Jun 07, 2016 10:13 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (124)

Assalaamu Alykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kuzungumzia riwaya ambayo tuliijadili katika kipindi kilichopita na kutazama moja ya sababu za udharura wa kuwepo Imam maasumu ambaye amechaguliwa na Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kwenye njia nyoofu na ya saada katika zama zote.

Na hili linatokana na haja ya wanadamu kumuhitajia mtu ambaye atawaondolea shaka na wasiwasi kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwemo ya kidini maishani. Riwaya hii inaashiria kwamba madhumuni na maana yake halisi imebainishwa kwenye vitabu vya Nabii Ibrahim na Musa (as), maana ambayo imeashiriwa katika Surat al-A’la.

*********

Riwaya ifuatayo imeandikwa kwenye marejeo kadhaa ya kutegemewa ikiwa ni pamoja na kitabu cha ar-Rijaal cha Kishiy na Kamal ad-Deen, Ilalu as-Sharai’ na Aamal vya Sheikh Swaduq na vilevile al-Ihtijaj cha Tabarsi na vinginevyo vikimnukuu Yunus bin Ya’qub kwamba alisema: Kundi fulani la masahaba wa Abu Abdillah as-Swadiq (as) lilikuwa mbele ya Imam huyo, akiwemo Hamran bin A’yun, Mu’min Twaq, Hisham bin Salim, Tayar na wengineo. Kulikuwepo na Hisham bin Hakam ambaye alikuwa angali ni kijana. Abu Abdillah (as) as-Swadiq akasema: ‘Je, hauniambii ulivyomfanya Amru bin Ubeid na jinsi ulivyomuuliza?

Hisham alisema: ‘Nifanywe kuwa fidia yako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa hakika ninakuheshimu na kukuonea haya na wala ulimi wangu haufanyi kazi mbele yako. Imam Swadiq (as) akasema: ‘Ewe Hisham! Mkiamrishwa jambo litekelezeni.’ Hapo Hisham alijibu amri ya Bwana wake as-Swadiq (as) na kumueleza yeye na masahaba zake mjadala ufuatao:

Na kabla ya kukufafanulieni mjadala huo tunaashiria hapa kwamba Hisham bin al-Hakam alikuwa mmoja wa masahaba bora zaidi wa Imam Swadiq na Imam Kadhim (as) na mbora wa wajuzi wa masuala ya kiitikadi waliokuwa wakiwatetea vilivyo Maimamu (as) na kubatilisha hoja za maadui wao.

Ama Amru bin Ubeid alikuwa mwanazuoni mkubwa zaidi aliyekuwa akitegemewa na watawala na ufalme wa Bani Abbas katika zama za ufalme wa Abu Ja’ffar ad-Dawaniqi na alikuwa akificha uadui mkubwa aliokuwa nao kwa Imam Swadiq (as) na kudhihirisha zuhudi bandia. Alikuwa akiutetea vikali utawala wa Bani Abbas na kuupiga vita Uimamu wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ambao watawala wa Bani Abbas walikuwa wakieneza propaganda kubwa dhidi yao.

*********

Ndugu wasikilizaji, na baada ya utangulizi huo mfupi kuhusiana na utambulisho wa pande mbili za mjadala huo wa kiitikadi sasa tunakunukulieni mjadala wenyewe.

Hisham alisema: ‘Yalinifikia mambo aliyokuwa akiyafanya Amru bin Ubeid na wafuasi wake katika msikiti wa Basra na hilo kuwa zito kwangu (yaani hujuma yake kwa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) na uteteaji wake kwa Bani Abbas).

Hisham akasema: ‘Nikaelekea kwake (kutokea Kufa) na kufika Basra siku ya Ijumaa. Niliingia kwenye msikiti wa mji huo na kupata humo mzunguko mkubwa wa watu ambapo nilimwona Amru bin Ubeid akiwa amevalia shuka nyeusi ya sufi (yaani Washairi wa Bani Abbas) na shuka nyingine pia huku akiwa anaulizwa maswali na watu. Niliketi juu ya magoti yangu upande wa mwisho kabisa wa watu kisha nikasema: Ewe mjuzi! Mimi ni mgeni, je, utaniruhusu nikuulize suala?

