Akhlaqi Katika Uislamu (19)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 19 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu ambapo maudhui yetu ya leo ni nafasi ya suluhu, upatanishaji na maridhiano katika Uislamu.
Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia umoja, mshikamano, ushirikiano na kuwa kitu kimoja umma wa Kiislamu; usuli na msingi muhimu ambao unaudhaminia Ulimwengu wa Kiislamu nguvu, uwezo, izza na ushindi; na pia una mchango mkuu na nafasi ya msingi katika kuimarisha uhusiano baina ya Waislamu. Kama nilivyotangulia kueleza, kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, katika mfululizo huu wa 19 tumekusudia kuzungumzia "suluhu" likiwa ni moja ya mahitaji makuu na ya msingi ya mwanadamu, hususan katika zama zetu hizi. Suluhu, ni kwa maana ya maridhiano, mapatano na kuishi kwa amani na masikilizano, jambo ambalo linakubaliwa na kila dini na kila njia ya itikadi na fikra. Hisia za kupenda suluhu, kama ulivyo umoja na kuwa kitu kimoja, imo kwenye fitra na maumbile ya mwanadamu; na hakuna shaka, moja ya matunda ya umoja na kuwa kitu kimoja ni kupatikana suluhu na utulivu katika jamii ya wanadamu. Katika utamaduni wa Uislamu sahihi na wa asili pia, ambao unatilia mkazo umuhimu wa kuishi kwa amani na masikilizano, suluhu imepewa hadhi na nafasi maalumu. Lakini ni wazi kwamba, sharti la kufanya suluhu, na kama lilivyo suala la umoja, ni kuwapo masuala ya pamoja ya kiitikadi, kifikra na kimatendo yanayowaunganisha watu. Na ni kwa sababu hiyo, ndio maana kundi la mwanzo ambalo Qur'ani imelizungumzia kuhusu suluhu na maridhiano ni la watu wenye sifa ya "uumini", kama inavyoeleza aya ya 10 ya Suratul-Hujurat ya kwamba: "Hakika Waumini ni ndugu, basi (zitokeapo tofauti) patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe."
Kwa hivyo, sharti la kuleta suluhu ni watu kuwa na usuli na misingi ya pamoja ya kiitikadi; na inapokuwa hivyo, watakuwa na mfungamano wa masikilizano, kama walivyo ndugu walio na uhusiano wa upendo mkubwa na wa karibu zaidi baina yao.
Lakini ikiwa kwa sababu yoyote ile zitazuka suutafahamu na tofauti baina yao, ili kutatua hitilafu na tofauti hizo, hakuna haja yoyote ya kuruhusu uingiliaji wa maajinabi wasio Waislamu; na haitakiwi kuwaruhusu wao, ambao hawana misingi yoyote ya pamoja ya kiitikadi na Waislamu, kuingilia suala hilo; bali Waislamu, wabebe wenyewe jukumu la kuratibu na kupanga namna ya kutatua tatizo lililojitokeza na kuzihitimisha kwa nia njema na kwa moyo safi tofauti hizo zilizozuka baina yao.
Jambo jengine ambalo linaweza kutoa mchango athirifu katika kutatua tofauti na kuleta suluhu na mapatano ni kwamba, utatuaji wa tofauti ufanyike kwa kuzingatia taqwa na uchaMungu; kwa maana kwamba, usifanyike upendeleo wa aina yoyote; na wale wanaosimamia suluhu hiyo wasisukumwe na matashi na malengo ya kimapote, kikabila, kitaifa, kimbari, kijiografia na kisiasa; bali wapiganie kuleta suluhu na mapatano kwa nia na lengo moja tu, ambalo ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuzimaliza tofauti zilizojitokeza baina ya ndugu zao Waislamu. Endapo watafanya hivyo, suluhu watakayoleta itakuwa ya haki na uadilifu; suluhu ambayo itakuwa imechunga na kuheshimu haki za pande mbili bila kuchanganya ndani yake utashi wowote ule wa kisiasa.
Kwa hivyo kuwa na masuala ya pamoja ya kiitikadi na kuchunga taqwa katika kuleta suluhu, na kuiunganisha na nguzo ya haki na uadilifu, ni miongoni mwa misingi mikuu ya kujengea suluhu na kuleta amani na masikilizano. Pamoja na hayo, maelezo haya hayamaanishi kwamba Uislamu unaweka mpaka wa mduara wa suluhu, yaani kwa Waislamu pekee; isipokuwa katika hatua ya mwanzo, kipaumbele ni kwa jamii ya umoja, iliyoungana na ya suluhu na maridhiano, ya Ulimwengu wa Kiislamu; lakini kiujumla Uislamu unataka suluhu na mapatano yawepo dunia nzima baina ya jamii za wanadamu na unaandaa mazingira mwafaka na kwa kupitia awamu na marhala mbalimbali ili kufanikisha lengo na muelekeo huo.
Kuhusiana na nukta hii na kwa kuanzia, Uislamu unawataka wafuasi wa dini za mbinguni za tauhidi wanyoosheane mkono wa umoja kwa amani na masikilizano kwa kushikamana na msingi wa imani yao ya tauhidi inayowakutanisha pamoja.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anamweleza hivi Nabii Muhammad SAW, Mtume wake mteule aliyekuja na ujumbe wa suluhu na urafiki:
"Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu."
Kwa hivyo Uislamu, si tu umejaribu kufungiana ahadi na mkataba na wafuasi na viongozi wa dini nyingine za mbinguni kwa kuzingatia usuli na misingi ya pamoja ya kiitikadi iliyopo kati yao, lakini pia, na kwa sababu ni dini yenye utamaduni wa kupenda amani na kuishi kwa masikilizano na wapinzani bali hata maadui zake, unazungumza nao kwa lugha ya maridhiano na uchukulivu, kwa matumaini kwamba, katika anga na mazingira ya suluhu na mapatano, jamii ya wanadamu wote itaweza kuishi pamoja kwa amani na utulivu bila watu wake kuandamana kwa vitisho vya aina yoyote ile. Na kwa ajili ya kufikia lengo hilo, Mwenyezi Mungu Mola mwenye huruma na urehemevu, anamwamuru Mtume wake, ambaye ni rehma kwa walimwengu wote, afanye yafuatayo katika aya ya 61 ya Suratul-Anfal: "Na wakielekea amani, nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua."
Ilikuwa ni baada ya amri hiyo ya wahyi uliotoka mbinguni, Bwana Mtume SAW alisaini mkataba wa suluhu na washirikina wa Makka. Na katika hatua nyingine isiyo na mfano katika historia, wakati alipoingia Makka kwa ajili ya kuukomboa mji huo, huku akiwa ameandamana na jeshi la wapiganaji elfu kumi na akiwa katika kilele cha nguvu na uwezo, tena pasi na kupigana vita wala kumwaga damu, Nabii huyo wa rehma alitoa amri ya kutangazwa msamaha kwa watu wote.
Msikilizaji mpendwa, kwa maelezo hayo niseme pia kwamba, sehemu ya 19 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 20 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/