Nov 06, 2022 10:04 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (7)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya saba ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu.

Leo tutaangalia ni namna gani mafundisho ya Akhlaqi za Kiislamu kwa upande mmoja yanavyokabiliana kimtazamo na baadhi ya imani za dini zenye mielekeo ya kuabudu na kukumbatia dunia; na kwa upande mwingine yanavyopiga vita baadhi ya imani nyingine za dini zinazoitakidi kuwa akhlaqi sahihi ni za watu kujitenga na kuishi maisha ya utawa na kuipa mgongo dunia. 

Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu kusikiliza yale niliyokuandalia katika mafululizo huu.

Bila shaka ungali unakumbuka mpendwa msikilizaji kwamba katika sehemu ya sita ya kipindi hiki tulizungumzia kwa ujumla kuhusu nadharia tatu za kifikra za masuala ya akhlaqi ambazo ni nadharia inayotoa kipaumbele kwa “raha na starehe” kwa kuufanya mhimili mkuu wa kuzingatiwa katika akhlaqi; nadharia inayomzingatia “mtu binafsi” na maslahi yake kama msingi wa kila jambo; na nadharia inayotanguliza mbele maslahi ya “kijamii” ya watu kuliko kitu chochote kingine. Katika kuzitolea ufafanuzi nadharia za vyuo hivyo vya kifikra tukabainisha kwamba kwa vile hakuna hata moja kati ya nadharia hizo tatu za kiakhlaqi inayochunga na kuzingatia msingi wa tauhidi wa kumwamini Mungu Mmoja na Pekee wa haki pamoja na Maádi, yaani imani ya kufufuliwa kwa viumbe, kujaliwa na kuheshimiwa misingi ya kiakhlaqi katika nadharia hizo huwa na udharura na umuhimu ikiwa tu hakutakinzana na kuwa na mgongano na raha na starehe za watu pamoja na manufaa na maslahi ya mtu binafsi na ya kimakundi ya watu katika jamii. Halikadhalika tulieleza kwamba, kwa mujibu wa usuli na misingi ya mitazamo ya nadharia hizo tatu, akhlaqi si jambo la kufungamana nalo kimutlaki, bali linategemea hali na mazingira; na kwa hivyo pale wafuasi wa nadharia hizi wanapofika njiapanda huzitoa kafara na kuzipa mgongo thamani za kiakhlaqi mkabala na maslahi yao ya kimaada. Lakini katika utamaduni uliotukuka wa Kiislamu, wenye malengo aali na wa kumfikisha mja kwenye ukamilifu wa kiutu, kuitambua mtu nafsi yake na kumjua Mola wake, huwa usuli, msingi na mhimili mkuu katika nyuga na nyanja za masuala yote na ndio unaojenga fikra na mitazamo ya kiakhlaqi. Na katika mtazamo huu, matashi, hawaa na matamanio ya nafsi hayapewi nafasi yoyote, wala maslahi haramu ya mtu binafsi na ya kijamii hayapewi kipaumbele chochote. Dira na mwongozo unaofuatwa na mtu aliyeleleka kiakhlaqi katika chuo cha Uislamu na mwenye imani sahihi ya Mwenyezi Mungu, ni ule uliobainishwa katika aya ya 162 ya Suratul-Anám inayomuhutubu Bwana Mtume SAW, ambaye ndiye ruwaza na kigezo kilichokamilika cha kiakhlaqi, ya kwamba: "Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote."

 

Ukiachilia mbali nadharia zilizobuniwa na wanadamu, lakini hata katika matapo ya wafuasi wa baadhi ya dini za mbinguni za tauhidi pia ambazo zimekumbwa na wimbi la upotoshaji na kutiwa mkono mafundisho yao ya asili katika zama mbalimbali za historia, humo pia kuna fikra pogo na potofu, ambazo zinakinzana vikali na mafundisho halisi ya Uislamu. Kwa kutoa mfano tunaweza kuashiria matapo ya dini ya Kiyahudi yenye mielekeo ya kimaada na kukumbatia dunia na yale ya Kinasara au Kikristo yanayokumbatia utawa na kuipa mgongo dunia. Katika muelekeo wa kiakhlaqi, mitazamo yote hiyo miwili haiendani na wala haikubaliani kabisa na misingi na thamani za akhlaqi za Uislamu. Katika aya ya 96 ya Suratul-Baqarah, Quráni tukufu inabainisha na kutoa taswira ya hulka ya kupenda umaada na kukumbatia dunia waliyonayo Mayahudi kwa kusema: “Na hakika utawaona (Mayahudi) ni wenye kuwashinda watu wote kwa pupa ya kuishi, na kuliko washirikina. Kila mmoja wao anatamani lau angeli pewa umri wa miaka elfu."

