Akhlaqi Katika Uislamu (15)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 15 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu, ambayo kwa leo yatahusu sifa ya uaminifu na kutunza amana na jinsi ilivyotiliwa mkazo katika dini tukufu ya Uislamu.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia thamani na hadhi maalumu ya sifa ya ukweli na kusema kweli katika utamaduni wa Kiislamu. Lakini tujue pia kwamba, sambamba na ukweli katika maneno na matendo, kuna dhihirisho jengine miongoni mwa thamani za kiakhlaqi, ambalo ni "kutunza amana", sifa ambayo imepewa uzito na umuhimu mkubwa katika mafundisho ya dini. Inatosha kuelewa umuhimu wa suala hii la msingi kwa kuirejea kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sehemu ya mwanzo ya aya ya 58 ya Suratun-Nisaa aliposema: "Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe."
Kwa kuzingatia kwamba katika aya hiyo neno "amana" limetumika kiujumla bila kufungamanishwa na kitu maalumu, maulamaa na wafasiri wa Qur'ani wametoa rai tofauti kuizungumzia maana ya amana na wakasema, madhumuni yaliyokusudiwa kuhusu amana yanaweza yakawa ni siri za mambo, kitu kama fedha na au hata wadhifa wa kidini, kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi na kijeshi; kwa maana kwamba, kama mtu havimlaiki na hana ustahiki navyo, basi anatakiwa bila kufanya ajizi avikabidhi kwa wanaostahiki kushika vyeo na nyadhifa hizo; na asipofanya hivyo, si tu atakuwa hajachunga msingi wa kutunza amana, lakini atakuwa ameisaliti pia jamii yake.
Moja ya sifa maalumu walizokuwa nazo Mitume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kusifika kwa "uaminifu" kwa watu wa zama zao; na kwa sababu hiyo wakawa wanaaminika mno kwa watu wao. Katika zama za ujahilia katika ardhi ya Bara Arabu, ambayo ndani yake haikuwepo athari na alama yoyote ya thamani za kiakhlaqi na kiutu, hata kabla Nabii Muhammad SAW hajabaathiwa na kupewa Utume, alijulikana na watu wa huko kama Muhammad al-Amin, kutokana na alivyotajika kwa sifa njema ya uaminifu.
Imam Jaafar Sadiq AS, ambaye alilelewa na kukulia katika chuo cha malezi ya Utume anaizungumzia falsafa ya kutumwa Mitume kwa kusema: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mwenye Izza na Aliyetukuka hakumtuma kuwa Nabii Mtume yeyote isipokuwa (Mtume huyo) alipambika kwa sifa mbili tukufu za ukweli na uaminifu." (Usulul-Kafi).
Lakini mbali na Mitume, watu waumini pia, ambao wana imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake itokanayo na uelewa, wanatakiwa waifanye sira na mwenendo wa Manabii hao kuwa ruwaza na mfano wao wa kuiga; na kama walivyokuwa wao, wajipambe kwa sifa ya kiakhlaqi ya uaminifu na kuchunga amana. Katika aya za mwanzo za Suratul-Muuminun, Qur'ani tukufu inataja sifa za kiibada, kiakhlaqi, kijamii na za usafi wa kimaadili za waumini, ikiwemo aya ya 8 isemayo: Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao. Aidha aya ya 32 ya Suratul-Maarij inasema: Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao.
Kinyume na mtazamo wa watu na vyuo vya kifikra vinavyoichukulia akhlaqi kuwa kitu kinachoendana na hali na mazingira na kwa hivyo wanazitumia thamani za kiakhlaqi kimaslahi tu kwa namna ambayo, pale zinapokidhi maslahi na manufaa yao wanafungamana nazo, na pale wanapoamiliana mathalan na mtu waliye na uadui naye wanazipa kisogo thamani hizo, Uislamu unawataka wafuasi wake wa kweli waheshimu misingi yote ya kiakhlaqi, ukiwemo wa uaminifu na kuchunga amana; na waamiliane na marafiki na maadui zao kiusawa, pasi na kuwatafautisha kwa namna yoyote ile.
