Akhlaqi Katika Uislamu (9)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya tisa ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa, katika kipindi kilichopita tulizungumzia na kuchambua sifa tatu kuu za akhlaqi za Kiislamu, ambazo ni: kuwepo ustawi wenye mlingano na wa pande zote wa thamani zilizotukuka za kiakhlaqi; kumlea na kumjenga mtu kwa sifa kamilifu na za pande kadhaa za kiakhlaqi na hatimaye kumfanya afikie daraja na upeo wa juu kabisa wa thamani za kiakhlaqi.
Hakuna shaka sifa hizi tulizozitaja zinapatikana kwenye chuo cha fikra za kiakhlaqi cha Uislamu; na hakuna chuo kingine chochote kile cha fikra kilichoweza kukusanya sifa hizi kwa ukamilifu wake. Na kama tutaongezea juu ya sifa hizi kufanya mambo kwa nia ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na tukatambua kuwa thamani za kiakhlaqi hupata chimbuko na asili zinapokuwa na mfungamano na Mola Mwenyezi, hapo tena haibakii shaka yoyote kuwa chuo cha fikra cha akhlaqi cha Uislamu ndicho chuo cha akhlaqi cha asili zaidi na kilichokamilika zaidi, kwa sababu mambo yote ayafanyayo mtu huwa hayatokani na sababu za binafsi, utaifa, rangi na asili yake, eneo la kijiografia analoishi wala ria, kujionesha na kutaka kuwaghilibu au kuwadanganya watu.
Maudhui nyingine muhimu ambayo huwa haizingatiwi ipasavyo katika kutathmini na kuzungumzia vyuo vya fikra vya kiakhlaqi ni kwamba, kuwepo hali na mazingira mwafaka na yanayostahiki ni sharti la lazima kwa ajili ya kulea na kujenga thamani za kiakhlaqi katika jamii. Usuli na msingi huu mkuu inapasa upewe uzito mkubwa ili iweze kupatikana tija maridhawa na inayotamaniwa. Kwa kutoa mfano, ikiwa jamii yoyote ile inataka watu wake wapate makuzi mema na safi ya kielimu na kimafunzo, inapasa iandae mazingira na kutimiza masharti yote yanayohitajika ili kuweza kufikia lengo hilo, ikiwemo kuanzisha vituo vya elimu na utafiti, kuandaa walimu na wahadhiri weledi na wajuzi, kuandaa vitabu vya masomo vinavyoendana na maendeleo mapya ya kielimu, kuandaa mazingira mazuri pamoja na kugharimia na kutenga bajeti ya kutosha na inayohitajika ili kuweza kutoa ushindani katika uga wa elimu na kuzitangulia na kuzipiku jamii zingine. Au kama nchi yoyote ile inataka kujitegemea kwa kujitosheleza kwa mazao ya kilimo, inatakiwa iandae mazingira yote yanayohitajika, yakiwemo ya kuwa na ardhi yenye rutuba, zana na pembejeo za kisasa, mifumo bora ya umwagiliaji maji, mbegu na miche mizuri, mafunzo bora kwa wakulima na kuandaa mabwanashamba wajuzi na wataalamu, ili nchi hiyo iweze kujitosheleza kimahitaji kwa wingi na ubora wa mazao na kutohitajia msaada wa maajinabi.
Baada ya utangulizi huu mpendwa msikilizaji, inapasa tuseme kuwa, kukua kwa thamani na heshima tukufu za kiakhlaqi na kiutu katika mfumo wowote ule, huyumkinika na ikawezekana kuwa na matarajio ya kuona tabia, silka, mwenendo na matendo yenye thamani ya kiakhlaqi kwa watu wa mfumo huo wa utawala, pale yanapokuwa yameandaliwa mazingira sahihi na mwafaka ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi, katika pande zote za siri na dhahiri ya mfumo huo. Na ni kwa sababu hiyo, ndio maana katika malengo ya Uislamu wa asili aliokuja nao Bwana Mtume Muhammad SAW ni kuhakikisha kuwa watu wanaoshika hatamu za madaraka katika mfumo wa kisiasa wa Uislamu, wanakuwa ni watu walioleleka na kupambika na sifa tukufu katika kila hali, na wenye imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu, ili wasije wakapotoka kwa kutumbukia kwenye lindi la uchu wa madaraka na kughilibiwa na hawaa na wasiwasi wa shetani. Wasiwe pia watu ambao fikra zao zote zimejikita katika kupora mali za umma na kujilimbikizia utajiri; na kwa ufupi ni kuwa, wawe ni watu ambao madaraka si lengo kwao, bali wayaangalie kama wenzo tu wa kuweza kuutumia katika juhudi za kusimamisha uadilifu na kupambana na ufisadi, ubaguzi na upendeleo.
