Akhlaqi Katika Uislamu (13)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 13 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia "tabia njema" na nafasi muhimu iliyonayo katika utamaduni wa malezi ya kiakhlaqi na kimwenendo ya Uilsamu. Na kama ujuavyo mpendwa msikilizaji, moja ya madhihirisho makubwa na ya wazi ya tabia na akhlaqi njema ni suala la kusamehe. Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye alikuwa ruwaza njema na kigezo bora na kisicho na mfano cha usamehevu, kwa maadui zake waliomtendea ubaya kwa uelewa na watu wake mwenyewe waliomkosea kwa sababu ya ujinga na kutojua, amesema katika Hadithi kwamba: "Je, nikujulisheni sifa bora za kitabia za duniani na akhera?" Kisha akasema: "Kuunga uhusiano na mtu aliyevunja nawe, kumsamehe na kumsaidia mtu aliyekunyima na kukataa kukupa msaada, na kumsamehe aliyekudhulumu na kukufanyia ubaya (ni katika alama za tabia na akhlaqi njema.)" (Usulul Kafi, Mlango wa Kusamehe).
Katika Hadithi nyingine, Nabii huyo wa rehma anawaelezea wenye kupambika na sifa hizo kuwa ndio watu bora duniani na akhera kutokana na moyo wa usamehevu kutawala tabia na mienendo yao ya kiakhlaqi.
Imam Jaafar Sadiq AS, amezitaja sifa hizo tatu za kiakhlaqi kuwa ndio utukukaji wa kiakhlaqi duniani na akhera.
Viongozi wa kweli wa Uislamu na Maimamu wateule wa dini, daima walikuwa wakijibidiisha kuyafanyia kazi mafundisho ya kitabia ya Uislamu kwa kuyatekeleza na kuyathibitisha kivitendo.
Siku moja, bwana mmoja kutoka mji wa Sham, aliyekuwa ameathiriwa na propaganda chafu na maneno ya sumu yaliyokuwa yakienezwa na Bani Umayya, alifika mjini Madina; na katika pitapita zake alimwona mtu amekaa kitako mahali. Akamuuliza mtu mmoja aliyekuwepo karibu na mahali hapo: "yule nani?" akaambiwa: Ni Hussein Ibn Ali (AS)". Aliposikia vile, yule mtu, ambaye alikuwa na kinyongo na uadui na watu wa kizazi cha Bwana Mtume SAW alimwendea Imam Hussein AS mahali alipokuwa amekaa na kuanza kutoa kila uchafu wa matusi alioweza kuutema kutoka kinywani mwake na kuuelekeza kwa mtukufu huyo. Imam Hussein aliisoma aya ya 199 ya Suratul-A'raaf isemayo: Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na kwa uso wa tabasamu na maneno ya upole, akamuuliza yule bwana: Wewe ni mtu wa Sham? Yule bwana, ambaye hakutarajia kabisa kama Imam Hussein angeamiliana na kulahikiana naye kwa upole na uchangamfu, alijibu, "naam". Imam Hussein, alikuwa akijua vyema kwamba bwana yule alikuwa amechochewa na watawala wa kiimla wa Bani Umayyah waliopanda mbegu ya sumu na uadui akilini mwake ili awe na uadui na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume. Lakini kinyume na alivyotegemea alimwambia: "Wewe ni mgeni katika mji wetu, kwa hivyo kama una shida ya kitu tukusaidie, kama una njaa tukakukirimu nyumbani. Kama una tatizo la nguo tukupatie cha kuvaa; na la kama una shida ya fedha na uko kwenye hali ngumu basi tukupatie." Yule mtu, ambaye hakutegemea katu kama Imam Hussein angeonyesha upole na usamehevu kwa matusi aliyomtolea, alitamka kwa soni na aibu: "Natamani ardhi ingepasuka ikanifukia kuliko ufidhuli huu niliofanya". Kisha akaendelea kunena: "hadi kabla ya leo hakuwepo mtu niliyekuwa nikimchukia zaidi duniani kama wewe na baba yako Ali (AS), lakini kuanzia sasa, hakuna mtu kipenzi zaidi kwangu mimi kuliko wewe na baba yako mtukufu." (Muntahal-Aamal Ukurasa 350)
Kusamehe mpendwa msikilizaji kumefananishwa na alkemia inayobadilisha shaba kuwa dhahabu. Qur'ani tukufu inabainisha taswira ya hali hiyo katika aya ya 34 ya Suratu Fussilat inaposema: "Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu".