Amru akasema: Nam, niulize…. Nikasema: Je, una macho?

Akasema: Ewe mwanangu! Ni swali gani hili? Kama unaona kitu ni vipi utauliza kukihusu? Hisham akasema: Nikasema: Swali langu ni hivi.

Akasema: Ewe mwanangu! Uliza hata kama swali lako ni la kipumbavu….. Nam, nina macho.

Nikasema: Unayaonea nini? Akasema: Rangi na watu.

Nikasema: Je, una pua? Akajibu: Nam… Nikasema unalitumia kufanyia nini?

Akasema: Ninalitumia kunusa harufu.’

Wasikilizaji wapenzi, Hisham bin al-Hakam (MA) aliendelea kumuuliza hivi Amru bin Ubeid kuhusiana na hisi zote tano na viongo vingine vya mwili pamoja na umuhimu wavyo hadi alipofikia kumuuliza kuhusu moyo.

Hisham akasema: Nilikuuliza, je, una moyo? Aalasema: Nam, nikasema: Unaufanyia nini? Akasema: Ninautumia kuelewa na kufahamu vyema kila jambo ninalofahamishwa na viungo hivi.

Hisham akasema: Je, viungo hivi havijitoshelezi na kutoutegemea moyo? Akajibu hapana. Nikasema: Itakuaje hivyo ilihali vyote ni sahihi na salama?

Amru bin Ubeid akasema: Ewe mwanangu! Ikiwa viungo hivi vitashuku jambo fulani basi, hulinusa, kulitazama, kulionja, kulisikiliza au kuligusa na kisha kulirejesha kwa moyo ambao hatimaye huyakinisha yakini na kubatilisha shaka.

**********

Wapenzi wapenzi baada ya hayo na kufuatia kukiri Amru bin Ubeid haja ya viungo kuhitajia moyo kama imam wavyo, Hisham bin al-Hakam alianza kufafanua haja ya binadamu kumuhitajia Imam pia kwa sababu hiyohiyo yaani kuthibitisha yakini na kuondoa shaka. Riwaya hii inasema mwishoni:

Hisham alisema: ‘Nikasema: Kwa hivyo Mwenyezi Mungu aliumba moyo kwa ajili ya kuondoa shaka ya viungo? Akasema: Ndio, nikasema: Ewe Abu Marwan! Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuviacha viungo vyako hivihivi bali alivijaalia imam ambaye anathibitisha jambo lililosahihi na kuviyakinishia vinalolishuku, basi inawezekanaje aache viumbe wote katika hali ya kuchanganyikiwa, wasiwasi na hitalifu zao bila ya kuwaachia Imam ambaye wanaweza kumrejea ili awaondolee shaka na kuchanganyikiwa huko?

Hapo Amru bin Ubeid alinyamaza kimya bila kusema lolote…. Kisha alimkumbatia Hisham na kumketisha kwenye majlisi yake na wala hakusema lolote hadi alipoondoka. Mpokezi wa riwaya hii anasema: Hapo Aba Addillah as-Swadiq (as) alicheka kisha akasema: Hisham, ni nani aliyekufundisha haya? Hisham akasema: Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Maneno haya yalinitoka tu. Imam (as) akasema: Ewe Hisham! Wallahi maneno haya yameandikwa kwenye vitabu vya Ibrahim na Musa (as).’

*********

Ndugu wasikilizaji, hivyo inabainika wazi kwamba moja ya sababu za kuwepo haja ya kuwa na Imam maasumu aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu kwenye jamii ya wanadamu katika zama zote ni kuondoa mchanganyiko, wasiwasi, hitilafu, mvutano na shaka inayotokana na mitazamo tofauti juu ya maana na hata usomaji wa maandiko matakatifu. Ni wazi kuwa wasiwasi na shaka haiondolewi na mtu asiyekuwa Imam maasumu ambaye ufafanuzi wake ndio unaomfikisha mwanadamu kwenye yakini kwamba anayoyasema ndiyo yaleyale yaliyokusudiwa na Mwenyezi Mungu kwenye maandiko matakatifu ambayo baadhi hayafahamiki moja kwa moja.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wasaalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.