Jun 07, 2016 10:18 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (126)

Assalaam Aleikum  wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa hamjambo na mko tayari kabisa kutegea siku kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho tumekutayarishieni kwa juma hili.

Swali la wiki hii linasema: Je, ni dalili gani ya Qur’ani Tukufu ambayo inathibitisha Uimamu wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw)? Tunatafuta kwa pamoja jibu la swali hili kutoka kwenye kitabu hicho kitakatifu, karibuni.

**********

Ndugu wasikilizaji, tunaanza kujibu swali hili kwa kukumbushia hakika asilia ya Qur’ani Tukufu nayo ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu  alimpa Mtume wake (saw) ambaye hatamki wala kuteda jambo kwa matamanio na matakwa yake mwenyewe, bali kutokana na wahyi na amri ya mwenyezi Mungu, jukumu la kuwabainishia wanadamu mambo ambayo ameyafupisha kwenye Qur’ani Tukufu kwa kusema katika aya ya 44 ya Surat an-Nahl: ……Nasi tumekuteremshia wewe ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri.

Kwa hivyo dalili ya Qur’ani ya suala hili la Uimamu inafafanuliwa na Mtume Mtukufu mwenyewe (saw) na hili ni jambo ambalo pia linazihusu aya nyinginezo za Qur’ani Tukufu ambazo zinathibitisha Uimamu wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Na kwa kukumbushia hakika hii ya Qur’ani, tunasema kuwa kitabu kitakatifu hiki kina aya nyingi ambazo zinaashiria Uimamu wa Ahlul Beit (as) na kuthibitishwa na Mtume mwenyewe (saw). Miongoni mwa aya hizo ni aya ya 59 ya Surat An-Nisaa ambayo ni mashuhuri kwa jina la aya ya Ulil Amr ambapo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na mwisho mwema.

Na Mwenyezi Mungu amekamilisha maana ya aya hii tukufu na aya nyingine ya 83 katika sura hiyohiyo kwa kusema: Na linapowafikia jambo lolote liliohusu amani au lahofu wao hulitangaza. Na lau wangelilipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wale wanaochunguza wangelilijua. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Yake mngelimfuata shetani ila wachache wenu tu.

Wapenzi wasikilizaji, katika utafiti wao wa Qur’ani, wanazuoni wametegemea aya tuliyotangulia kuitaja ya Ulil Amr katika kuthibitisha kuwepo kwa Imam maasumu katika kila zama hadi Siku ya Kiama, Imam ambaye kutiiwa kwake ni sawa na kutiiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Imam huyu ndiye anayepaswa kutiiwa na kurejewa kwa ajili ya kututa matatizo na hitilafu zinazojitokeza kwenye jamii kwa sababu yeye ndiye aliyerithi elimu ya Mtume (saw) na hivyo kuwa mwenye nadharia maasumu katika kutambua na kufahamu hakika ya Qur’ani na kuwafahamisha watu. Na Mtume (saw) amesema wazi kwamba Maimamu kumi na wawili kutoka nyumba yake ndio Ulil Amr yaani watu walio na mamlaka waliotajwa kwenye aya hii kama ambavyo ushahidi wa kihistoria pia unathibitisha kwamba wao peke yao (as) ndio walio na isma na utambuzi halisi na usio na makosa wa hakika ya Qur’ani Tukufu, bali hakuna mtu yoyote aliyewahi kudai kuwa na sifa hiyo maalumu isipokuwa wao tu. Hivi pundi tutakunukulieni baadhi ya mifano ya hadithi hizo za Mtume Mtukufu (saw).

***********

Sheikh Swaduq amenukuu katika kitabu cha Kamal ad-Deen wa Tamam an-Ni’ma hadithi iliyonukuliwa na Sahaba mwema Jabir bin Abdallah an-Answari akisema: ‘Mwenyezi Mungu alipoteremsha aya ya: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Nilisema, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tumemjua Mwenyezi Mungu na Mtume wake, sasa ni nani hawa Ulil Amr ambao Mwenyezi Mungu amefungamanisha utiifu kwao na utiifu kwake?

