Jun 25, 2022 07:47 UTC
  • Jumamosi, 25 Juni, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1443 Hijria sawa na tarehe 25 Juni 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita Nabii Muhammad (saw) aliondoka Madina akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja na kuelekea Makka kwa ajili ya kutufu nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba. Tangu alipohamia Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kutufu al Kaaba lakini alifanikiwa mara mbili tu kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija, Mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada ya Hija kwa njia sahihi. Baada ya kukamilisha ibada hiyo, Mtume Muhammad (saw) alirejea Madina na alipofika katika eneo la Ghadir Khum aliwakusanya masahaba zake, na kwa amri ya Mola wake alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na Kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake. ***

 

Miaka 200 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia. ***

Bendera ya Liberia

 

Tarehe 4 Tir miaka 59 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alihamishiwa katika kambi ya kijeshi ya Eshtar-Abad baada ya kukamatwa na Shirika la Usalama Wa Taifa la Shah maarufu kwa jina la Savak. Siku 40 baada ya kushikiliwa katika kambi hiyo, Imam Khomeini kwanza alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq. Katika kipindi chote cha miaka 13 ya kubaidishiwa nje ya nchi, Imam aliongoza harakati zake za mapinduzi kupitia wanafunzi wake waliokuwa wakiwasilisha ujumbe zake kwa wananchi ndani ya Iran. Februari mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini na kupokewa na watu milioni tano. Siku 10 baadaye Imam alifanikiwa kuuangusha utawala wa kifalme ulioiongoza Iran kwa kipindi cha miaka 2500. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsia, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran. ***

Silaha za kemikali

 

Tags