Oct 12, 2022 02:37 UTC
  • Jumatano tarehe 12 Oktoba 2022

Leo ni Jumatano tarehe 15 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Oktoba 2022.

Leo tarehe 20 mwezi wa Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan. 

Tarehe 12 Oktoba miaka 530 iliyopita mvumbuzi na baharia wa Kitaliani, Christopher Columbus alivumbua bara la America. Columbus alianza safari yake ya baharini kwa kutumia merikebu tarehe 3 Agosti mwaka 1492 kutoka kwenywe bandari ya Palos nchini Uhispania akielekea kwenye Bahari ya Atlantic. Baharia huyo hakujua kwamba anaelekea bara America na kwa msingi huo tarehe 12 Oktoba 1492 na baada ya safari ya siku 70 baharini alipoona nchi kavu kwa mbali alidhani kuwa anakaribia Asia, kwa sababu alikua akiamini kwamba ardhi ina umbo la mviringo. Kwa msingi huo Christopher Columbus alivipa visiwa alivyokuwa amegundua jina la India ya Magharibi.

Christopher Columbus

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais. 

Jenerali Parviz Musharraf,

 

Tags