Ayatullah Khatami: Trump ana jeni ya kusema uongo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138678-ayatullah_khatami_trump_ana_jeni_ya_kusema_uongo
Imamu wa Swala ya Idul Adh'ha iliyofanyika mapema leo mjini Tehran amesema: "Maadui wanatamani taifa la Iran lichoke, lakini kwa neema ya Mungu, wataingia kaburi na matarajio hayo."
(last modified 2026-05-27T15:19:14+00:00 )
May 27, 2026 15:17 UTC
  • Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami
    Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami

Imamu wa Swala ya Idul Adh'ha iliyofanyika mapema leo mjini Tehran amesema: "Maadui wanatamani taifa la Iran lichoke, lakini kwa neema ya Mungu, wataingia kaburi na matarajio hayo."

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema katika hotuba za Swala ya Eid al-Adh'ha iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran kwamba mfano dhahiri wa uchamungu katika zama za sasa ni muqawama na kusimama kidete katika njia ya kupigania ukweli na haki, na kuongeza kuwa: "Kile ambacho watu wa Iran wamefanya katika usiku wa 87 zilizopita na wataendelea kufanya hadi ushindi wa mwisho utakapopatikana, ni mfano dhahiri wa uchamungu."

Ayatullah Khatami amesema: "Maadui wanatamani kuona watu wa Iran wakichoka, lakini kwa neema ya Mwenyezi Mungu, watapeleka matarajio hayo makaburini mwao; taifa hili litauchosha uchovu, lakini kamwe halitachoka wala kulegalega."

Imamu wa Swala ya ya Idul Adh'ha ameendelea kwa kunukuu Hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W.) ambaye amesema, "Anayekubali kudhalilishwa si miongoni mwetu," na akaelezea kuwa: Kukubali kudhalilishwa si tu kwamba ni jambo lisilopendeza, bali pia ni uovu wa kimaadili. Maadui zetu, hasa wakazi wa 'jumba jeusi', ambalo linaitwa kwa makosa "Ikulu Nyeupe," (White House) wanatamani kona taifa la Iran likidhalilika; lakini wataingia kaburini na ndoto yao hiyo."

Ameitaja Marekani kama muongo asiye na kifani katika historia na kusema: Adui lazima aseme ukweli walau mara moja ili ulimwengu uweze kuona kama anajua njia na desturi za kusema ukweli au la; Jeni ya Trump ni jeni la kusema uongo, ambayo mara zote inakuja na udanganyifu na uongo katika mazungumzo; adui hataki mazungumzo, bali kujisalimisha taifa la Iran; hata hivyo ukweli ni kama alivyosema Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake kwa Mahujaji: "Taifa la Iran limemfanya adui ashindwe kulipigisha magoti."

Ayatullah Khatami amesema: Jambo lingine ambalo halipaswi kupuuzwa ni simulizi ya msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza "Global Sumud Flotilla", ambao umekusanya watu kutoka kote dunia kuwasaidia binadamu wanaokandamizwa huko Gaza.

Hatibu wa Swala ya Idi ya Tehran amesema: "Tukio hili limeonyesha mambo mawili. Picha ya kwanza ni kubakia hai dhamiri ya ubinadamu. Walianzisha msafara huo licha ya kujua kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel utawatendea uhalifu, na hili ni jambo lenye thamani. Kuwaunga mkono watu wanaokandamizwa ni thamani, kwa watu wa dini na imani zote."

Sayyid Khatami amesema:"Picha ya pili ni ile inayodhihirisha tena kiwango cha juu cha uovu, uhalifu na ukatili wa utawala haramu wa Israel. Kiwango hiki cha uovu kimenakshiwa kwenye paji la uso la Wazayuni na Trump mhalifu anayemuunga mkono mhalifu huyo muuaji wa watoto."