Jeshi la Sudan lazuia shambulio la RSF huko Blue Nile
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138880-jeshi_la_sudan_lazuia_shambulio_la_rsf_huko_blue_nile
Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limezima shambulio la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwenye eneo la kimkakati la Al-Baraka nje kidogo ya mji wa Kurmuk katika Jimbo la Blue Nile, kusini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-06-04T11:21:38+00:00 )
Jun 04, 2026 11:19 UTC
  • Jeshi la Sudan
    Jeshi la Sudan

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limezima shambulio la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwenye eneo la kimkakati la Al-Baraka nje kidogo ya mji wa Kurmuk katika Jimbo la Blue Nile, kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya Jeshi la Sudan imeeleza kwamba vikosi vyake vimesababisha hasara kubwa kwa "wanamgambo waasi," ikiwa ni pamoja na kuangamiza makumi ya waasi hao, kuharibu idadi kubwa ya magari ya kivita, na kuwakamata mateka wengine. RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu taarifa hiyo ya Jeshi al Sudan.

Chanzo cha Jeshi la Sudan mapema kilisema vikosi vya jeshi vimekomboa mji wa Al-Baraka katika jimbo la Kurmuk la eneo la Blue Nile, saa chache baada ya wapiganaji wa RSF kuudhibiti, kufuatia mapigano makali yaliyoshirikisha silaha nzito.

Eneo la Al-Baraka lina umuhimu wa kistatijia likiwa sehemu muhimu ya usambazaji wa misaada na makutano ya barabara kuu za kusini za Jimbo la Blue Nile, ambalo linapakana na Ethiopia.

Mnamo Mei 24, Jeshi la Sudan lilitangaza kwamba limekomboa eneo la Al-Baraka karibu na mji wa Al-Karmak.

Waasi wa RSF na Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini (SPLM-N) waliudhibiti mji wa Kurmuk mwishoni mwa mwezi Machi, kama sehemu ya juhudi za kupanua ushawishi wao kwenye miji ya Jimbo la Blue Nile linalopakana na Ethiopia.

Tangu Aprili 2023, waasi wa RSF wamekuwa wakipigana na jeshi la Sudan suala lililosababisha mauaji ya makumi ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.