Nov 07, 2022 02:14 UTC
  • Jumatatu tarehe 7 Novemba 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na 7 Novemba 2022.

 Siku kama ya leo miaka 1312 iliyopita, yaani tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani mwaka 132 Hijria, Abul Abbas Abdullah bin Muhammad maarufu kwa jina la 'Saffah' alikalia kiti cha uongozi akiwa khalifa wa kwanza wa kizazi cha Bani Abbasi. Utawala huo wa Kiabbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khorasani na majeshi yake, ulimuuwa Marwan wa Pili, mtawala wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah na kuondoa madarakani utawa wao. Bani Abbas nao kama walivyokuwa watawala wa Bani Umayyah, waliwakandamiza raia na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) na kufanya dhulma kubwa, na utawala wao uliendelea kushika madaraka katika ulimwengu wa Kiislamu hadi mwaka 656 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.

Marie Curie

Katika siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, Leo Trotsky mmoja kati ya viongozi wakuu wa mapinduzi nchini Russia alizaliwa. Alibaidishwa Siberia mara mbili katika zama za utawala wa Tsar kutokana na kujihusisha kwake na harakati za mapinduzi. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Russia, Trotsky alirejea nchini Russia. Hiyo ilikuwa mwaka 1917 na akapatiwa wadhifa wa Kamishna wa Masuala ya Kigeni. Mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Kamishna wa Vita ambapo baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Ujerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, alianzisha mapambano dhidi ya wapinzani wa mapinduzi. Hata hivyo baada ya kuaga dunia Lenin, mwanamapinduzi huyo alishindwa katika vita vyake na Joseph Stalin na mwaka 1925 alibaidishiwa Siberia na baadaye huko Uturuki. Hatimaye aliuawa mwaka 1940 huko Mexico na makachero wa Lenin.

Leo Trotsky

Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Albert Camus mwandishi mashuhuri wa Ufaransa. Licha ya kuwa familia yake ilikuwa masikini, lakini kutokana na kipaji, bidii pamoja na irada thabiti aliyokuwa nayo, Camus alifanikiwa kupata umashuhuri mkubwa. Mwandishi huyo wa Kifaransa ana vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Firs Man, The Fall, The Stranger na A Happy Death. ***

Albert Camus

Na siku kama ya leo miaka 66 iliyopita vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo.

Vita vya Suez