Jumanne, Agosti 23, 2022
Leo Jumanne tarehe 25 Muharram mwaka 1444 Hijria, sawa na Agosti 23 mwaka 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1349 iliyopita, yaani tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, alifariki dunia Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Imam Sajjad au Imam Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein bin Ali (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (swa). Imam Zainul Abidini alifariki dunia mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38. Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe wa mwendelezo wa malengo ya baba yake, Imam Hussein (as). Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha utamaduni wa Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na Suna za Mtume Muhammad (saw), jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa hai Qur'ani na Suna za Mtume. Imam Zainul-Abidin alifahamika kwa uchamungu mkubwa na alikuwa mwingi wa kusujudu na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

Siku kama ya leo ya tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani inatambuliwa kuwa ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali bin Sina na inatambuliwa kuwa ni Siku ya Daktari hapa nchini. Abu Ali Sina mwanafalsafa na tabibu mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani aliyejulikana pia kwa laqabu ya Sheikhul Rais alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Msomi na tatibu huyo mashuhuri wa Kiislamu alijifunza tiba baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.
Miaka 191 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 25 Muharram 1253 Hijria Qamaria
"Kaghez Akhbar", gazeti la kwanza la Iran, lilichapishwa. Gazeti hili lilichapishwa na Mirza Saleh Shirazi katika kurasa mbili kubwa zenye maandishi lithografia mjini Tehran. Gazeti hilo lilisambazwa mara moja kwa mwezi na lilichapisha habari kuhusu mji wa Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki. Nakala pekee iliyopo ya karatasi hiyo imehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Uingereza.
Siku kama ya leo, miaka 78 iliyopia, mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.
Miaka 24 iliyopita katika siku hii sawa na ya kwanza ya Shahrivar mwaka 1377 Hijria Shamsia:
Mpiganaji wa mapinduzi na mmoja wa wanachama wakuu wa Chama cha Muungano wa Kiislamu "Sayyid Asadollah Lajevardi" aliuawa shahidi na kundi la munafiqin. Seyed Sayyid Asadollah Lajevardi alizaliwa mjini Tehran mwaka 1314 Hijria. Akiwa kijana, aliacha shule ya upili na kuanza kufanya kazi na baba yake. Baadaye, alijiunga na chuo cha kidini. Kuanzia mwanzo wa harakati ya Kiislamu ya wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini, Shahidi Lajevardi naye alijiunga na mwenendo huo na akawa na nafasi muhimu katika kuanzishwa kwa jumuiya za muungano wa Kiislamu mwaka 1341. Pamoja na mashahidi Beheshti na Motahari, aliamua kuunda muungano dhidi ya serikali na alifanya jitihada kubwa katika uwanja huu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Sayyid Asadollah Lajevardi aliteuliwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mapinduzi ya Kiislamu. Uteuzui huo ulifanywa na Shahidi Dakta Beheshti aliyekuwa mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran wakati huo. Baada ya hapo akawa mkuu wa shirika la magereza nchini humo. Kundi la munafiqina lilijaribu kumuua mara nyingi hadi akauawa shahidi na mnafiki mamluki akiwa na umri wa miaka 63 mahali pake pa kazi katika soko la Tehran mnamo tarehe ya kwanza ya Shahrivar 1377.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.