Katika kulizungumzia suala hilo, Imam Jaafar Sadiq AS anasema: "Mcheni Mwenyezi Mungu na irejesheni amana kwa mtu aliyekuaminini; (kisha mtukufu huyo akaongezea kusema) laiti kama muuaji wa Amirul Muuminin Ali AS atanipa amana yake, basi nitamrejeshea. (Amali-Saduq 4/204)
Katika Hadithi nyingine mtukufu huyo amesema: "Irejesheni amana kwa mwenyewe, hata kama atakuwa muuaji wa Hussein Ibn Ali (AS). (Marejeo hayo hayo).
Inasikitisha mpendwa msikilizaji kuona kwamba, kinyume na mafunzo haya ya kiakhlaqi, baadhi ya watu wanafiki wanaojali maslahi yao tu, ambao hujionyesha kuwa ni waumini ili kuwahadaa watu, wanakhitari kufuata njia ya usaliti na uhaini kwa kutochunga mipaka yoyote na kuamua kukanyaga na kukiuka usuli na misingi yote ya kiitikadi na thamani za kiakhlaqi. Katika aya ya 27 ya Suratul-Anfal, Qur'ani tukufu inazungumzia sifa hiyo mbaya ya watu hao kwa kusema: "Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua."
Kutokana na ujumbe tunaopewa na aya hii ya Qur'ani, inatupasa tuwe macho na makini na kuchukua hadhari kubwa tusije tukahadaiwa na wanafiki na kunasa kwenye mtego wa tabia na mienendo yao ya udanganyifu.
Imam Jaafar Sadiq AS ametupa mwongozo wadhiha na wenye kuweka wazi kila kitu kuhusiana na suala hilo aliposema: "Msihadaiwe na Funga na Sala (za baadhi ya watu), kwani si hasha mtu akawa amezizowea hawezi kuziacha; (kwa hivyo mkitaka kuwapima) watazameni katika ukweli na uaminifu wao wa kuchunga amana." (Usulul-Kafi).
Kwa maelezo haya, tunatakiwa tuachane na mtazamo wa kijuujuu tu katika kuwatambua watu; na badala yake tuuchunguze kwa makini muamala, hasa wa watu wanaojidai kidhahiri kuwa waumini na wenye kushikamana na thamani za kidini na kiakhlaqi, ilhali hawana lengo jengine isipokuwa kuwafanyia wenzao uhaini na usaliti.
Katika aya zake nyingi, Qur'ani tukufu imeweka wazi sura halisi na hatari ya wanafiki, ikiwemo aya ya nane na ya tisa ya Suratul-Baqarah zisemazo: "Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini. Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.
Kwa kutumia ilhamu ya maneno ya wahyi, Bwana Mtume SAW alizikataa imani za wanafiki waliodai kiuongo kuwa wameamini aliposema: "Mtu asiye na moyo wa uaminifu wa kuchunga amana, hana imani (ya dini). (Biharul-Anwar 72/198)
Na katika Hadithi nyingine inayolizungumzia suala hilo kwa uzito mkubwa zaidi, mtukufu huyo amesema: "Mtu ambaye kwa mtazamo wake, kutunza amana ni kitu kidogo na kisicho na thamani, si katika sisi (yaani hana hata harufu ya Uislamu) (Biharul-Anwar 75/172).
Katika kuhitimisha mazungumzo yetu inapasa tuseme kuwa, Waislamu wa kweli huwa wamepambika na sifa mbili kuu za kuwa wakweli na waaminifu katika amana; na sifa mbili hizi muhimu zinawapambanua na kuwatafautisha wao na wale wanaotekeleza amali za ibada na imani za kidini kwa sura ya kujionyesha tu. Na kwa maelezo hayo, niseme pia mpendwa msikilizaji kwamba, sehemu ya 15 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 16 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/