Akhlaqi Katika Uislamu (6)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya sita ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu ambapo leo tutafanya uhakiki wa ukosoaji wa kulinganisha mitazamo miwili katika uga wa akhlaqi.
Wa kwanza ni ule unaomzingatia mtu binafsi kama asili na mhimili mkuu wa kila jambo, na ule unaoizingatia jamii kama mhimili mkuu wa mambo yote. Endelea kuwa name basi hadi tamati ya mazungumzo yetu, kusikiliza niliyokuandalia kwa leo.
Kabla ya kuendelea mbele mpendwa msikilizaji, nikukumbushe kwanza na kwa muhtasari ya kwamba, katika vipindi kadhaa vilivyopita tumechambua na kuzungumzia baadhi ya vielezi vya akhlaqi katika utamaduni wa Kiislamu. Vielezi hivyo ni kuitambua mtu nafsi yake kiutu na kimaanawi, kufanya kila tendo la kiakhlaqi kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu, kuzirasimisha thamani na tunu za kiakhlaqi na kiutamaduni, kuendana kwake na fitra na kiu ya kutaka kumjua Mwenyezi Mungu, kufaidika na utaalamishaji wa Mitume, kuendana kwake na urazini na mantiki, kujiweka mbali na hawaa na wasiwasi wa shetani na kuwa na bidii na idili ya kutunza hadhi na daraja ya ukhalifa na heshima aliyopewa mwanadamu na Allah ili kuweza kufikia vilele vya ukamilifu kwa kutegemea imani juu ya Allah na imani juu ya kufufuliwa. Kwa kujengeka na imani hizo, kwa upande mmoja mwanadamu hutambua kuwa Mwenyezi Mungu yuko haadhir na anashuhudia amali na matendo yake; na kwa upande mwingine huwa na yakini kwamba yote aliyotenda hapa duniani yatakwenda kuhesabiwa na kulipwa katika mahakama ya uadilifu ya Allah Siku ya Kiyama.

Sifa hizi maalum ambazo ni jumuishi, za kimantiki na zenye misingi imara, ndizo zinazokifanya chuo cha akhlaqi cha Uislamu kiwe na ubora na upekee kulinganisha na nadharia nyingine za akhlaqi duniani. Ili kuthibitisha dai hili, hebu na tuihakiki sasa na kuichambua mitazamo ya nadharia hizo.
Mtazamo unaokubaliwa na wanafikra wengi mpendwa msikilizaji ni kwamba thamani na tunu za kiakhlaqi ndizo zinazoyapa afya na uhai mataifa; na jamii zinazokosa kuchunga na kufuata matukufu ya kiakhlaqi huwa zinapotoka na kuporomoka. Lakini wakati huohuo, kuna tapo la wanaojiita wanafalsafa, wakiwemo waliotangulia na wa sasa ambao mtazamo wao ni kwamba ‘starehe’ ndicho kipaumbele cha maisha ya mtu. Kwa mtazamo wa watu hao, kuzikamata barabara thamani za kiakhlaqi na tabia njema kunamnyima mtu fursa ya kujistarehesha kwa raha na matamanio yake ya nafsi ya kupita na hivyo wanashikilia mtazamo na dhana potofu kwa kusema, kuna haja na ulazima gani wa mtu kujinyima raha na anasa nyingi zilizopo katika kipindi kifupi tu cha umri na uhai alionao? Qur'ani inawaelezea watu hao kuwa ni washughulishwaji wa mapambo, anasa na vitu vya kidhahiri tu vya maisha, lakini wameghafilika na ulimwengu wa akhera. Hawana imani yoyote juu ya dunia ya baada ya kifo na hivyo wanafanya kila wawezalo ili kujistarehesha kwa raha na anasa za dunia hii.
Katika kuuhakiki kiukosoaji mtazamo huu tunaweza kusema kuwa, mwanadamu hakuumbwa bila ya lengo; hata awe sawa na wanyama wa miguu minne ambao wanashughulika kujitafutia chochote wapatacho machungani kulingana na utashi wao bila ya kuwajibika kwa lolote lile. Imam Ali AS anaukosoa na kuubatilisha mtazamo huo kwa kusema: "Hata kama tutakuwa hatuna matarajio ya Pepo wala khofu ya Moto, basi itastahiki tujipambe kwa sifa za akhlaqi njema.” (Mustadrakaul Wasaail, Juzzu ya 11, ukurasa wa 193).

