Sep 30, 2022 01:02 UTC
  • Ijumaa tarehe 30 Septemba 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Septemba 2022.

Siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 8 Mehr, ni maarufu hapa nchini Iran kama siku ya kumuenzi Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi. Maulana Jalaluddin alizaliwa mwaka 604 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh uliokuwa moja kati ya miji ya Iran ya kipindi hicho. Moulavi alikuwa gijwi wa mashairi na malenga mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Maanavi.

Tarehe 3 Rabiul Awwal miaka 1003 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa al Ma'arri. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Ma'arri

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani.

Mkutano wa kihistoria wa Munich

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.

Bendera ya Namibia

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.

Charles Richter

Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina hilo ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.