Aug 04, 2022 06:29 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hiki ni kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuongoza kwenye dini yake ya haki kupitia Mtume wake mkweli na mbora wa viumbe Muhammad (saw) na mawasii wake watoharifu (as). Ni matumaini yetu kuwa mko tayari kabisa kusikiliza kipindi hiki ambacho tunatumai kitakunufaisheni vya kuto

**********

Tulisema kifupi katika kipindi chetu kilichopita kwamba Uimamu ni sawa na Utume kwa maana kuwa umeanishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na kutangazwa wazi na Mtume wake kwa waja wake. Tulisema pia katika kipindi hicho kuwa Wilaya, yaani uongozi wa Maimamu ni itikadi na imani ya kidini. Kuhusu hilo Aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume (saw) zimebainisha wazi sifa na fadhila za Imam Ali (as) pamoja na ustahiki wake wa kuwa Imam na khalifa wa Umma wa Kiislamu baada ya kuaga na kuondoka duniani Mtume Mtukufu (saw).

Kadhalika kuna mamia ya Hadithi zinazozungumzia wilaya na ukahalifa wa Maiamu baada ya kuaga dunia Mtume, na Hadithi iliyo wazi na madhuhuri zaidi kati ya Hadithi hizo ni ile inayozungumzia tukio la Ghadir Khum. Licha ya uwepo wa Hadhithi chungu nzima zinazozungumzia tukio hilo muhimu katika historia ya Uislamu lakini bado kuna watu wengi na hata wale walioshuhudia tukio hilo kwa karibu ambao bado wana shaka na kusita kuhusu Uimamu na Ukhalifa wa Imam Ali ambao ulitangazwa wazi katika uwanja wa Ghadir Khum. Hii ni licha ya kuwa watu hao hao ambao wanaona vigumu kukiri na kukubali Uimamu wa Ali (as) walikubaliana wazi na wito uliotolewa na Mtume Mtukufu mbele ya makumi ya maelfu ya Mahujaji kutoka mataifa tofauti katika uwanja huo kuhusiana na kadhai ya Imam Ali kuchukua uongozi wa Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume.

Mtume Muhammad kwa kutangaza wito huo alioteremshiwa na Mwwenyezi Mungu kutoka mbinguni alikuwa ametekeleza wajibu wake wa kuthibitisha nafasi ya Uimamu kama msingi mkuu na wa asili katika Uislamu, kama ambavyo alithibitisha pia nafasi na majina ya Maimamu na makhalifa wote kumi na wawili katika tukio hilo muhimu, wa kwanza wao akiwa ni Imam Ali na wa mwisho wao Imam Mahdi (af). Kati ya Maimamu hao ni Imam Hassan na Imam Hussein na waliofuata kutoka katika kizazi cha Aba Abdillah Imam Hussein (sa).

Na ni katika hekima yake Mungu kwamba dilili hizi za kuthibitisha Umimamu wa Maimamu watoharifu zimethibiti na kuandikwa katika vitabu vya Waislamu wote licha ya wengi kukadhibisha na kupinga jambo hilo ambalo limebainishwa wazi katika Qur'ani na Hadithi za Mtume na kujaribu kuhalalisha ukadhibishaji wao huo kwa kutumia dalili batili ambazo hazikubaliki kiakili wala kiuadilifu seuze dini ya Mwemnyezi Mungu Mtukufu.

Wote wanakubali kwamba mtu aliyefaa zaidi kuchukua uongozi na ukhalifa wa Umma wa Kiislamu baada ya kuondoka Mtume (saw) na Imam Ali (as) ni Imam Hassan na Hussein (as) ambao ni mabwana wa vijana wa Peponi. Walilelewa katika Nyumba ya Wahyi wa Mwenyezi Mungu, wapendwa wa kipenzi cha Mwenyezi Mungu, hawakuachana hata kidogo na mafundisho ya Qur'ani wala sunna ya Mtume wake (saw).

Ni kwa kiwango gani Mwislamu huwa na utulivu wa moyo, kuwa kwenye njia nyoofu ya wongofu na kuwa na mwamko wa sawa kuhusu makatazo na maamrisho yake Mungu Muumba anapoongozwa na viongozi na Maimamu wema kama Hassan na Hussein (saw)? Mwislamu wa iana hii huwa na fura iliyoje anapojisalimisha mbele ya watukufu kama hawa, kuwaonyesha mapenzi yake yote na kutayarisha moyo wake kwa ajili ya kufuata uongozi na maelekezo yao, ambapo humuongoza na kumfundisha njia ya sawa na kuushika mkono wake kuelekea kwenye mwanga na nuru ya haki na wema, wongofu, maadili mema, fadhila na ushindi mkubwa wa mbinguni?!!

Wapenzi wasikilizaji, endeleeni kuwa pamoja nasi katika sehemu hii ya kipindi ambapo tunapitia baadhi ya maandiko yaliyomo kwenye vitabu vya Waislamu kuhusu fadhila za Maimamu wawili hawa watukufu (as).

*************

Ibada ni hali na dhihirisho la juu zaidi katika imani na hii ni kutokana na ukweli kwamba inahusiana moja kwa moja na Mwenmyezi Mungu na mvuto kuelekea kwake. Mvuto na hamu hii hudhihirika kupitia ulimi na moyo, roho, itiifu na unyenyekevu, kutii na kutekeleza yale yote aliyoamuru na kuyakataza Mwenyezi Mungu, kama vile kusimamisha swala, kuomba dua, kutoa zaka, kutembelea na kuwa na uhusiano mwema na jamaa wa karibu na kuwasaidia wanyonge na wahitaji. Sifa hizi zote nzuri na hata zaidi ya hizo katika mafundisho ya Uislamu zilidhihirika wazi katika maisha ya Maimamu wawili hawa, Al-Hassan na al-Hussein (as). Walitekeleza vyema na kwa ikhalsi ya juu majukumu yao ya kidini bila ya kuwa na tamaa yoyote ya kidinua na hili ni jambo ambalo wote wanalikiri wazi katika vitabu vyao na hata wale wasiokubali kuwafuata kiuongozi.

