Alkhamisi tarehe 4 Agosti 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Muharram 1444 Hijria sawa na Agosti 4 mwaka 2022.
Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1383 iliyopita mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake mjini Madina. Barua hiyo ilisema: "Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nami hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba Imam Hussein alikuwa akijua kuwa atauawa shahidi yeye na masahaba zake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala kwamba wote watauawa shahidi na kwamba mtu mwenye malengo mengine bora arejee Madina.
Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, Habib bin Mudhahir, aliyekuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad akiwaomba wakimbilie kumsaidia mjukuu huyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia watu wa kabila la Bani Asad.” Imam Hussein alimruhusu Habib bin Mudhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Sahaba huyo wa Mtume aliwaambia watu wa kabila la Bani Asad kwamba: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.”
Siku kama ya leo miaka 1038 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alifahamika kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za Fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine ya Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihii ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).
Miaka 230 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania.
Miaka 217 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland alizaliwa. Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton taratibu akaanza kuwa na mapenzi makubwa na elimu za fizikia na hisabati. Aidha alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari ni mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865.
Katika siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark. Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo. Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki.
Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had Iran Ayatullah Sayyid Ali Sistani fakihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia. Alianza kujifunza Qur'an akiwa na miaka 5 na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baadaye Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Hii leo Ayatullah Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuleta umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye bahari ya China ya Kusini. Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini.