Aug 30, 2022 06:40 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (48)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri. Kipindi chetu kilichotangulia kilimzungumzia Mirza Abul-Qassim Gilani mashuhuri kwa jina la Mirza Qumi. Tulisema kuwa, Mirza Abul-Qassim aliishi katika zama za wafalme wa Qajar nchini Iran Agha Muhammad Khan na Fat-h Ali Shah. Moja ya sifa na tabia mashuhuri ya Mirza Abul-Qassim ni kuzingatia sana suala la kutoa nasaha, kutoa miongozo na kuamrisha mema na kukataza mabaya. Sehemu ya 48 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia msomi na mwanazuoni mwingine wa Kishia aliyeishi katika karne ya 13 Hijria ambaye ni Sayyid Ali Tabatabai, mashuhuri kwa lakabu ya Swahib Riyadh. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Sayyid Ali Tabatabai, alimu na fakihi mtajika wa karne ya 13 Hijria alizaliwa mwezi Rabiul-Awwal 1161 Hijria katika mji wa Kadhmein, Iraq. Babu yake ni Abul-Muali mmoja wa masharifu wakubwa ambao ukoo wao unaishia kwa  Imam Hassan Mujtaba katika mji wa Isfahan Iran ambaye alihajiri kuelekea Karbala Iraq. Babu yake ametoa huduma kubwa kwa jamii ya Mashia. Mama yake ni dada wa Allama Wahid Bahbahani. Sayyid Ali Tabatabai alianza kusoma masomo ya dini mwanzoni mwa ujana wake na katika kipindi cha muda mfupi tu alidhihirisha kipaji kikubwa alichokuwa nacho na hivyo kumfanya Allama Bahbahani avutiwe naye. Allama Bahbahani ambaye alikuwa mjomba wa Sayyid Ali Tabatabai alimtaka mwanawe yaani Muhammad Ali Bahbahani aliyekuwa mmoja wa walimu wa Hawza wakati huo achukue jukumu la kumfundisha Sayyid Ali elimu ya fikihi.

Picha inayonasibishwa na Sayyid Ali Tabatabai, mashuhuri kwa lakabu ya Swahib Riyadh

 

Baada ya kitambo kidogo, Sayyid Ali aliyekuwa kijana mwenye hima na juhudi kubwa masomoni alifanikiwa kuanza kusoma pamoja na mwalimu huyo na kuwa mwanafunzi mwenzie na hivyo wote wakawa wakishiriki pamoja darsa za Allama Wahid Bahbahani. Haukupita muda, Sayyid Ali akafanikiwa kupata daraja ya juu kabisa katika masomo ya dini yaaani Ijtihadi.

Akiwa katika njia ya kutafuta elimu, Sayyid Ali ambaye ni mashuhuri kwa jina la Swahib Riyadh alipata taabu na mashaka mengi. Hata hivyo hayo yote hayakuweza kumkatisha tamaa na kumfanya aachane na njia aliyoichagua ya kutafuta elimu.

Inanukuliwa kuwa, kutokana na shauku na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo ya kutafuta elimu, daima katika dua na minong'ono yake na Mwenyezi Mungu alikuwa akimuomba na kumtaaradhia ampe tawfiki katika masomo na utafutaji elimu. Wasomi na wanazuoni wakubwa wanaamini kwamba, mafanikio ya Sayyid Ali yalitokana na dua hizo, hasa kwa kuzingatia kwamba, muda aliosoma ulikuwa ni mdogo sana hata akwee na kufikia daraja ya juu ya elimu namna hii.

 

Sayyid Ali Tabatabai alikuwa mahiri mno katika elimu ya fikihi, Usul na hadithi. Hata hivyo alikuwa ametabahari zaidi katika elimu ya Usul-Fikih ikilinganishwa na elimu zingine. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akaandika kitabu cha Sahib Riyadh na kuondokea kuwa mashuhuri kwa jina hilo.

Kama ilivyokuwa kwa Maulamaa wengine wakubwa wa Kiislamu, Sayyid Tabatabai naye alifanya hima na idili kubwa katika kubainisha na kueneza mafundisho ya dini ya Kiislamu. Alitumia nguvu zake zote kuhudumia Uislamu. Harakati muhimu za msomi huyu katika uwanja huu ni kulea na kuandaa wanafunzi ambao waliondokea kuwa wasomi na wanazuoni wakubwa wa Kiislamu. Akitelekeza agizo la mwalimu wake yaani Wahid Bahbahani, msomi huyu alijishughulisha na kazi ya kufundisha katika mji wa Karbala, Iraq. Wasomi wakubwa katika zama hizo walikuwa wakihudhuria darsa zake na hivyo kufanikiwa kutoa wanafunzi wengi wasomi na mahiri katika taaluma mbalimbali.

