Aug 04, 2022 06:37 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaama Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipindi hiki kama mnavyojua wasikilizaji wapenzi, huzungumzia sifa na fadhila za Maimamu na wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) yaani al-Imamain Hassan na Hussein (as) kwa mujibu wa Qur'ani Takatifu na Hadithi za Mtume (saw).

Kati ya mambo yaliyopokelewa katika sifa za maimamu wawili hao watukufu wa Mtume (saw) ni kuitwa kwa jina la Sibtain yaani wajukuu wawili wa Mtume. Kuna hadithi nyingi zilizopokelewa na kunukuliwa katika vitabu vya Waislamu wa madhehebu zote ikiwa ni pamoja na zile zilizonukuliwa na Bukhari katika kitabu cha Tarikh al-Kabir, Ibn Kathir ad-Dimashki katika al-Bidaya wa an-Nihaya, Ibn Hajar al-Haithami as-Shafi katika Swawaiq al-Muhriqa, Tirmidhi, Ibn Majah na wengine wengi katika vitao vyao wakisema kupitia Ya`la Ibn Murrah kwamba Mtume (saw) alisema: 'Hassan na Hussein ni wajukuu wawili kati ya wajukuu.'

Amenukuliwa pia wasikilizaji wapenzi kuhusu hadithi hii na al-Hafidh as-Suyuti as-Shafi' katika kitabu chake cha al-Jami' as-Swaghir, al-Mutaqi al-Hindi katika Kanz al-Ummal, al-Khorazmi al-Hanafi katika Maqtal a-Hussein na wengine wengi. Huenda msikilizaji akauliza kwamba je, nini maana ya neno 'as-sibt' na lina umuhimu gani ambao ulimpelekea Mtume Mtukufu (saw) kusisitiza sana juu ya neno hilo kuhusu wajukuu wake hao? Tunalijadili suala hili baada ya kipande hiki kifupi cha kasida.

**********

Kwa kifupi wapenzi wasikilizaji ni kuwa neno 'as-sibt' ambalo linamaanisha mjukuu sana sana au mara nyingi hutumika kumaanisha mjukuu anayetokana na mtoto wa kike kinyume na ilivyo 'hafid' ambaye ni mjukuu anayetokana na mtoto wa kiume.

Na huenda swali hili likaulizwa hapa kwamba kati ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) yaani Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein ni nani kati yao aliyekuwa karibu zaidi na Mtume (saw)? Ni nani kati yao alipendwa zaidi na Mtume?

Ni wazi kuwa hakuna yeyote kati ya wanahistoria, wataalamu wa Hadithi wala wafasiri wa Qur'ani Tukufu kutoka madhehebu zote za Kiislamu wanaoafikiana kuhusu suala hilo.

Inasemekana kuwa suala la wajukuu wa upande wa watoto wa kike walipendwa sana na mababu zao kwa kadiri kwamba jambo hilo baadaye lilichukuliwa kuwa jambo la kawaida lililokubalika katika dini zote na baadaye likakubaliwa katika Uislamu na kuhesabiwa kuwa jambo la fahari na la kujivunia. Suala hilo lilipewa umuhimu mkubwa katika Uislamu ambapo Mtume Mtukufu (saw) na Imam Ali (as) walijivunia sana kuwa na wajukuu wa upande wa watoto wao wa kike.

Tunalizungumzia suala hili kwa undani kidogo baada ya kipande hiki kifupi cha kasida.

********

Al-Mutaqqi al-Hindi ambaye ni katika wanazuoni wa Kisuni ananukuu katika kitabu chake cha Kanz al-Umma fi Sunan al-Aqwaal wal Af'aal kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Kila umma una mjukuu na mjukuu wa Umma huu ni Hassan na Hussein.'

Katika kitabu chake cha al- Mirqaat al-Mafateeh Ali bin Sultan ananukuu Hadithi ambayo imenukuliwa pia na Tabarani ash-Shafi' katika kitabu cha Mu'jam na Tabari as-Shafi' katika kitabu cha Dhakhair al-Uqba fi Manaqib Dhawil Qur'aba kwamba Muhammad al-Mustafa (saw) alimwambia binti yake Fatwimah (as) katika kusifu utukufu na fahari ya Ahlul Bayt wake kwa kusema: Katika sisi kuna wajukuu wa Umma huu: Al-Hassan na al-Hussein, nao ni watoto wako, na katika sisi kuna al-Mahdi.'

