtatuwekea mzingiro wa kiuchumi basi tutaimarika zaidi na ni kwa maslahi yetu."

Siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin  baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo.

 

Tags