Katika mazingira ya kawaida, yaani wakati mtu anapokuwa hana nguvu na mamlaka, haiwi tabu sana kwake kusamehe makosa na mabaya anayofanyiwa na wenzake; na si ajabu akaona ni kitu rahisi kwake kufumbia macho makosa na mabaya hayo. Lakini wakati mtu anapokuwa na uwezo na mamlaka, na likawa jambo linalowezekana kwa yeye kulipiza kisasi kwa nama yoyote atakayo; na katika mazingira hayo akawa tayari kuvumilia na kusamehe ubaya anaofanyiwa, usamehevu wa aina hiyo huwa ni wa kiungwana na unastahili sifa na pongezi. Imam Hussein Ibn Ali (AS), ambaye ni Imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia analizungumzia hilo kwa kusema: "Mtu aliye msamehevu zaidi ni yule anayewasamehe watu (makosa na mabaya yao) wakati ana nguvu na uwezo." (Mizanul-Hikmah, Mlango wa Kusamehe, 4335).
Moja ya mifano mikubwa zaidi, uliong'ara zaidi, usiosahaulika na utakaobakia milele katika historia kuhusiana na kusamehe na usamehevu, ni agizo la Bwana Mtume Muhammad SAW la utoaji msamaha kwa wote, wakati ulipokombolewa mji mtukufu wa Makka. Ni pale mtukufu na Mtume huyo wa Allah alipoongoza jeshi la watu elfu kumi na kuingia Makka, akiwa kwenye kilele cha nguvu na mamlaka. Katika lahadha na muda huo, pale maashrafu na vinara wa Makureishi, hususan Abu Sufyan, ambaye hakuwa amesita kufanya kila njama na hakuacha kuchukua kila hatua aliyoweza ili kuuangamiza Uislamu na kumshinda Bwana Mtume SAW na masahaba zake, aliposikia kwamba Bwana Mtume na jeshi lake wanaingia Makka kwa nguvu na uwezo kamili, alitetemeka kwa hofu na kudhani kwamba, kama yafanyavyo majeshi mengi ya watekao na kukomboa miji, Bwana Mtume SAW, naye pia atatoa amri ya wao wote kuuliwa; na hasa alipomsikia mbeba bendera ya jeshi la Uislamu Saad Ibn Ubadah akipaza sauti na kutoa kaulimbiu ya "leo ni siku ya kulipiza kisasi". Ilikuwa wakati huo na katika anga hiyo iliyogubikwa na wingu la woga na hofu iliyokuwa imejaa ndani ya nyoyo za washirikina wa Makka, ghafla Bwana Mtume Muhammad SAW akamwamuru Ali (AS) ashike na kuinua juu bendera ya ushindi ya jeshi la Uislamu na kutangaza kaulimbiu ya "leo ni siku ya msamaha na urehemevu". Na kwa hatua hiyo, mji wa Makka, ambao kabla yake ulikuwa kitovu cha ukafiri, shirki, kuabudu masanamu na kambi kuu ya maadui wakubwa walioukamia kuuangamiza Uislamu na Waislamu, ukakombolewa bila kumwagwa damu. Na mvuto wa msamaha huo wa Kiislamu ulipenya na kuziathiri mno nyoyo, kiasi cha kuwafanya watu wasilimu makundi kwa makundi; na mbiu isiyo na kifani ya ushindi huo ikasikika na kuenea katika kila pembe ya Bara Arabu na ulimwengu wote wa zama hizo na kubakisha kumbukumbu yake kwenye kurasa za historia ya Uislamu.
Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 13 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 14 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/