Matembezi ya kilomita 10 katika Siku Kuu ya Ghadir jijini Tehran
-
Matembezi ya Ghadir jijini Tehran
Leo joto kali la mwezi Juni katika barabara za Tehran halikuweza kupunguza hamasa na shauku ya wananchi waliojitokeza kushiriki katika “Ugeni wa Ghadir wa Kilomita 10”.
Tangu saa tisa alasiri njia ya matembezi hayo ilijaa familia zilizoshikana mikono, zikiambatana na watoto wao pamoja na wazee, wakihudhuria sherehe hii kubwa ya Siku Kuu ya Ghadir.
Matembezi yam waka huu yameanzia Medani ya Imam Hussein (AS) hadi Medani ya Azadi, na katika urefu wa kilomita kumi za njia hiyo, zimeandaliwa programu mbalimbali na zenye kuvutia kwa ajili ya wapenzi wa Imam Ali (AS).
Kwa mujibu wa ripoti ya IRNA, miongoni mwa umati walionekana watoto ambao wakati mwingine walichoshwa na joto la hewa. Wazazi wao waliwaburudisha kwa kuwanyunyizia maji baridi nyusoni ili waweze kuendelea na matembezi ya kilomita 10 pamoja na familia zao.
Mmoja wa akina mama aliyeshiriki, aliyekuja pamoja na watoto wake wadogo na wazazi wake wazee, alisema: “Tumetembea katika njia hii kwa mapenzi ya Imam Ali (AS), kwa heshima ya mashahidi na kwa ajili ya nchi yetu. Joto ni kali, lakini mapenzi ya Amir al‑Mu’minin (AS) hurahisisha ugumu wa safari.”
Katika njia hiyo ya kilomita 10 kulikuwa na mahema ya huduma (maukibu) ambapo washiriki wa siku kuu hii ya Ghadir walipata maji baridi, sharubati na vipande vya tikiti maji. Kila baada ya hatua chache, makundi ya wahudumu wa kujitolea, wakiwa na nyuso zenye bashasha, walijitahidi kupunguza uchovu wa washiriki. Wengine walikaribisha kwa vikombe vya maji, wengine walitoa bendera kama zawadi, na wengine walitoa huduma za kitamaduni na kijamii kwa wananchi.
Watoto pia walikuwa na nafasi yao maalumu katika sherehe hiyo. Vibanda vya uchoraji, michezo mbalimbali na bustani za michezo vimeleta nyakati za furaha kwao, huku sauti za vicheko na msisimko wao zikisikika katika baadhi ya maeneo ya njia.
Katika kona moja ya njia, mtu mmoja alikuwa akipiga rangi viatu vya washiriki kama ishara ya heshima na mapenzi kwa wageni wa Ghadir. Si mbali na hapo, wahudumu wengine walikuwa wakigawa bendera miongoni mwa wananchi. Kila mmoja alijitahidi, kwa kadiri ya uwezo wake, kuchangia kufanikisha sherehe hii kubwa na yenye baraka.
Sherehe ya Ugeni wa Ghadir wa Kilomita 10 mwaka huu, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, imekuwa taswira ya mshikamano wa kijamii, furaha ya pamoja na ushiriki mkubwa wa familia. Uwepo huu umeonyesha kuwa joto la hewa, hata liwe kali kiasi gani, haliwezi kupunguza ari ya watu waliokusanyika kwa mapenzi ya Ghadir.
Ikumbukwe kuwa siku kama hii miaka 1437 iliyopita, Mtume Muhammad (SAW), akiwa njiani kurejea Madina kutoka katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Talib (AS) kuwa kiongozi wa Waislamu baada yake.
Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu (SAW) ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum, katika makutano ya njia kati ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume (SAW) alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu, kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Talib na kusema: “Kila ambaye mimi ni kiongozi wake, basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende anayempenda na amfanyie uadui anayemfanyia uadui.” Siku hii huadhimishwa na idadi kubwa ya Waislamu kama Siku Kuu ya Ghadir.