Mgawanyiko waongezeka kati ya Rais wa Senegal na Waziri Mkuu wa zamani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138876-mgawanyiko_waongezeka_kati_ya_rais_wa_senegal_na_waziri_mkuu_wa_zamani
Mvutano kati ya Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal na mshauri wake wa zamani, Ousmane Sonko umezusha mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi inayosumbuliwa na deni kubwa.
(last modified 2026-06-04T05:55:04+00:00 )
Jun 04, 2026 03:45 UTC
  • Faye na Sonko haziivi tena
    Faye na Sonko haziivi tena

Mvutano kati ya Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal na mshauri wake wa zamani, Ousmane Sonko umezusha mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi inayosumbuliwa na deni kubwa.

Siku ya Jumatatu Rais Faye alitangaza baraza jipya lenye mawaziri 30, wiki mbili baada ya kumfuta kazi Waziri Mkuu, Ousmane Sonko, kufuatia kutoelewana katika masuala mbalimbali likiwemo suala la uchumi wa Senegal unaolegalega.

Baada ya kuondolewa katika wadhifa wa Waziri Mkuu, Sonko alichaguliwa na waitifaki wake kuwa Spika wa Bunge. Ousmane Sonko pia ameendelea kuwa kiongozi asiye na mpinzani wa chama cha Pastef; chama ambacho alikianzisha mwaka 2014 ambacho Rais Faye pia anatoka.

Chama cha Pastef kinadhibiti viti 130 kati ya jumla ya viti 155 vya Bunge la Taifa la Senegal.

Sonko ameahidi kuliongoza Bunge la Senegal kwa uaminifu akisema hatatumia mamlaka yake mapya kuanzisha ghasia za kisiasa na kuonya kuwa chombo hicho cha kutunga sharia hakitahodhi madaraka.

Youssou Diallo afisa mstaafu wa taasisi ya umma amechambua mvutano unaoendelea nchini Senegal kwa kusema, anaamini Spika wa Bunge hawezi kuzuia utendaji wa serikali kwa kiasi kikubwa. Amesema, Rais ni msingi mkuu wa uongozi wa nchi, ndiye anayeongoza majeshi ya ulinzi na mwenye mamlaka ya kulivunja Bunge. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, masaa kadhaa kabla ya Rais wa Senegal kutangaza serikali mpya siku ya Jumatatu, Sonko alitangaza kuwa chama cha Pastef hakitashiriki na hakitawakilishwa na mawaziri wowote katika serikali hiyo.

Hata hivyo, waitifaki wake wasiopungua 10 na wanachama wa chama cha Pastef wameonekana katika orodha ya uteuzi wa serikali ya Rais Diomaye Faye.