Mbali na kazi ya kufundisha na kulea wanafunzi, Sayyid Ali Tabatabai hakuwa nyuma pia katika taaluma ya kualifu na kuandika vitabu, kwani amevirithisha vitabu vingi vizazi vilivyokuja baada yake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni "Riyadh al-Masail Fi Bayan al-Ahkam Bidalail" (ریاض المسائل فی بیان الاحکام بالدلائل ) ambacho kinajulikana zaidi kwa jina la Riyadh al-Masail. Kitabu hiki kisicho na mithili na muhimu ni sherhe na ufafanuzi wa kitabu cha Mukhtasar al-Nafi'i kilichoandikwa na Muhaqqiq wa Kwanza. Ndani ya kitabu hiki kuna nadharia na mitazamo ya kifikihi ya wasomi na Maulamaa wakubwa wa Fikihi kama Sheikh Tusi, Sheikh Saduq, Allama Hilli, Shahidi wa Kwanza, Shahidi wa Pili, Qadhi Said al-Ddin, Sheikh Kulayni, Muhammad Baqir Sabzawari, Tabarsi, Rawandi, Fadhil Miqdad, Fakhrul-Muhaqqiqin, Muqaddas Ardebili na wengineo.

Kitabu kingine muhimu cha Sayyid Ali Tabatabai ni Risat al-Bahiyah ambacho ni radiamali na majibu kwa nadharia za mrengo wa Akhhbariyun unaoamini kwamba, dhahiri ya hadithi inatosha kwa ajili ya kufahamu maamrisho na maagizo ya dini na hivyo hakuna haja ya kumkalidi na kumfuata Marjaa. Hii ni katika hali ambayo, mkabala na kundi hilo, kuna mrengo wa Usuliyun ambao unaamini kwamba, ili kuainisha kwa njia sahihi hukumu za dini, ni lazima mtu awe na utaalamu na ubobezi wa kielimu na kuna haja ya kuweko watu ambao kutokana na umahiri na kutabahari kwao kwa vyanzo vya dini na kwa kutumia mbinu makini ya kielimu na kiakili wanyambue hukumu za dini kuhusiana na masuala mbalimbali. 

 

Wakati alipofikia daraja ya Marjaa Taqlidi, Swahib Riyadh alikuwa akiletewa na watu Khumsi na Zaka. Alitumia Khumsi na Zaka hizo katika huduma za kijamii na mambo ambayo yana maslahi jumla kwa umma. Alinunua nyumba na maeneo mengi kwa ajili ya wahitaji kando kando ya mji wa Karbala na kuyafanya kuwa Wakfu kwa ajili ya masikini na wasiojiweza. Miongoni mwa mambo mengine aliyoyafanya akitumia Khumsi na Zaka ni kujenga maeneo ya kidini, kuyakarabati au kuyapanua. Mfano wa wazi ni ujenzi wa Msikiti wa Jamia wa Karbala. Msikiti huu upo jirani na soko kubwa la Karbala na ujenzi wake ulikamilika mwaka 1220 Hijria.

 

Moja ya sifa iliyokuwa ikimtofatisha sana Sayyid Ali Tabatabai na Maulamaa wengine wa zama zake ni akhlaqi ya hali ya juu na tabia njema aliyokuwa nayo, pamoja na kushikamana kwake vilivyo na masuala ya kimaanawi. Alikuwa makini sana katika kuchunga na kuheshimu haki za wengine na alikuwa akiwashajiisha na kuwahimiza wengine juu ya jambo hili.

Hatimaye mwanazuoni huyo mkubwa wa Kishia aliaga dunia mwaka 1231 huko Karbala Iraq baada ya kuishi kwa miaka 70, umri ambao ulijaa baraka na huduma yenye ikhlasi kwa maktaba ya Ahlul-Baiti (as). Sayyid Ali Tabatabai amezikwa jirani na kaburi la Allama Wahid Bahbahani.

Muda nao wa kipiindi hiki kwa juma hili unafikia tamati, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya safari yetu hii ya kutupia jicho historia na maisha ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.