Iran yazindua kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya saratani Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138846-iran_yazindua_kituo_kikubwa_zaidi_cha_matibabu_ya_saratani_asia_magharibi
Iran imezindua kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya saratani katika eneo la Asia Magharibi, ambacho kinachukua nafasi ya kituo cha zamani, kwa hospitali mpya yenye ghorofa 18, vitanda zaidi ya 610 na teknolojia ya kisasa ya matibabu.
(last modified 2026-06-03T04:10:30+00:00 )
Jun 03, 2026 04:09 UTC
  • Jengo jipya la Taasisi ya Saratani ya Iran
    Jengo jipya la Taasisi ya Saratani ya Iran

Iran imezindua kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya saratani katika eneo la Asia Magharibi, ambacho kinachukua nafasi ya kituo cha zamani, kwa hospitali mpya yenye ghorofa 18, vitanda zaidi ya 610 na teknolojia ya kisasa ya matibabu.

Jengo jipya la Taasisi ya Saratani ya Iran (Iran Cancer Institute) lilizinduliwa jana Jumanne katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Afya Mohammadreza Zafarghandi.

Kituo hicho, kinachotumika kama kitovu cha kisayansi cha nchi kwa ajili ya kuzuia, kutambua na matibabu ya aina zote za saratani, kimejengwa katika eneo la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 60,000 katika ghorofa 18.

Kituo hicho kinajumuisha idara 37 maalumu, vifaa 11 vya upigaji picha na tiba ya mionzi, na vitanda 96 vya tibakemikali (chemotherapy.)

Waziri wa Afya na Elimu ya Tiba wa Iran, Mohammad Reza Zafarghandi, amesema wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Hospitali ya Taifa ya Taasisi ya Saratani kwamba ufunguzi wa kituo hiki ni mojawapo ya hatua muhimu zaidi katika sekta ya afya ya nchi katika miaka ya hivi karibuni na kusisitiza kwamba uzinduzi wa kituo hicho katika hali ngumu ya nchi unatuma ujumbe wazi wa mwendelezo wa utoaji huduma za afya na azma ya kitaifa ya kuendeleza miundombinu ya matibabu.

Zafarghandi ameongeza kuwa: "Jambo muhimu ni kwamba mradi huu unaanzishwa katikati ya vita, na suala hili lina ujumbe wa wazi; jamii ya afya ya Iran inasimama upande wa watu."

Waziri wa Afya wa Iran ameendelea kusema: "Hivi majuzi, katika mkutano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva, nilisisitiza kwamba jamii ya afya ya Iran haijaacha kuwahudumia watu katika hali ngumu zaidi, na tunashuhudia roho hiyo hiyo leo."

Mkurugenzi wa Hospitali ya Imam Khomeini Complex, Abdolrahman Rostamian pia amesema katika sherehe ya uzinduzi wa kituo hicho kwamba hospitali mpya, yenye zaidi ya vitanda 610 vya kulazwa wagonjwa, vyumba 19 vya upasuaji, na vifaa na teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu, vitakuwa na nafasi muhimu katika kutoa huduma maalumu na za kitaalamu zaidi za saratani.

Kwa upande wake, Sayyid Reza Raeeskarami, Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran, pia amesema kwamba wakati wa kutayarishwa na kukamilisha jengo hilo, vita viwili vilianzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Raeeskarami ameelezea zaidi kwamba hospitali hiyo itatibu aina zote za saratani kwa watoto na watu wazima.

Amethibitisha kwamba wataalamu bora na wenye uzoefu zaidi watakuwepo katika kituo hicho.