Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (125)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 125 katika mfululizo wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo kama kawaida hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Swali la kipindi cha leo linasema, je, tunawezaje kunufaika na Surat al-Qadr katika kuthibitisha kwamba ardhi haiwezi kuwa bila ya Imam maasumu hadi Siku ya Kiama? Wapenzi wasikiliazaji kama tulivyosema hili ndilo litakalokuwa swali la kipindi chetu cha juma hili basi kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi huku tukijadili kwa pamoja Sura hii ili tupate jibu muafaka kuhusiana na swali hili, karibuni.
**********
Wapezi wasikilizaji, tunaona kwamba Sura tukufu ya al-Qadr kwanza inazungumzia jinsi ya kuteremshwa kitabu kitakatifu cha Quer’ani kwa kusema kuwa kiliteremshwa katika usiku mtukufu wa Qadr na kubainisha fadhila zake huku ikisisitiza juu ya masuala mawili muhimu. Suala la kwanza ni kutumiwa lafudhi ya kitendo kilichopita kuhusiana na kuteremshwa Qur’ani Tukufu yaani ‘Inna Anzalnahu’ katika aya ya mwanzo ya Sura hiyo inayosema: Hakika Sisi tumeiteremsha (Qur’ani) katika usiku wa heshima (Laylatul Qadri). Ama suala la pili ni kutumiwa kitendo cha hivi sasa ambacho bila shaka kinaashiria kuendelea na kutokatika kwa jambo, nacho ni kile ambacho kimetumiwa katika aya ya nne ya sura hiyohiyo inayosema: Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo.
Suala na hali hii ya pili tunaiona pia mwanzoni mwa Surat ad-Dukhan ambapo Mwenyezi Mungu anasema: H'a Mim. Naapa kwa Kitabu kinachobainisha! Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima. Ni amri itokayo Kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. Ni rehema itokayo kwa Mola wako. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Kwa hivyo tukio ambalo hujikariri kila usiku wa Qadr ni kuteremska Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo la Mbinguni ambapo kila jambo la hekima hubainishwa.
Mtume wa MwenyezI Mungu (saw) amesema wazi kwamba Leilatul Qadr itaendelea kuwepo hadi Siku ya Kiama ni hili ndilo jambo linaloaminiwa na kufanyiwa kazi na Waislamu wa madhehebu yote ya Kiislamu hata kama watakuwa wanahitilafiana kuhusiana na usiku huo iwapo ni usiku wa tarehe 23 au 27 ya mwezi mtukufu wa Ramdhani. Hapa swali hili linajitokeza kuwa je, Malaika na Roho huwateremkia nani katika usiku wa Leilatul Qadr kila mwaka kwa amri ya Mwenyezi Mungu ambapo kila jambo la hekima hubainishwa hadi kufikia Leilatul Qadr nyingine mwaka unaofuata? Tunapata jibu la swali hili ndugu wasikilizaji kutoka kitabu hikihiki kitakatifu cha Qur’ani, hivyo endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.
**********
Ndugu wasikilizaji tunaanza kujibu swali hili kwa kuzitazama Surat al-Qadr na ad-Dukhan zenyewe ambazo zinasema wazi kwamba katika usiku huo mtukufu Malaika na Roho huteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakiwa na amri ambayo hubainisha kila jambo la hekima katika usiku wa Leilatul Qadr. Tunapoirejea Qur’ani Tukufu tunaona kwamba inabainisha wazi kwamba wale wanaoongoza kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia kuwa Maimamu wa watu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 73 ya Surat al-Anbiyaa: Na tukawafanya Maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri, na wasimamishe Swala na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu pia anasema katika aya ya 24 ya Surat as-Sajda: Na tukawafanya miongoni mwao Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.
Kwa hivyo Malaika na Roho huwateremkia watu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu Mungu kuwaongoza watu kwa amri yake katika kila usiku wa Lailatul Qadr na kwa idhini ya Mola wao.
Hivyo basi madamu Leilatul Qadr itaendelea kuwepo kila mwaka hadi Siku ya Kiama, ni wazi kuwa Imam maasumu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu pia anapasa kuwepo miongoni mwa watu ili apate kuteremkiwa na Malaika na Roho ili apewe mambo ya hekima anayopasa kuwaongoza kwayo wanadamu.
***********
Na ukweli na hakika hii ya Qur’ani Tukufu imesisitizwa na hadithi nyingi ambazo zimebainisha na kuweka wazi mifano yake ambapo hapa tunaashiria baadhi ya mifano hiyo. Kwa mfano Mtume Mtukufu (saw) amenukuliwa katika kitabu cha Al-Kafi akiwaambia masahaba zake: ‘Iaminini Leilatul Qadr kwa sababu ni kwa ajili ya Ali bin Abi Talib na wanawe kumi na mmoja baada yake.’
Imam Ali (as) pia amenukuliwa kwenye kitabu hichohicho akimwambia Ibn Abbas: Hakika Leilatul Qadr huwa katika kila mwaka. Kwenye usiku huu huteremka amri kwa ajili ya mwaka mzima, amri ambayo ina watu wa kuisimamia baada ya Mtume Mtukufu (saw), nao ni mimi na wanangu kumi na mmoja, ambao ni Maimamu wanaozungumziwa.’
Imam Sajjad Zeinul Abideen (as) pia amenukuliwa kwenye kitabu hichochicho akizungumzia Suratul Qadr ambapo alitaja fitina ya watu walioritadi kwa kukana kubakia usiku wa Leilatul Qadr kila mwaka. Alibainisha sababu ya ukanushaji wao huo kwa kusema: Hii ni kwa sababu wakisema: (Usiku wa Leilatu) upo bila shaka ni lazima kuwepo na amri ya Mwenyezi Mungu kwenye usiku huo, na wakikiri kuwepo kwa amri hiyo basi ni lazima amri hiyo iwe na mtu wa kuisimamia.’
Yaani ni lazima kuwepo na Imamu maasumu ambaye amri hiyo ya Mwenyezi Mungu itamteremkia katika usiku huo wa Leilatul Qadr ali apate kusimamia utekelezaji wake kwenye jamii.
Na Imam Baqir (as) anabainisha katika hadithi nyingine njia za kuhitajia uthibitisho wa uimamu na kuendelea kwake dhidi ya wale wanaoupinga kwa kusema: ‘Enyi Mashia! Jadilianeni kwa Surat Qadr mtafaulu, kwa sababu Wallahi (aya hii) ni hoja ya Mwenyezi Mungu (Maimamu) kwa waja baada ya Mtume Mtukufu (saw). Kwa hakika ni bwana wa dini yenu na upeo wa elimu yetu….Enyi Mashia! Jadilianeni kwa H'a Mim. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha! Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji, kwa sababu (aya hii) ni mahususi kwa ajili ya usimamiaji amri baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).’
*************
Muhtasari wa mambo tuliyojifunza ni kwamba bainisho la wazi la Qur’ani Tukufu katika Suratul Qadr na mwanzoni mwa Surat ad-Dukhan kuhusiana na kuteremka amri ya Mwenyezi Mungu katika usiku wa Leilatul Qadr kila mwaka ni dalili ya kuwepo Imam mwongozaji aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu katika kila zama ili apate kupokea amri hiyo ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu.
Na kwa muhtasari huo ndio tunafikia mwisho wa sehemu hii ya 25 katika mfululizo wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, ambavyo hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Tunakutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.