Vikosi vya jeshi la Iran: Adui amelazimishwa kukubali sheria mpya za Iran
Vikosi vya jeshi la Iran vimetangaza kuwa adui amelazimika kukubali sheria mpya zilizowekwa na Tehran kwenye uwanja wa vita, hasa kuhusu usimamizi na udhibiti makini wa Mlango-Bahari wa Hormuz, huku nchi hii ikiwa katika kumbukumbu ya kifo cha Imam Ruhullah Khomeini na mapambano ya 1963 dhidi ya utawala wa Shah.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesema katika taarifa iliyotolewa na mashirika ya habari leo Jumatano kwamba, taifa la Iran na vikosi vya jeshi vimeweka hali mpya kwenye uwanja wa vita ambayo Washington na washirika wake wanalazimika kuikubali.
"Adui analazimika kukubali sheria mpya ambazo taifa la Iran na vikosi vyake vya jeshi vimeziweka katika uwanja wa vita, hasa katika usimamizi na udhibiti makini wa Mlango-Bahari wa Hormuz," imesema IRGC.
Kauli hiyo imetolewa huku Iran ikikabiliwa na uhasama wa kijeshi wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya Jumanne jioni ya Marekani dhidi ya meli ya mafuta ya Iran na mnara wa mawasiliano kwenye Kisiwa cha Qeshm, pamoja na mzingiro unaoendelea wa jeshi la majini la Marekani dhidi ya bandari za Iran.
Kamandi Kuu ya Jeshi na Makao Makuu ya Khatamul-Anbiya zimetoa taarifa ya pamoja zikiapa kwamba Muqawama utaendelea hadi "kusambaratishwa kabisa" njama za mataifa kibeberu, kufukuzwa vikosi vya majeshi ya kigeni eneo la Asia Magharibi na kukombolewa al-Quds kwa kuangamizwa utawala wa Israel.
Taarifa hiyo imetolewa katika kumbukumbu ya kifo cha Imam Khomeini, baba wa Mapinduzi ya Kiislamu, na uasi wa Juni 5, 1963 dhidi ya nasaba ya zamani ya Pahlavi, ambao ulianza baada ya kukamatwa Imam Khomeini.
"Taifa la Iran halitarudi nyuma licha ya vitisho na uchokozi bali litaendeleza njia ya heshima kwa umoja na imani zaidi kuliko hapo awali," imeongeza taarifa ya IRGC.
IRGC pia imeashiria mauaji yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Israel dhidi ya watoto 168 katika shule ya Minab kama moja ya mamia ya uhalifu wa tawala hizo mbili, ikisema kwamba mapigano ya hivi karibuni yaliyochochewa na Washington na Tel Aviv yamefichua sura halisi ya wale wanaodai kwa uongo kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani.
Vilevile Kamandi Kuu ya Jeshi imesema maadui, Marekani na Wazayuni, hawatakuwa na chaguo ila kujisalimisha mbele ya irada ya Mungu ya vikosi vya jeshi na taifa la Iran.
Vikosi vya Jeshi, chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, vitatetea maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu na mamlaka ya taifa hadi tone la mwisho la damu, imesema taarifa hiyo.
Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia mwezi Juni 1989 akiwa na umri wa miaka 87.