Jumatano 24 Agosti 2022
Leo ni Jumatano tarehe tarehe 26 Muharram 1444 Hijria Qamaria sawa na tarehe 24 Agosti 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita katika siku hii ya 26 ya Muharram 64 Hijiria Qamaria:
Mji mtakatifu wa Makka ulizingirwa na askari wa Yazid bin Muawiya, mtawala katili wa ardhi za Kiislamu. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS na masahaba zake huko Karbala na kutekwa kwa Ahlul-Bayt na manusura wao, Yazid ibn Muawiya alipoteza itibari na thamani sambamba na kudharauliwa na Waislamu. Kwa upande mwingine, ufichuzi uliofanywa na Ahul Bayt AS na waungaji mkono wao ulipelekea umma kuanzisha harakati dhidi ya serikali ya Yazid. Kwa sababu hii, katika mwaka wa 63 Hijria Qamaria, kulikuwa na uasi na harakati dhidi ya Yazid huko Hijaz. Huko Makka, Abdullah ibn Zubair aliwakusanya watu kumpinga Yazid bin Muawiya, na taratibu akapata nguvu na kuweza kuutoa mji wa Makka kutoka mikononi mwa Yazid. Baadaye majeshi ya Syria yaliivamia Makka na kuuzingia mji huo. Abdullah bin Zubair na watu wengi walikimbilia Masjid al-Haram ili kujilinda kutokana na hujuma ya maadui, lakini maadui waliulenga kwa mawe Masjid al-Haram na Kaaba. Hatimaye, Yazid alifariki Rabi al-Awwal mwaka huo huo, na majeshi ya Syria yakaondoka Makka, kisha Abdullah ibn Zubair akachukua jukumu la kusimamia masuala ya Hijaz.

Miaka 421 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.

Miaka 44 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha.

Na siku kama leo miaka 31 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake.