Hormuz, vita na ukweli ambao Washington haikuwa na budi ila kuukubali
Katika hali ambayo sera ya "mashinikizo ya juu zaidi" na chaguo la kijeshi la Trump vilipaswa kuilazimisha Iran ilegeze msimamo na kurudi nyuma, lakini matukio ya karibuni yameonyesha kuwa Washington inatafuta njia ya kujiondoa kwa heshima katika mgogoro ambao imejianzishia yenyewe.
'Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kudai siku zote kuwa ni hodari na kiranja wa sanaa ya mapatano na miamala, lakini hivi karibuni amethibitisha kivitendo kuwa ni mwalimu wa mazungumzo yaliyofeli.' Maneno haya makali na adimu ya Kent Roth, mhadhiri na mkurugenzi mtendaji wa zamani wa Human Rights Watch, katika gazeti la Guardian ni mojawapo ya maelezo yanayobainisha wazi hali ya sasa ya sera za Marekani dhidi ya Iran. Sera ambazo zilipaswa kuilazimisha Iran "isalimu amri bila masharti yoyote" kupitia mashinikizo ya juu zaidi, vita na vitisho, lakini Washington imesukumwa katika nafasi ambayo sasa inatafuta njia ya kujinasua kwa heshima kutoka kwenye mgogoro ambao ilijianzishia yenyewe.
Donald Trump alianzisha vita hivi dhidi ya Iran kwa ushirikiano wa karibu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa mujibu wa wapangaji wa vita, uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran ulipaswa kubadilisha uwino wa nguvu katika eneo. Lengo lililotangazwa rasmi lilikuwa ni kusimamisha mpango wa nyuklia wa Iran, lakini malengo makuu yalikuwa ni kudhoofisha muundo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu, kupunguza nguvu za kijeshi za Iran na kuandaa mazingira ya kupinduliwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Pamoja na hayo kilichotokea kivitendo kilikuwa tofauti na kinyume kabisa na matarajio ya awali ya wapangaji vita. Ripoti ya The Guardian inasisitiza ukweli muhimu kwamba baada ya kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa 2015, hatimaye Trump amerejea huko huko alikouachia miaka minane iliyopita. Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, JCPOA pamoja na mapungufu yake yote, lakini iliweza kuuweka mpango wa nyuklia wa Iran chini ya uangalizi mkubwa wa kimataifa na kupunguza kiwango cha urutubishaji urani. Kujiondoa kwa upande mmoja Marekani katika mapatano hayo si tu kwamba hakujaleta mapatano mazuri zaidi, bali pia kumeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa nyuklia wa Iran ikilinganishwa na kipindi cha JCPOA.
Hiki ndicho kitendawili ambacho wakosoaji wa siasa za Trump wanakizungumzia leo. Rais ambaye aliahidi kuwasilisha "mpango bora" sasa anajaribu kujadili makubaliano ambayo kwa njia nyingi yanafanana na kile alichokiita "mpango mbaya zaidi katika historia."
Muhimu zaidi kuliko suala la nyuklia ni matukio ambayo yametokea katika uwanja wa jiopolitiki wa eneo. Vita vya karibuni vimethibisha kuwa Iran bado ina zana nyingi za kutoa mashinikizo dhidi ya Marekani na washirika wake katika eneo. Mfano mzuri zaidi ni Lango-Bahari la Hormuz; njia ambayo bado inachukuliwa kuwa mojawapo ya mishipa na njia-panda muhimu zaidi ya upitishaji nishati duniani.