Akili na fitra, yaani maumbile timamu ya mwanadamu, havikubaliani na dhana ya mtu kuwa huru mutlaki na kujistarehesha na anasa zisizo na mipaka; na vinaafiki mtazamo wa kwamba ili mwanadamu atukuke na kufikia ukamilifu, kuna haja ya kujiwekea mipaka ya kimantiki na kutoitoa kafara heshima na utukufu wake wa kiutu, na kuifanya mhanga wa hawaa na matamanio yasiyo na udhibiti ya nafsi yake, ambayo hayana hatima nyingine ghairi ya majuto; ni kama wasemavyo wahenga “raha ni ya kupita, lakini majuto ni ya milele.”
Nadharia nyingine inayozungumziwa katika uga wa akhlaqi ni ya akhlaqi zinazompa kipaumbele mtu katika kila jambo. Chimbuko la mtazamo huu ni ulimwengu wa Magharibi na katika nadharia ya Ubepari inayoitakidi kuwa, katika jambo lolote lile, kuamua kufanya au kutofanya suala lolote la kiakhlaqi, inapasa kila mtu awe huru kufanya atakalo bila kuwekewa mpaka wala kushurutishwa, ili kuhakikisha anaburudika na kujistarehesha na maisha vyovyote apendavyo, pasi na kujikhini na kujinyima raha na starehe yoyote kubwa iliyopo. Hakika ya mtazamo huu ni kujali maslahi ya mtu binafsi, mpaka kufikia hadi kwamba, utokeapo mgongano kati ya manufaa ya mtu binafsi na jamii, basi hutangulizwa mbele manufaa ya mtu; na inapolazimu hujuzishwa hata kukiuka haki za wanajamii wengine.
Kinyume na watetezi wa nadharia hii, kuna kundi jengine la wanaoamini kuwa jamii ndiyo inayostahiki kupewa kipaumbele katika masuala ya akhlaqi; na kwa hivyo linasisitiza kupangwa na kutekelezwa masuala hayo kwa namna itakayoendana na matakwa ya waliowengi katika jamii. Hata kama mtazamo huu unafadhilisha na kutanguliza manufaa ya jamii badala ya mtu binafsi katika akhlaqi, lakini kasoro yake ya msingi ni kwamba, suala la haki na batili katika akhlaqi huwa halina umuhimu mkubwa kwake. Kitu kipekee kinachopiganiwa na nadharia hiyo ni kuhakikisha masuala yote ya kiakhlaqi yanaendana na matashi na matakwa ya wanajamii; na hivyo inajaribu kutumia kila njia iwezekanayo ili kufanya yale yatakayoiridhisha jamii.
Misingi na thamani za akhlaqi za Uislamu hazikubaliani na mitazamo yote hii miwili, kwa sababu zinaitakidi kuwa viwili hivyo vimechanganyika pamoja na kwamba mitazamo na miono ya kiakhlaqi ya mtu binafsi na ya jamii inaathiriana; na ujengekaji wa shakhsia ya akhlaqi za mtu binafsi na jamii hauwezi kutenganika.
Muhimu zaidi ya hilo ni kwamba, Uislamu unaikubali hoja ya kudhamini maslahi ya mtu na jamii, lakini ni pale kufanya hivyo kusipochochewa na hawaa za nafsi na matashi ya kishetani, bali kukachukua ilhamu ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu na wa kiutu. Na ndiyo maana katika aya ya 116 ya Suratul- An’am Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumpa tahadhari ya kutofuata matashi na matamanio ya walio wengi alipomwambia: “Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu.”

Kwa maelezo hayo ya aya ya 116 ya Suratul An’am mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya sita ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya saba ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/