Aug 04, 2022 06:23 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikiliza wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, hii ikiwa ni sehemu ya 33 katika mfululizo huu wa vipindi cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.

Wapenzi wasikilizaji, wengi wa Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu huwa hawapati tatizo wala kusumbuka wanapozungumzia umoja na upweke wa Mwenyezi Mungu na kukanusha kushirikishwa kwake au kwa ibara nyingine Tauhidi, lakini hutatizika na kuingiwa na shaka wanapokumbwa na suala la kuthibitisha Uimamu na Maimamu na hii ni katika hali ambayo suala hili ni tawi la Tauhidi kwa maana kuwa linatokana na imani juu ya Mwenyezi Mungu mmoja ambaye ndiye aliwaamuru Waislamu walizingatie na kuliamini na wakati huo huo kuwachagua watu waliopaswa kufuatwa katika uwanja huo.

Uimamu ni moja ya itikadi za kimatendo zinazotokana na imani juu ya Mwenyezi Mungu mmoja na bila shaka watu watapimwa imani zao kwa itikadi hiyo na ima kulipwa malipo mema au au kuadhibiwa kutokana na itikadi hiyo. Ni kwa nini tunasema hivi wapenzi wasikilizaji? Hii ni kwa sababu Uimamu umekuwa na ungali ni msingi thabiti katika misingi ya dini ya Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu na imani haitimii ila kwa msingi huu thabiti. Jambo hili, wasikilizaji wapenzi linatokana na ukweli kwamba Uimamu ni rehema na neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Muumba kama ulivyo Utume kwa waja wake. Neema mbili zote hizi ni nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo huwaongoza waja kuelekea kwa Muumba wao mtukufu na kwa ajili ya kupata ridhaa zake. Pamoja na hayo kuna tofauti kati ya Utume na Uimamu kama tunavyoshuhudia hilo katika Aya ya 7 ya Surat ar-Ra'd ambapo Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume wake Mtukufu (saw) kwa kumwambia: Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoa. Na ili kuwaepusha Waislamu wasitaabike na kutofahamu mtu aliyekusudiwa kufuatwa baada ya mwonyaji ambaye ni Mtume (saw), Mtume mwenyewe aliweka mkono wake kwenye kifua chake kitakatifu na kusema: 'Mimi ndiye mwonyaji.' Kisha kuuweka kwenye bega la Ali (as) na kusema: 'Ewe Ali! Wewe ndiwe mwongozi, ambaye wataongoka nawe walioongoka baada yangu.'

Maneno haya yamenukuliwa na sahaba mashuhuri Abdallah bin Abbas. Ibn Jurair at-Tabari pia amemnukuu akiyasema hayo katika tafsiri yake ya Jamiul Bayaan, Fakhr ar-Razi katika tafsiri ya al-Kabir, as-Suyuti katika ad-Durr al-Manthur fi at-Tafsir bil Maathur, Muttaqi al-Hindi katika Kanzul Ummal na vitabu vingine vingi. Kisha tusisahau wasikilizaji wapenzi kuwa Aya tukufu tuliyotangulia kuisoma inasema, 'na kila kaumu ina wa kuwaongoa.' Na hii ina maana kuwa katika kila zama kuna kiongozi anayewaongoza watu katika zama hizo la sivyo watapotea na kuangamia. Kwa maelezo hayo je, ni viongozi gani waliochaguliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na hivyo kustahiki kuongoza Umma wa Kiislamu kuelekea kwenye njia nyoofu na ya saada ya humu duniani na huko Akhera, baada ya kuuawa shihidi Imam Ali (as)?

Hili ndilo swali analolijibu Mtume wa Rehema mwenyewe (saw) hivyo hebu na tulisikilize kwa makini.

Mwanazuoni wa madhehebu ya Hanafi Sheikh Suleimani al-Qunduzi anaseme katika kitabu cha Yanabiul Mawadda Lidhawil Qurba naye Sheikh wa Kishafi' Sheikh Ibrahim al-Juwaini katika kitabu cha Faraid as-Simtain kwamba: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliushika mkono wa Imam Ali (as) katika siku ya Ghadir na kuwaambia watu: Ambaye mimi ni Bwana (Mawla) wake, basi Ali pia ni Bwana wake. Ewe Mwenyezi Mungu, mpende anayempenda na mchukie anayemchukia'

Hapo Salman al-Farsi akawa amesimama na kuuliza: Je, nini maana ya ubwana wa Ali? Mtume (saw) akamjibu kwa kusema: 'Ubwana (uongozi/utawala) wake ni sawa kabisa na ubwana wangu. Yule ambaye mimi ni bwana wa nafsi yake (namtawalia zaidi nafsi yake) kuliko yeye mwenyewe basi na Ali ni bwana wa nafsi yake kuliko yeye mwenyewe.'