Ingawa katika miaka ya nyuma, wachambuzi wengi wa nchi za Magharibi walizungumza kuhusu kupungua kwa umuhimu wa kimkakati wa Hormuz, lakini mgogoro wa hivi karibuni umeonyesha kwa mara nyingine tena kwamba usalama wa nishati duniani bado unafungamana na matukio ya eneo hili.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, Iran imeweza kuonyesha mojawapo ya silaha zake bora zaidi bila kuhitajia silaha za nyuklia. Ongezeko la gharama za bima za meli, wasiwasi kuhusu soko la nishati duniani, kupanda kwa bei ya mafuta na gesi pamoja na wasiwasi wa watumiaji biadhaa katika uchumi wa nchi za Magharibi, yote yamethibitisha kuwa kukosekana utulivu katika Ghuba ya Uajemi kunaweza kuwa na taathira kubwa kimataifa. Katika hali hiyo, utawala wa Trump umelazimika kutafuta ufumbuzi wa kufunguliwa kikamilifu njia za kuhamisha nishati na kutuliza masoko ya dunia badala ya kujishughulisha na suala la nyuklia. Hii ndiyo nukta ambayo The Guardian inaiona kuwa ishara ya kushindwa kwa mkakati wa awali wa Washington, kwa sababu mara hii imehamisha uzingatiaji wake kutoka suala kuu la "kuibana Iran" hadi "kudhibiti matokeo ya vita na Iran".
Wakati huo huo migawanyiko ya kisiasa katika kambi ya Magharibi nayo imedhihirika wazi zaidi. Msimamo wa karibuni wa Uhispania ni mfano wazi wa katika uwanja huu. Serikali ya Waziri Mkuu Pedro Sánchez sio tu imekataa kutekeleza siasa za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran, bali pia imetangaza hadharani kuwa vita hivyo ni haramu na vinafanyika kinyume na sheria za kimataifa. Jose Manuel Albarez, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania pia ametangaza kupitia taarifa nadra kwamba Madrid imechagua kati ya "utawala wa sheria" na "sheria ya msitu" na kwamba haiko tayari kushiriki katika hatua zinazoongeza vurugu na mivutano katika Lango Bahari la Hormuz.
Umuhimu wa misimamo hii sio kupinga vita fulani tu. Kinachojitokeza kutokana na tofauti hizi ni ishara ya kudhoofika taratibu mshikamano wa Magharibi kuhusu namna ya kukabiliana na migogoro ya kimataifa. Uzoefu wa Iraq, Afghanistan, Libya na sasa Iran umezifanya serikali nyingi za Ulaya kuwa na mtazamo mbaya kuhusu chokochoko za kijeshi za Marekani. Kwa mtazamo wa nchi hizi, gharama za kisiasa, kiuchumi na kiusalama za vita mara nyingi zimekuwa kubwa zaidi kuliko mafanikio yanayodaiwa.
Hatimaye, matokeo muhimu zaidi ya mgogoro wa hivi karibuni ni kwamba kwa mara nyingine mapungufu ya nguvu za kijeshi katika utatuzi wa masuala tata ya kisiasa yamedhihirika wazi machoni pa waliwemgu, ambapo hata serikali kubwa zaidi ya kijeshi duniani imeshindwa kufikia malengo yake ya kisiasa kupitia mashambulizi ya mabomu na mashinikizo ya kijeshi. Uzoefu wa vita vya hivi sasa umeonyesha kuwa katika nchi za Asia Magharibi, kama ilivyo migogoro mingine mingi ya kimataifa, utatuzi wa kudumu wa migogoro hautimii kupitia vita, bali kupitia njia ya mazungumzo na kukubali ukweli uliopo. Leo, kuliko wakati mwingine wowote, Washington imefikia ukweli kwamba hakuna mbadala wa diplomasia katika kutatua mzozo wake na Iran. Kwa kuzingatia hilo, hata wakosoaji wa Trump nchini Marekani wanasisitiza kuwa rais huyo anayejiita “mfalme na fundi wa kufanya miamala” hatimaye amelazimika kurejea kwenye meza ile ile ya mazungumzo aliyowahi kuiacha; Lakini wakati huu kwa gharama kubwa zaidi kwa Marekani, washirika wake na uchumi wa dunia.