Oct 20, 2022 00:43 UTC
  • Alkhamisi tarehe 20 Oktoba 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Rabiul Awwal 2444 Hijria sawa na Oktoba 20 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1243 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kutoka Madina kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka na Imam wake huko Khorasani. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake  Imam Ridha (as), Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo Haram ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatma Maasuma (as) katika mji wa Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia huenda kufanya ziara katika eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya ziliangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita.

Vita vya Ghuba ya Navarone

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture". John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.

John Dewey

Miaka 70 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.

Jomo Kenyatta

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani alimu na mwanazuoni mchamungu. Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa imeshikamana kikamilifu na dini. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali alielekea katika mji wa Qum, Iran na baadaye Najaf huko Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika huko Ayatullah Tehrani alihudhuria darsa na masomo ya walimu mahiri wa zama hizo. Miongoni mwa sifa alizopambika nazo Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani ni uchamungu, kuipa mgongo dunia na mapenzi yake makubwa kwa Ahlul Bait (as). Msomi huyo wa Kiislamu hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu. 

Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.

Muammar Gaddafi