IRGC yaitungua ndege ya kivita ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi, yatoa onyo kali
-
Jeshi la IRGC
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa vitengo vyake vya ulinzi wa anga vimetungua ndege ya kivita ya Marekani isiyo na rubani, aina ya MQ-9 Reaper, katika anga ya Ghuba ya Uajemi.
Katika taarifa IRGC imetoa onyo kali kuwa ukiukaji wowote wa makubaliano ya kusitisha mapigano utakaofanywa na Marekani utakabiliwa na jibu kali.
Idara ya Uhusiano wa Umma ya IRGC, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne hii, imesema kuwa “jeshi la kigaidi” la Marekani, katika mwendelezo wa “chokochoko za kuingilia kati na tabia za uchokozi katika eneo hili,” limeingia kinyume cha sheria katika anga la Iran juu ya maji ya Ghuba ya Uajemi.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa vitengo vya ulinzi wa anga vya IRGC, kufuatia ufuatiliaji makini wa kijasusi, vimefanikiwa kuitungua ndege hiyo ya MQ-9 Reaper wakati vikiwa katika jukumu la kulinda mamlaka ya anga la nchi hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa vikosi vya ulinzi wa anga vya IRGC pia vilivifyatulia risasi na kutimua ndege zingine mbili. Ya kwanza ilikuwa ndege ya ujasusi ya RQ-4 Global Hawk na ndege ya kisasa ya kivita ya F-35, na kuzilazimu kutoroka na kuondoka katika anga la Iran.
Mwishoni mwa taarifa yake, IRGC imeonya dhidi ya ukiukaji wowote wa usitishaji vita utakaofanywa na “jeshi vamizi la Marekani,” ikisisitiza kuwa Iran inachukulia hatua za kulipiza kisasi na mashambulizi ya kisheria kama haki yake ya msingi na isiyopingika.
Tukio hili limekuja baada ya msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), Timothy Hawkins, kudai kuwa vikosi vya Marekani vilitekeleza mashambulizi kusini mwa Iran “kwa ajili ya kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitisho vya vikosi vya Iran.” Aliongeza kuwa shabaha zao zilikuwa ni pamoja na maeneo ya kurushia makombora na pia boti za Iran zilizodaiwa kujaribu kutega mabomu ya majini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa uchokozi wowote wa kigeni katika eneo hili, hususan katika Lango muhimu la Hormuz , unahatarisha usalama wa safari za kimataifa za majini na usalama wa nishati duniani, na utajibiwa kwa uthabiti na kwa kiwango kinachostahiki na vikosi vya ulinzi vya Iran.