Ibn Kathir anasema katika kitabu chake cha al-Bidayatu wa an-Nihaya kwamba: "Hassan aliposimama kuswali swala ya Alfajiri katika Msikiti wa Mtume (saw) alikuwa akiketi kwenye muswala akidhikiri na kumuomba Mwenyezi Mungu hadi jua lilipochomoza."

Abu Naim al-Isfahani anasema katika kitabu cha Hilyatul Auliyaa kwamba Imam Hassan (as) alisema: 'Ninahofu kukutana na Mola wangu hali ya kuwa sijatembea kwenda kuzuru Nyumba yake.' Hivyo akawa ametembea kwa miguu kutoka mjini Madina mara ishirini kwenda kuzuru nyumba hiyo mjini Makka.

Na katika kitabu cha Sunan al-Kubra, al-Baihaqi anamnukuu Ibn Abbas akisema: 'Hassan bin Ali alifanya hija mara ishirini na tano kwa miguu.' Na Hadithi nyingine inayofanana na hiyo imenukuliwa na Tabari al-Shafi katika kitabu cha Dhakhair al-Uqba, Hakim an-Nisaburi katika Mustadrak ala as-Swahihain na al-Qunduzi al-Hanafi katika Yanabiul Mawaddah.

Kadhalika Sheikh as-Swadouq anamnukuu Imam Sajjad Ali bin al-Hussein (as) akisifu na kubainisha kwa kina hali ya ibada ya Imam Hassan al-Mujtaba (as) katika kitabu cha Aamali ambapo sehemu sehemu ya ubainishaji huo inasema: 'Imam (as) kila alipokuwa akisoma katika kitabu cha Mwenyezi Mungu maneno yanayosema: Enyi Mlioamini! Alikuwa akisema: Labbaika Allahumma Labbaika. Na aliposhuhudia hali yake kwenye kitu chochote alikuwa akimdhikiri Allah.' Naye Ibn Shahr Ashub anasema katika kitabu cha Manaqib Aali bin Abi Talib kwamba: Kila wakati Imam Hassan alipotawadha vifundo vyake vilikuwa vikitetemeka na rangi yake kugeuka kuwa ya njano. Alipoulizwa kuhusu jambo hilo alisema: Ni haki ya kila anayesimama mbele ya Mola wa Enzi kubadilika rangi yake kuwa ya njano na kutetemeka vifundo vyake.' Az-Zamakhshari amenukuu Hadithi hii pia katika kitabu chake cha Rabiul Abrar katika hali ambayo Sheikh Nasr bin Muhammad as-Samarqandi an-Hanafi anasema kuwa Imam Hassan (as) alipokaribia mlango wa msikiti alikuwa akiinua juu kichwa chake na kusema: 'Ewe Mungu wangu! Mja wako amesimama mbele ya mlango wako. Ewe uliye Mwema! Amekujia mkosa, hivyo nisamehe makosa yangu kwa wema ulionao, ewe uliye Mkarimu!'

*********

Wapenzi wasikilizaji, sifa na hali ya kuvutia ya ibada aliyokuwa nayo Imam Hassan (as) na ambayo tumetangulia kuizungumzia kwa muhtasari ndiyo ile ile aliyokuwa nayo Imam Hussein (as).

Ibn Jauzi anamnukuu katika kitabu chake cha Swifat as-Swafwa Abdallah bin Ubaid bin Umair akisema: 'Hussein bin Ali (as) alifanya hija mara ishiri na tano kwa miguu.'

Tabarani amesisitiza suala hilo katika kitabu cha Mu'jamul Kabir, Ibn al-Athir katika Usud al-Ghaba, as-Dhahbi katika Siyar A'laam an-Nubalaa, Haithami as-Shafi' katika Majmau' az-Zawaid na wasomi wengine wengi wa masuala ya Hadithi na Riwaya.

Naye Sheikh Nur ad-Deen bin Ali bin as-Swabbagh wa madhehebu ya Maliki anasema katika kitabu chake cha al-Fuswul al-Muhima kwamba Imam Hussein (as) aliposimama kwa ajili ya swala rangi yake ilikuwa ikibadilika kuwa ya njano, hivyo akaulizwa: Ni kitu gani hiki tunachokiona kwako wakati unapotawadha? Akajibu: Hamjui nataka kusimama mbele ya nani!'

Zamakhshari anasema katika kitabu cha Rabiul Abrar kwamba Imam Hussein alionekana akitufu Baitul Haram kisha akienda katika eno la Maqam na kuswali hapo. Kisha aliweka shavu lake kwenye eneo hilo na kulia huku akisema: “Watumishi wako wako mlangoni kwako, wanakutumikia mlangoni kwako, mwombaji wako yuko mlangoni kwako, maskini wako yuko mlangoni kwako.” Alikariri maneno hayo mara kadhaa.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi huku tukitumai kwamba tumenufaika kwa pamoja na yale tuliyofanikiwa kukuandaleini katika kipindi cha leo. Basi hadi tutakapofanikiwa kukutana tena katika kipindi kijacho panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.