Hakuna shaka kuwa, tabia na mwenendo wa viongozi vina nafasi na taathira kubwa katika kujenga na kuikuza jamii katika hali ya kujali na kuheshimu thamani za kiakhlaqi au kukanyaga na kwenda kinyume nazo. Na ndio maana imeelezwa katika Hadithi kwamba: " الناسُعلی دین ملوکهم ." , yaani mwenendo na utaratibu wa maisha ya watu katika jamii yoyote ile huathiriwa na hata kufuata kigezo cha mwenendo wa viongozi wao. Ikiwa viongozi watakuwa kioo cha usafi, heshima na maadili mema ya kiakhlaqi, watu wao pia watafuata njia ya kujali na kuchunga thamani za kiakhlaqi; na kinyume chake, kama viongozi na watawala watakuwa dhihirisho la maovu na ufisadi, wananchi wao pia wataondokea hivyo kwa kupitisha maisha yao katika mazingira yaliyo dhidi ya maadili mema ya kiakhlaqi. Athari za mitazamo na mienendo ya viongozi wa kila jamii kwa watu wao ni kubwa kiasi ambacho, imeelezwa katika Hadithi ya kwamba: "watu wanafanana zaidi na viongozi wao katika tabia na mitazamo, kupita hata baba zao."
Jambo jengine muhimu ambalo lina nafasi kuu katika kuandaa mazingira ya kuwa na jamii safi kiakhlaqi ni utamaduni; yaani mjumuiko wa mila, desturi na mtindo wa maisha wa kila mfumo, ambazo ndizo nguzo za kujengea kila jamii na huwa na taathira kwa mielekeo na malengo yote ya mtu binafsi na jamii kwa jumla. Ni kwa kuwa na mtazamo huu, ndipo kujitegemea na kujitawala kiutamaduni kunapokuwa na umuhimu maalumu na wa kipekee; na ni kwa sababu hiyo pia, katika makabiliano baina ya tamaduni, jamii na ustaarabu unaofanikiwa ni ule ulio macho na makini katika kukabiliana na hujuma za kiutamaduni za maajinabi ili kuweza kulinda mipaka yake ya kujitawala na utambulisho wake wa kiutamaduni; na kwa njia hiyo, kuweza kuzuia kwa nguvu na uwezo wake wote ushawishi wa kiutamaduni wa adui. Mfumo wowote ule ambao haushughulishwi na kulinda kujitawala na kujitegemea kwake kiutamaduni huanza kidogo kidogo kupoteza utambulisho wake; janga ambalo leo hii linashuhudiwa kwa uwazi kabisa katika baadhi ya nchi za Ulimwengu wa Mashariki ambazo zina historia na staarabu kongwe na za asili, ambapo kizazi cha vijana wao kimeathiriwa mno na ushawishi wa utamaduni wa Magharibi kufika hadi ya kuufanya utamaduni huo kuwa ndio kigezo na mfano wa kuiga katika mtindo wao wa maisha. Matokeo yake ni vizazi vya jamii hizo kughiriki na kutopea kwenye ufuska na mambo ya anasa na kukikosesha moja kwa moja fursa ya kukijenga katika mazingira ya thamani sahihi za kiutamaduni. Kwa sababu hiyo hakuna shaka yoyote kwamba, ili jamii yoyote ile iweze kukua na kujengeka kwa thamani za kiakhlaqi, ni lazima ijitegemee na kujitawala kiutamaduni.
Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya tisa ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 10 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/