Jumatatu tarehe 20 Juni 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Dhulqaada 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Juni mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika Bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo. Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan. Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo.
Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini. Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita magaidi wa kundi la Munafiqin walitenda jinai kubwa ya kutisha katika haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had. Bomu liliripuka ndani ya haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein(a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi katika haram hiyo tukufu.
Na katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia alifariki dunia Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, mlinganiaji mkubwa wa Uislamu katika kanda ya mashariki mwa Afrika. Hujjatul Islam Walmuslimin Rizvi alizaliwa huko mashariki mwa India na baada ya kupata masomo ya awali kwa baba yake alijifunza masomo ya juu na lugha za Kingereza, Kifarsi na Urdu na kupata daraja ya Fakhrur Afadhil. Baada ya kulingania dini kwa miaka mingi nchini India, Sayyid Akhtar Rizvi alihisi wajibu wa kuelekea Tanzania, barani Afrika na kuanza kueneza maarifa ya dini na mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume (saw). Allamah Rizvi ameandika na kufasiri vitabu vingi kwa lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani ya al Miizan na kitabu cha Al Ghadir na kujenga makumi ya misikiti, madrasa, maktaba na zahanati. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 76.