Vile vile Ibn Quluwayh anasema katika kitabu chake cha Kamil az-Ziyaraat kwamba Mtume Mtukufu (saw) baada ya kuwausia Waislamu washikamane na wafuate uongozi na Uimamu wa Ali (as), alitaja baadhi ya sifa na fadhila zake kwa kusema: 'Na wajukuu wawili wa Umma wangu, ambao ni Hassan na Hussein watatokana naye, nao ni watoto wangu. Na katika kizazi cha Hussein watatoka Maimamu wangofu na pia Imamu wa Zama al-Mahdi.' Kisha Mtume (saw) aliendelea kusema: 'Hivyo wapendeni, wafuateni, wala msiwafanye adui zao kuwa kimbilio lenu badala yao, na hivyo kufikwa na ghadhabu ya Mola wenu Mlezi na fedheha katika maisha yenu ya dunia. Na hakika wamepata hasara wale wanaokashifu.'

Kadhalika Abu Jaffar Muhammad bin Abil Qassim at-Tabari wa madhehebu ya Shia anaashiria kwa urefu katika kitabu cha Bisharat al-Mustafa Lishiatihi al-Murtadha maneno aliyoyatamka Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as) mbele ya wale waliompokonya fursa ya kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) katika kutolea hoja ubora na ustahiki wake kwa kusema: 'Basi ninakusihini na kukuulizeni kwa jina la Mwenyezi Mungu: Je, katika nyinyi kuna mtu aliye na wajukuu kama Hassan na Hussein ambao ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na ambao pia ni mabwana wa vijana wa Peponi?! Wakajibu: Allahumma! Hapana.'

La muhimu hapa wasikilizaji wapenzi ni kuwa suala la wajukuu na ujukuu lilitokea kuwa jambo na ibara maalumu iliyotumika kwenye dini kumaanisha watu waliokuwa karibu zaidi, warithi na makahalifa wa Mtume Mtukufu (saw) katika Ahlul Bayt wake. Mtume alisisitiza juu ya ujukuu na mwisho wa ujukuu wake kama ambavyo utume wake ndio uliokuwa wa mwisho. Sheikh Mufid anasena katika kitabu cha Aamali kwamba Mtume alisema katika Hadithi: 'Baba yangu alinizaa, na Mungu akawa amehitimishia kwangu utume, na akazaliwa Ali, na wasia ukawa umehitimishiwa kwake. Kisha mbegu mbili kutoka kwangu na kwa Ali zikaungana na wakawa wamezaliwa al-Jahr na al-Jaheer, Hassanaan (Hassan na Hussein). Hivyo Mwenyezi Mungu akahitimishia kwao ujukuu wa utume, na akajaalia kizazi changu kutokana nao…... Hivyo wao ni watakatifu waliotakazwa wakatakasika. Nao ni mabwana wa vijana wa Peponi. Heri yao wale wanaowapenda, baba yao na mama yao, na ole wao wale wanaowapiga vita na kuwachukia.'

Na hivi ndivyo ujukuu ulikutana na kufungamana na utume ni kana kwamba mambo mawili haya yanaashiria suna na mambo yalivyokuwa katika zama za mitume waliotangulia. Siku moja Salman al-Farisi alimuuliza Mtume (saw): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika kila Mtume ana mawasii na wajukuu, basi ni nani wasii na wajukuu wako wawili?

Mtume alimjibu kwa kumtajia mawasii wa mitume waliomtangulia tangu zama za Nabii Adam (as) hadi zama zake mwenyewe. Kisha alimtaza Ali (as) na kusema: Mimi nitakupa ewe Ali! Nawe utampa mwanao Hassan naye Hassan atampa ndugu yake Hussein, Hussein atampa mwanaye Ali……….' Aliwataja Maimamu wote mmoja baada ya mwingine hadi alipofikia wa mwisho wao ambaye ni Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi na ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhiri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.