Akasema (sa): Wao ni makhalifa wangu - ewe Jabir! – Na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa mwanzo wao ni Ali bin Abi Talib, kisha al-Hassan, kisha al-Hussein, kisha Ali bin al-Hussein, kisha Muhammad bin Ali ambaye ni mashuhuri katika Torati kwa jina la al-Baqir na utakutana naye ewe Jabir! Na utakapokutana naye basi mpe salamu zangu. Kisha akasema (saw): Kisha, as-Swadiq Ja’ffar bin Muhammad, kisha Musa bin Ja’ffar, kisha Ali bin Musa, kisha Muhammad bin Ali, kisha Ali bin Muhammad, kisha ak-Hassan bin Ali, kisha aliye na jina na kunia kama yangu, Hujja ya Mwenyezi Mungu kwenye ardhi yake na bakisho lake kwenye waja wake (Imam Mahdi (AF)) Ibn al-Hassan bin Ali. Huyo ndiye ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atakomboa Mashariki na Magharibi mwa ardhi kupitia kwake, huyo ndiye ataghibu machoni pa Mashia na mawalii wake, ghaiba ambayo hakuna atakayethubutu kuzungumzia uimamu wake isipokuwa yule ambaye Mwenye Mungu atakuwa ameutahini moyo wake kwa imani.

Jabir akasema: Nikamwambia, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, Mashia watanufaike naye wakati wa kughibu (kutoweka) kwake? Akasema (saw): Naapa kwa jina la yule aliyenipa utume! Hakika wao watanufaika na nuru yake pamoja a wilaya yake katika ghaiba yake kama wanavyonufaika na jua hata kama litakuwa limefunikwa na mawingu. Ewe Jabir! Hizi ni siri za Mweyezi Mungu ambazo ziko kwenye hazina ya elimu ya Mwenyezi Mungu basi usizitoe ila kwa watu wanaofaa.’

************

Ndugu wasikilizaji, Kuna hadithi nyingi sana za Mtume Mtukufu (saw) zilizonukuliwa katika vitabu vya kuaminika ambazo zinathibitisha wazi kwamba Maimamu wa Nyumba ya Mtukufu huyo ni kumi na wawili ambao (as) ni misdaki na maana halisi ya Ulil Amr na ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amefungamanisha utiifu kwao na utiifu kwake pamoja na Mtume wake Muhammad (saw). Ni wazi kuwa madhumuni ya hadithi hizi yamezidi kiwango cha tawatur yaani wingi wa hadithi zinazozungumzia jambo fulani mahususi. Na miongoni mwa wanazuoni wa kale waliokusanya hadithi kuhusiana na suala hili ni al-Hafidh al-Khazaz ambaye ni katika wataalamu wa masuala ya hadithi walioishi katika karne ya nne hijiria. Amekusanya hadithi hizo katika kitabu chake chenye thamani kubwa cha ‘Kifayat al-Athar fi al-Aimat al-Ithnei Ashar.’

Na miongoni mwa wanazuoni wa zama hizi waliokusanya hadithi hizo ni Ayatullah as-Sheikh Lutfullah as-Swafi ambaye amekusanya hadithi zipatazo 270 kutoka vyanzo tofauti vya kuaminika katika kitabu cha Muntakhab al- Athar fi al-Imam at-Thany Ashar. Hii ni mbali na vitabu vingine vingi muhimu  kama vile Abaqaat al-Anwaar  na Mulhaqaat Ihqaaq al-Haq ambavyo vinatoa hoja ya kuyakinisha kwamba kusudio la pekee na halisi la Ulil Amr katika aya tukufu tuliyoizungumzia mwanzoni ni Maimamu wa Nyuma ya Mtume Mtukufu (saw).

Na katika kipindi kijacho wapenzi wasikilizaji tutakunukulieni Inshallah hadithi nyingine tukufu ambazo zinazungumzia suala hili kwa uwazi zaidi.

Kwa kutilia maanani kwamba muda uliotengewa kipindi hiki umefikia ukingoni, tunakushukuruni nyote kwa kutenga wakati wa kusikiliza kipindi hiki mabacho kimekujieni kupitai Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mtajiunga nasi juma lijalo kusikiliza kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain. Basi hadi wakati huo tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.