Mpokezi wa Riwaya hii anasema: Hapo ikawa imeteremka Aya tukufu ya: 'Leo nimekukamiliishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini (5:3). Kisha Mtume Mtukufu (saw) akasema: "Allahu Akbar kwa kukamilika dini na kutimika neema, na kuridhishwa Mwenyezi Mungu na utume wangu na vile vile na wilaya ya Ali baada yangu.'

Masahaba waliokuwa katika mkusanyiko huo mkubwa walipaza sauti wakisema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, Aya hii inamhusu Ali peke yake? Akajibu: 'Ndio, yeye, mimi na mawasii wangu hadi Siku ya Kiama.' Mara hii ombi likawa limetoka kwao: Tubainishie ni akina nani hao. Mtume akawajibu kwa kuwaambia: Ali ambaye ni ndugu na mrithi wangu, wasii wangu na walii wa kila muumini baada yangu, kisha watoto wangu al-Hassan, kisha al-Hussein na kisha watoto tisa wanaotokana na kizazi cha al-Hussein. Wao wako pamoja na Qur'ani nayo Qur'ani iko pamoja nao. Hawatatengana nayo wala Qur'ani haitatengana nao hadi viwili hivi vitakaponijia kwenye Hodhi.'

************

Na hapa wasikilizaji wapenzi tunawauliza maswali kadhaa wale wanaotilia shaka na kuchukizwa na Uimamu wa Imam Hassan na Hussein baada ya Mtume na Imam Ali (as). Je, kuna madhara gani kwa Waislamu iwapo watukufu wawili hawa watakuwa mawasii na viongozi wao baada ya Mtume (saw)? Je, si wao ni katika Nyumba ya Mtume ambao walilelewa na kuishi kwenye nyumba hiyo tukufu na kupewa mafunzo na malezi mema na Mtume mwenyewe (saw) hali ya kuwa wanaona jinsi Wahyi ulivyokuwa ukimteremkia babu yao Mtume Mtukufu na pia kushuhudia kwa karibu matukio mengi yaliyotokea katika Uislamu? Je, si wao ni watoto wa Mtume (saw) kwa mujibu wa maandiko matakatifu ya Qur'ani, na wana wa Ali na Fatwima ambao wanaotokana na kizazi kitukufu na kitoharifu zaidi? Je, baada ya Mtume Mtukufu, Ali na Fatwima az-Zahra (as), si wao ndio wako kwenye nafasi bora zaidi ya kiakhlaqi, kimaadili na kiutukufu inayowafanya Waislamu wawajivunie?

Ni kitu gani kinachowakera baadhi ya watu wakiona watukufu wawili hawa wakiwaongoza Waislamu kwa kuwa ndio wabora wao katika utukufu, elimu, ibada, takwa na sifa nyingine zote bora, jambo linalowafanikisha Waislamu na kuwafanya wanufaike na rehema na baraka za Mwenyezi Mungu na kisha kupata maghfira na radhi zake kutokana na uongozi wa watukufu hao wema?

Kisha ni nini kinachowafanya wanaositasita wasite kuhusu Uimamu wa Hassan na Hussein hali ya kuwa utukufu na Uimamu wao umetajwa wazi mahala pengi katika maandiko ya Qur'ani na Hadithi tukufu za Mtume (saw), ambapo ni mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliwateua naye Mtume (saw) akawatangaza hadharani kuwa mawasii na warithi wake?

Tunashindwa kuelewa ni kwa nini baadhi ya watu wanakerwa na kuchukizwa na Uimamu wa watukufu hawa ambao ni wajukuu na maua ya Mtume Mtukufu (saw) na wakati huo huo viongozi wa vijana wa Peponi na kutochukizwa wala kusita kufuata watu ambao hawana sifa zozote za kuwa viongozi wa dini ya Mwenyezi Mungu na ambao hawako karibu au kufanana na Mtume (saw). Huamua kuwafuata, bila dalili ya kimantiki wala kisheria, watu wasiofaa na ambao hawana sifa zozote za kumrithi Mtume wa Mwenyezi Mungu kiuongozi wala kuwa na ujuzi wowote wa mafundisho ya dini wala kitabu kitakatifu cha Qur'ani, suna za Mtume wala kufungamana na misingi asilia ya kulinda na kutetea dini ya Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji, hapa kuna mtihani mkubwa wa kupima imani ya waja. Watu wanapobainishiwa Aya tukufu za Mwenyezi Mungu na Riwaya za kuaminika kwamba Imam Hassan na Hussein ni Maimamu wawe wanaoongoza ua wamezuiwa kuongoza na kwamba wanapendwa sana na Mwenyezi Mungu na kusifiwa kwenye kitabu chake kitakatifu na kwamba ni makhalifa na mawasii wa Mtume wake, atakayeamini na kuyakubali haya atakuwa amesibu na kusadikisha imani yake, na atakayepinga na kukataa atakuwa amemkadhibisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kupinga waliyoyataka. Hii ni katika hali ambayo Mwenyezi Mungu anatuhutubu katika kitabu chake kitakatifu cha Qur'ani kwa kutwambia: Na anachokupeni Mtume kichukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia……….