Nov 06, 2022 11:47 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (20)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 20 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika sehemu kadhaa zilizopita za kipindi hiki tumezungumzia misingi miwili mikuu ya "Akhlaqi za Kijamii", ambayo ni umoja na suluhu na tukaeleza wazi kwamba, ikiwa jamii itakuwa na umoja na mshikamano, utamaduni wa kupenda suluhu na kuishi kwa maridhiano na masikilizano utastawi na kutawala ndani yake. Msingi mwingine muhimu wa "Akhlaqi za Kijamii", ambao una uhusiano wa karibu mno na umoja na suluhu ni "Uadilifu". Kwa maana kwamba, katika mfumo wowote ule, ambao uadilifu unatawala ndani yake, bila shaka yoyote moyo wa umoja, mshikamano, suluhu na masikilizano utadhihiri ndani ya mfumo huo. Na sababu ni kuwa uadilifu, maana yake ni kila mtu kuwa katika hali anayostahiki hasa kuwa; kwa sababu linapofanyika hilo, hakuwepo na athari yoyote ya upendeleo, ya mtu asiye na sifa kupewa asichostahiki na ya mtu kudhulumiwa kwa kunyimwa anachopasa kuwa nacho. Na katika hali hiyo ndipo yanapoandaliwa mazingira ya kuleta umoja, suluhu na utulivu.

Katika utamaduni wa Kiislamu "uadilifu" umepewa hadhi na umuhimu wa kipekee, kiasi cha kuwa na nafasi kuu na ya msingi katika mfumo wa uumbaji wa ulimwengu na pia wa upangaji sharia za Uislamu. Imam Ali (AS), ambaye ni dhihirisho la utetezi wa uadilifu amesema: "uadilifu ni msingi uliowekwa na kusimamia juu yake ulimwengu wa uumbaji." Kwa hivyo, kama katika ulimwengu wa uumbaji inashuhudiwa nidhamu, uratibu na uwiyano wa kustaajabisha, sababu yake ni kwamba, kila kitu katika mfumo huo kipo mahala pake kinapostahiki na kinafanya kazi kwa kufuata njia mahususi kilichopangiwa na mkondo maalumu kiliowekewa; na huo ndio uadilifu katika mfumo wa uumbaji, ambao unavifanya viumbe vyote katika ulimwengu wa uumbaji viwe katika hali ya kadiri, uwiyano na mlingano. Na moja ya matunda ya mfumo wa ulimwengu kuwa na uwiyano na utangamano ni kuwawezesha wanadamu wote kuishi kwa utulivu katika sayari hii ya dunia. Mwenyezi Mungu, ambaye ameuumba ulimwengu kwa msingi wa uadilifu, mbali na katika mfumo wa uumbaji, ameliweka hilo pia katika mfumo wa hukumu na sharia kama inavyoeleza aya ya 90 ya Suratu-Nahl ya kwamba: "Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani…"

Imam Ali (AS), ambaye mwandishi wa Kikristo George Jordac, amemtaja kuwa ni sauti ya uadilifu ya ulimwengu wa ubinadmu, ameitumia ilhamu ya maneno ya wahyi kuielezea kama ifuatavyo nafasi na faslafa ya uadilifu: "Mwenyezi Mungu aliyetakasika, ameufanya uadilifu kiimarishi cha maisha ya watu, kuepusha upotezaji haki, dhulma, uonevu, ufanyaji madhambi na kuwepesisha mambo katika Uislamu. (Ghurarul-Hikam). Kwa hivyo kudumu na kubaki kwa mfumo wowote ule, kuko kwenye utegemezi usiokanushika wa uadilifu. Na sababu ni kuwa, katika mfumo kama huo, hakutakuwepo na alama yoyote ya dhulma, ambayo ni mkabala na dhidi ya uadilifu; na kwa njia hiyo, anga na mazingira mwafaka yatapatikana kwa ajili ya kustakimu, kustawi na kuamirika kwa Uislamu. Kwa hivyo katika mfumo wa kiuadilifu wa Uislamu, jamii haipasi kukengeuka mkondo wa uadilifu kwa namna yoyote ile na kwa sababu yoyote ile iwayo.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amelikabidhi zaidi jukumu na masuulia ya kutekeleza uadilifu kwa watu walio na imani ya kweli ya Uislamu. Na ndipo akawahutubu kama ifuatavyo, katika aya ya nane ya Suratul-Maaidah: "Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda."

