Oct 08, 2022 02:18 UTC
  • Jumamosi, 08 Oktoba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1444 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Oktoba 2022 Miladia.

Siku kama ya miaka 151 iliyopita kwa mujbu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allama Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. ***

Allama Agha Bozorge Tehrani (wa katikati)

 

Miaka 141 iliyopita katika siku kama ya leo, kimbunga kikubwa kilitokea nchini Vietnam, Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tufani hiyo kubwa yalikuwa ya kusini mwa nchi hiyo. Kimbunga hicho kiliharibu mashamba na kubomoa kikamilifu nyumba za maeneo ya kusini mwa Vietnam. Aidha kufuatia janga hilo la kimaumbile, zaidi ya watu 300,000 waliaga dunia. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania. Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake. Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo. ***

Vita vya kwanza vya Balkan

 

Miaka 94 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya udikteta wa Reza Khan Pahlawi, mtawala huyo aliwaamuru askari wake wavamie nyumba ya Ayatullah Muddares, kumpiga na kumjeruhi na kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran. Askari hao pia waliwatia nguvuni watu wa familia ya mwanazuoni huyo. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Reza Khan mwaka 1316 Hijiria Shamsia. ***

Sayyid Hassan Mudarres

 

Katika siku kama ya leo miaka 90 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hassan Sadr mmoja wa maulama mahiri wa Kiislamu. Alikuwa mmoja wa mafakihi ambao walipata daraja ya Ij’tihad katika kipindi cha ujana. Sayyid Hassan Sadr alikuwa katika orodha ya walimu mashuhuri katika Chuo KIkuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sadruddin katika elimu ya fikihi, Usul, Itikadi, falsafa na hadithi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Sayyid Hassan Sadr ni Tahsil al-Furu’u al-Diniyyah fi Fikih al-Imamkiyah na Taasis al-Shiyah. ***

Sayyid Hassan Sadr

 

Na miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu wapatao 90 elfu walipoteza maisha yao na wengine milioni 3 na laki 6 kubaki bila makazi kufuatia mtetemeko huo. ***

Tetemeko la Pakistan