Ifahamike vyema hapa kwamba, kukemewa katika Uislamu hulka ya kupenda na kuikumbatia dunia na kujilimbikizia mali na utajiri, hakumaanishi kwamba dini hiyo iliyokamilika inapinga watu kujishugulisha na kujiimarisha kiuchumi; hasha wa kalla. Ukweli ni kwamba katika chuo cha fikra cha Uislamu kuna mfumo wa kimantiki wa uchumi uliokamilika katika kuangalia mambo na unaozingatia uhalisia wake. Mfumo wa kiuchumi ambao, lau kama utafuatwa na kutekelezwa kwa usahihi wake, unaweza katika zama zetu hizi, kuanzisha na kujenga muundo mpya katika nyuga mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya jamii ya walimwengu. Huo ni uchumi safi na salama, uliotakasika na ulaji riba, ulaji hongo na rushwa, kujilimbikizia wachache mali na utajiri, uchumaji mali wa dhulma na haramu, unyonyaji, kuwahilikisha watu kwa njaa na ufukara pamoja na kupoka na kupora utajiri na maliasili za mataifa mengine, ambazo zote hizi ni sifa hasi maalumu zinazoshuhudiwa katika baadhi ya vyuo vya kifikra vya kimaada vilivyoko katika dunia ya zama zetu hizi.

 

Mkabala wa mapote ya kinadharia yenye muelekeo wa kimaada na kujilimbikizia mali na utajiri tu, limejitokeza pia tapo katika wafuasi wa dini aliyokuja nayo Nabii Isa Masih (as) ambalo limejichagulia na kukhitari kufuata njia ya maisha ya utawa, kuishi maisha ya kujitenga na kuipa mgongo dunia. Na katika kufanya hivyo wafuasi wa tapo hili, wamejikhini na kuyapa kisogo mahitaji yao yote ya kimaumbile ikiwemo kujizuilia hata kufunga ndoa na kuanzisha familia, ambalo ni jambo la dharura kidini na kiakili; na badala yake kuamua kujitenga kwa kwenda kupiga kambi kwenye mahekalu na kuachana na shughuli zote za masuala ya kijamii. Lakini kwa vile uono na mtazamo huu unakhalifu fitra na maumbile aliyojaaliwa mwanadamu na Mola wake, matokeo yake ni kwamba wanaofanya hivyo wameshindwa kulifikia hata lengo la asili pia, ambalo ni kumcha Mwenyezi Mungu, kutokuwa na raghba ya kupenda dunia na kufikiria kupata radhi za Mola. Na matokeo yake huishia kunasa kwenye kinamasi cha upotofu na ufisadi wa mambo mbalimbali ya kiakhlaqi, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa; jambo linalothibitisha kuwa mwenendo wa kiakhlaqi uliofuatwa na watu wa tapo hilo si sahihi.

Lakini kinyume na mitazamo hiyo miwili ya kufurutu mpaka wa kupaparikia mambo au kujikhini nayo, mtazamo wa kadiri na wastani wa Uislamu umewatandikia wanadamu njia ya kati na kati, ambayo si ya kuifanya dunia na vivutio vyake ndio lengo la maisha ya mwanadamu; na si kuamua kujikhini na kujinyima raha zote za kimsingi na kimantiki zilizowekwa kwa ajili ya kiumbe huyo, na matokeo yake yakawa ni kutumbukia kwenye upotofu; mfano hai ukiwa ni visa na mikasa mbalimbali ya kashfa za kingono zinazofichuliwa kila uchao, zikiwahusisha wachungaji, watawa na viongozi wa kanisa katika pembe mbalimbali za dunia. Lakini kinyume na mitazamo hiyo, chuo cha akhlaqi cha Uislamu kinafuata njia ya kadiri na wastani katika mambo yote. Hakighafiliki na suala la msingi la kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kujipinda kutafuta masurufu kwa ajili ya ulimwengu wa milele anaoelekea mwanadamu, na wakati huohuo unashajiisha kufaidika inavyostahiki na neema za Mwenyezi Mungu za hapa duniani, ili kuonyesha kwamba ukamilifu wa mwanadamu unapatikana kwa kuwepo mizani ya mlingano kati ya dunia na akhera.

 

Mpendwa msikilizaji sehemu ya saba ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya nane ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/