Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 9 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na tarehe 4 Novemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alimu na msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu. Ayatullah Nahavandi alibobea katika elimu ya fiqhi na usulu fiqhi, na kutokana na hali hiyo wasomi wengi wa Iraq na Iran waliweza kustafidi na elimu yake. Inafaa kufahamisha kwamba, Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alizaliwa katika mji wa Nahavand, ulio magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo hususan Sheikh Murtadha Answari, ambapo kwa kipindi cha miaka 30 alijikita katika shughuli ya ufundishaji wa sheria za Kiislamu.

Katika siku kama hii ya leo miaka 140 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58, Ayatullah Sayyid Haidar Hilli. Abul-Hassan Sayyid Haidar Bin Sulaiman Bin Daud Hilli Husseini, ni miongoni mwa malenga na viongozi mashuhuri wa fani hiyo katika zama hizo. Ufasaha na uwezo mkubwa wa kiimani aliokuwa nao, vilimsukuma katika kuwasifu Ahlu Baiti wa Mtume (saw) kupitia mashairi yake. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'ad-Duraru-Yatim' na 'al-Aqdul-Mufaswal.'

Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufalme wa Austria-Hungary ulisalimu amri kwa Waitifaki wiki moja tu kabla ya kufikia tamati Vita vya Kwanza vya Dunia. Utawala huo ambao ndio uliokuwa umeanzisha vita, ulikuwa ukihesabiwa kuwa muitifaki muhimu wa Ujerumani. Hata hivyo kutokana na kushindwa mara nyingi katika vita, ulikubaliana na masharti ya kuacha vita. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Austria-Hungary uligawanywa kwa nchi kadhaa na ukoo wa Habsburg uliokuwa ukitawala ukasambaratika.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Miaka 44 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi."

Siku kama ya leo 43 iliyopita, wanafunzi na wanachuo wa Tehran walifanya maandamano makubwa katika mji huo kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kupelekwa uhamishoni nchini Uturuki Imam Khomeini MA na kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa wanafunzi na wanachuo wa Iran. Mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah. Wanafunzi na wanachuo kadhaa wa Kiislamu walioshiriki kwenye maandamano hayo ambao walikuwa wakijulikana kama Wafuasi wa Sera za Imam, waliuvamia ubalozi wa Marekani mjini Tehran, ambao ulikuwa pango la ujasusi dhidi ya wananchi wa Iran.
Miaka 27 iliyopita katika siku kama hii ya leo Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliuawa na Mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada. Rabin alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kuanzia mwaka 1974 hadi 1977 kwa tiketi ya Chama cha Leba. Hata hivyo aliuzuliwa wadhifa huo kwa tuhuma za ubadhirifu. Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.