IRGC: Tumejiandaa vya kutosha kwa uchokozi wa aina zote wa adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138850-irgc_tumejiandaa_vya_kutosha_kwa_uchokozi_wa_aina_zote_wa_adui
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa vikosi vyake vimejiandaa vyema kuliko hapo awali na viko tayari kikamilifu kwa dharura yoyote ya siku zijazo, likisisitiza kwamba kurudi kwa adui kwenye uvamizi wa kijeshi kutakabiliwa na mbinu tofauti za kiutendaji.
(last modified 2026-06-03T04:13:04+00:00 )
Jun 03, 2026 04:12 UTC
  • IRGC: Tumejiandaa vya kutosha kwa uchokozi wa aina zote wa adui

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa vikosi vyake vimejiandaa vyema kuliko hapo awali na viko tayari kikamilifu kwa dharura yoyote ya siku zijazo, likisisitiza kwamba kurudi kwa adui kwenye uvamizi wa kijeshi kutakabiliwa na mbinu tofauti za kiutendaji.

Msemaji wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Hossein Mohebbi amesifu uwezo na uzoefu wa jeshi hilo uliopatikana kupitia mapambano ya moja kwa moja na adui na kusema: "Iwapo adui atarudi kwenye uwanja wa vita, aina ya operesheni, jiografia ya vita, na hata aina ya silaha zitakazotumika zitakuwa tofauti."

Afisa huyo wa IRGC pia amesema Iran imetumia kipindi cha kusitisha mapigano kuimarisha utayarifu wake wa kijeshi na kurekebisha uharibifu.

"Ukweli ni kwamba katika kipindi cha kusitisha mapigano, uwezo wetu wa kijeshi na kiutendaji umeongezeka," amesema Brigedia Jenerali Hossein Mohebbi.

Mohebbi amesema moja ya matokeo makuu ya makabiliano ya hivi karibuni na adui ni uelewa wa kina zaidi wa utendaji wake.

Ameongeza kuwa vikosi vya jeshi la Iran sasa vina uelewa sahihi zaidi wa zana za kijeshi za adui, mifumo ya ulinzi wa anga, vituo vya uendeshaji wa operesheni zake na mbinu zake za mapigano.

"Maarifa ambayo hapo awali yalipatikana kwa kiasi kikubwa kutokana na tathmini za kijasusi na ripoti za vyombo vya habari sasa yameongezewa uzoefu wa makabiliano ya moja kwa moja katika uwanja wa vita", amesema Brigedia Jenerali Mohebbi.

Msemaji wa IRGC ametolea mfano wa jinsi, katika uvamizi wa hivi karibuni, Marekani imeshindwa kuvunja udhibiti wa Iran kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz licha ya kutumia uwezo mkubwa wa kijeshi.

Amesisitiza kwamba mamlaka ya Iran juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz imebaki kama ilivyo bila kubadilika na ameutaja udhibiti wa njia hiyo ya majini ya kimkakati kama ishara ya nguvu ya IRGC.