Katika hali hiyo uadilifu unakuwa mithili ya njiakuu, ambayo inapasa ipitwe na watu wote, pasi na yeyote yule kati yao kukwezwa au kupewa upendeleo. Kwa maana kwamba, haitakubalika mtu yeyote yule kukiuka msingi wa uadilifu, bila kujali hadhi yoyote ya kisiasa, kiuchumi au kijamii aliyonayo; hasa katika mfumo wa kiuadilifu wa Uislamu, ambapo kila mtu anatakiwa awe mchaMungu na awe na yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayaona matendo yake yote, na ni Mjuzi wa kila jambo na kwamba Siku ya Kiyama, kila mmoja wao atapaswa kuwajibika kwa matendo yake atakapohukumiwa kwa “uadilifu wa Mwenyezi Mungu”. Kwa maana kwamba, katika mahakama hiyo, amali ndogo na hafifu kabisa ya jema na baya tuliyofanya, itajidhihirisha; na haitawezekana mtu kulitolea udhuru kwa namna yoyote ile baya alilotenda.

Kinyume na dhulma na uonevu, ambao ni ukiukaji wa uadilifu na haupendezi mbele ya watu wote; uadilifu, ambao una chimbuko katika fitra na maumbile ya wanadamu wote, kama ilivyo suluhu na umoja, ni jambo linalopendwa na kila mtu. Imam Jaafar Sadiq (as) amelitolea taswira safi na wadhiha hitajio hilo la msingi la wanadamu, aliposema: “Uadilifu una ladha tamu zaidi kuliko asali, ni laini zaidi kuliko jabali na unanukia vizuri zaidi kuliko miski.” (Al Kafi, Juz. 2, Uk. 147)

Pamoja na yote hayo, haipasi kuufanya uadilifu kitu cha kaulimbiu tu na cha kutumiwa kama chombo cha kimaslahi; kwa sababu watu wataweza kuhisi ladha tamu ya uadilifu, na harufu nzuri ya manukato yake itaweza kuenea kwenye anga ya maisha yao, pale kila mmoja wao atakapohisi uadilifu unatekelezwa katika mfumo na jamii anayoishi; na akajionea kwa macho yake mifano hai ya namna uadilifu unavyofanya kazi katika maisha yake ya kijamii. Kwa kuzingatia ukweli huo, ndipo Mwenyezi Mungu akaamuru kwa msisitizo kutekelezwa uadilifu, kama alivyosema katika aya ya 58 ya Suratun-Nisaa: “Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Lakini mbali na hayo, ifahamike pia kuwa, uadilifu si suala la uga mmoja na upande mmoja tu, bali inapasa lijumuishe nyuga zote za utamaduni, siasa, elimu, uchumi, utoaji hukumu na masuala mengine yote yenye mfungamano na uhai wa jamii ya watu na ambayo kwao wao ni miongoni mwa mahitaji ya lazima. Nukta nyingine ya msingi ni kwamba, uadilifu utapata maana yake halisi na itakayokubalika na watu waliowengi katika jamii, pale viongozi wanapokuwa wa mbele katika utekelezaji wake. Linapothibiti hilo, ndipo uadilifu utapata nafasi na hadhi yake maalumu na kurasimishwa ndani ya jamii nzima. Imam Ali (as), ambaye baada ya kuvumilia machungu mengi na kuhimili misukosuko mingi, na hatimaye kutokana na kujitokeza watu kwa wingi waliomshikilia ashike hatamu za uongozi, alipokubali kubeba jukumu hilo, baadhi ya watu waliojali manufaa na maslahi yao tu walimshawishi aache kutekeleza uadilifu ili asije akateteresha nafasi yake ya utawala. Mtukufu huyo aliwakabili watu hao na kuwaambia: “Nyinyi mnanitaka nitafute ushindi kwa gharama ya kufanya ubaguzi na uonevu? Mnanitaka niutoe mhanga uadilifu kwa ajili ya siasa na ubwana? Naapa kwa Mwenyezi Mungu maadamu dunia ni dunia, sitafanya hivyo.” (Nahjul-Balagha, Khutba 126). Na kwa maneno hayo ya Imam Ali (as) aliyekuwa mwalimu na dhihirisho kamili la uadilifu, niseme pia kwamba sehemu ya 20 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga mpendwa msikilizaji hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 21 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/