Aug 05, 2022 01:11 UTC
  • Ijumaa tarehe 5 Agosti 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 7 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Agosti mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, Omar Bin Saad, alitoa amri ya kuuzuia msafara wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) kutumia kwa aina yoyote maji ya mto wa Furati (Euphrates.) Baada ya Ubaidullah Bin Ziyad, kutuma jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na mjukuu huyo wa Mtume, alituma barua kwa Ibn Saad ili kumzingira Imam Hussein na masahaba zake. Katika ujumbe huo, Bin Ziyad alimtaka Omar Bin Saad kumwamuru Al-Imamul-Hussein kumbai Yazid mwana wa Muawiya. Aidha sehemu nyingine ya barua hiyo ilimtaka kamanda huyo wa jeshi katili kumtenga mjukuu huyo wa Nabii wa Allah na maji ya Mto Furati na asimruhusu kamwe kuweza kuyanywa yeye au vamilia yake. Bila kuchelewa Ibn Saad aliwaamuru askari 500 wapanda farasi kumzuia Imam Hussein na maji ya mto huo. Kitendo hicho cha kikatili, kilijiri ikiwa ni siku tatu kabla ya kuuawa shahidi Imam Huusein (as). Hata hivyo Abul-fadhlil-Abbas alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwaletea maji watu wa msafara huo ingawa hata hivyo askari wale katili walimzuia na kumuua kinyama mtukufu huyo. Hadi asubuhi ya siku ya tisa ya mwezi huu wa Muharram, hakukuwa na tone la maji lililokuwa limesalia kwa wafuasi wa mjukuu huyo wa Mtume (Imam Hussein) suala ambalo liliwafanya watukufu hao kuvumilia tabu ya kiu kali kutokana na joto kali lililokuwepo eneo hilo.

Mto Furat

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, alizaliwa Sayyid Mohammad Hadi Milani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia. Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani alizaliwa tarehe saba mwezi Muharram mwaka 1313 Hijiria Qamaria huko mjini Najaf, Iraq. Alianza kusoma elimu ya dini akiwa na umri mdogo ikiwa ni pamoja na kujifunza Qur'ani Tukufu mjini hapo. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku akiandika pia vitabu vingi. Aidha kando na shughuli hiyo alikuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi elimu ya hawza ya kidini na kufikia daraja ya umarjaa. Msomi huyo alitambulika kwa uchaji-Mungu, taqwa, na tabia njema ya hali ya juu. Kitabu cha 'Muhaadharat fii Fiqhil-Imaamiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Sayyid Mohammad Hadi Milani

Tarehe 5 Agosti mwaka 127 iliyopita, alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Friedrich Engels

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Agosti 1960, nchi ya Burkina Faso iliyoko magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Burkina Faso ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tokea katikati mwa karne ya 19. Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Upper Volta, ilianza kujipatia mamlaka ya ndani mwaka 1958, lakini miaka miwili baadaye ilipatia uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, ilipofika mwaka 1984, nchi hiyo iliamua kubadilisha jina kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi hiyo ya Kiafrika inapakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.

Burkina Faso

Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza ulitiwa saini. Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi lilifikisha mgogoro huo kileleni. Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo ya jadi kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo. Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Oktoba mwaka 1963.

Majaribio la silaha za nyuklia

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini baada ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati  wa kutokea  harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini.

Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini

Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC walipasisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano  wa 19 wa mawaziri hao uliofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri. Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Azimio hilo lina utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Azimio la Haki za Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu. Sifa kuu inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya mwanaadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.