Akhlaqi Katika Uislamu (23)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 23 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia sifa muhimu ya utamaduni mkwasi wa Uislamu ya kukataa madhila, kudunishwa na kudhalilishwa. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Kama ujuavyo mpendwa msikilizaji, mada kuu tunayoendelea nayo kwa sasa katika mazungumzo yetu ni kuhusu akhlaqi katika jamii ya Kiislamu. Katika jamii hiyo inayotawaliwa na umoja na mshikamano, suluhu na urafiki, kutetea uadilifu na kupinga dhulma na uonevu; kuimarisha izza na heshima na kukataa kudunishwa na kudhalilishwa ni sifa nyingine maalumu na muhimu inayotawala katika jamii ya Kiislamu. Chimbuko la utamaduni huu wenye thamani kubwa ni Qur'ani tukufu, ambacho ni kitabu cha mwongozo wa maisha kinachowafunza Waislamu yafuatayo, kama sehemu ya mwisho ya aya ya nane ya Suratul-Munafiqun inavyosema: "Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui."
Wakati Imam Hussein (AS) alipofikishwa njiapanda na Bani Umayya, walioitoa kafara dini kwa sababu ya dunia na akalazimika kuchagua baina ya izza na heshima kwa kuuawa shahidi au kubaki hai katika hali ya kuwa duni na dhalili, aliitumia ilhamu aliyopata katika aya hii ya Qur'ani, akawaelekea watu na kuwaambia: "Tambueni kwamba, huyu asiye mwana wa halali, na mtoto wa asiye mwana wa halali (akimkusudia Ubaidullah na baba yake Ziyad), ameniweka njiapanda ya upanga (ili niuawe) au kukubali kuwa dhalili. Lakini katu sitaridhia madhila, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mtume na waumini hawapendelei sisi turidhie kuwa dhalili." Kisha mtukufu huyo akazungumzia jinsi Nyumba yenye izza na utukufu ya Utume na Uimamu ilivyochangia katika malezi yaliyojenga shakhsia yake na akasema:
"Nimekulia kwenye mikono toharifu (niliyopatia malezi) na watu wenye nyoyo safi, roho zenye ghera na nafsi zenye sharafu; na kwa hivyo tunafadhilisha kujitoa mhanga… kuliko kuwatii watu duni." (Historia ya T'abari 423/4/5).
Kwa maelezo hayo na kwa mujibu wa itikadi za kitauhidi, sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na viongozi wateule wa dini, hakuna mtu yeyote mwenye imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu, anayefikishwa kwenye njiapanda ya kuchagua baina uhai na mauti, akawa tayari kufanywa dhalili na kuwaridhia madhalimu ili aweze kubaki hai; kwa sababu moja ya neema ya kumwamini Mwenyezi Mungu ni kwamba, watu wote, hasa wenye imani ya tauhidi huwa wamezikomboa nafsi zao na minyororo ya utumwa na kuwa dhalili wa kukubali kutii nguvu zozote zile bandia; na badala yake wanapigania kupata izza, utukufu na heshima itokanayo na Mola wao. Ni muhimu tufahamu pia kwamba, hata kama Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa kumfanya kiumbe huru na kumwachia mwenyewe mamlaka ya kujiendeshea masuala yote ya maisha yake, lakini kama anavyotuelimisha Imam Jaafar Sadiq (AS) ni kwamba, hakumpa hiari na mamlaka ya kuridhia kuwa duni na dhalili pia. (Al-Kafi 63/5).
Katika kuurasimisha mtazamo na fikra hiyo ya kitauhidi ya kuleta izza na heshima, Imam Ali (AS), ambaye alikuwa akijifakharisha na kuona ni upeo wa izza na utukufu kwa yeye kuwa mja wa Mwenyezi Mungu, alimuusia yafuatayo mwanawe mpenzi Imam Hassan (AS), katika sehemu moja ya barua ya mawaidha na nasaha aliyomwandikia: "Mwanangu mpenzi, jiweke mbali kabisa na kila aina ya udhalili na kujidunisha, hata kama kutakufikisha kwenye unayoyatamani (ya kupita), kwa sababu matunda yoyote utakayopata katika muamala huo hayawezi katu kulingana na rasilimali ya izza, heshima na sharafu yako. (Nahjul-Balaghah/ barua ya 31)
Bila shaka, kinyume na mtazamo huu wa kitauhidi wa kutetea heshima na kupinga madhila, watu wenye uono finyu na ujuzi wa kijuujuu wa mambo, wanaotaka warefukiwe zaidi na maisha japo kwa siku chache na au kupata raha na uneemevu wa kupita wa dunia, huwa tayari kuridhia madhila ya aina yoyote, hasa ya wale wenye madaraka ya juu kabisa ya utawala, au walioghariki kwenye bahari ya utajiri, starehe na anasa za maisha. Si hao peke yao, lakini wakati mwingine hata watu wa mataifa yaliyozoea raha na ureda, huwa tayari kuridhia madhila japo ya muda mfupi ili tu waendelee kupata starehe zao bandia na za kupita. Imam Ali (as), ambaye alisikika akiwaambia watu, yeye si kama nyamahoa wa miguu mine anayeishi maisha ya malishoni, akawa anahughulishwa na malisho tu, aliupinga vikali udhalili kwa kusema: "Ni kitendo cha kuhasirisha mtu kukubali kudhalilishwa hata kwa muda mchache, ili aweze kuishi kwa heshima, raha na starehe hadi mwisho wa maisha yake." (Ghurarul-Hikam-58)
Hapana shaka kuwa, watu wasio na mtazamo wa kutetea izza na heshima na kupinga kudunishwa na kudhalilishwa, huwa wanadhani kwa mawazo yao kwamba, wataweza kuishi maisha ya kuheshimika na yenye izza pale watakapojikomba na kuwakumbatia waliohodhi nguvu za utajiri na madaraka; na kwamba kama watajiweka mbali nao au watataka kusimama dhidi yao watadunika na kudhalilika. Mwenyezi Mungu Mtukufu, mtoaji wa izza na sharafu ameibatilisha dhana hiyo ghalati na mtazamo huo potofu, alipomwagiza Mtume wake, ambaye ni mnadi wa izza, heshima na adhama ya jamii ya wanadamu, awatangazie watu maneno haya ya aya ya 26 ya Suratu-Aal Imran:
"Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza wa kila kitu."
Kwa mtazamo wa kiujumla, katika utamaduni wa Uislamu asili unaompa mtu izza na heshima na kupinga kudunishwa na kudhalilishwa, haikubaliki kwa namna yoyote ile mtu aridhie kudhalilishwa, hasa kama ataliridhia hilo kwa hamu na shauku yake mwenyewe. Bwana Mtume Muhammad SAW, aliyasema haya yafuatayo zaidi ya karne 14 nyuma:
"Yeyote atakayejitakia mwenyewe na kuungama kuwa duni na dhalili (kwa sababu ya mapambo na marembo ya kidunia), si katika sisi Ahlubaiti." (Tuhaful-Uqul 58)
Mpendwa msikilizaji, tumwombe kwa pamoja Mwenyezi Mungu Mtukufu aupe izza, heshima na utukufu zaidi Uislamu na Waislamu kwa kusimama imara dhidi ya Uistikbari na Ubeberu wa dunia. Na kwa dua hiyo ya kheri niseme pia kwamba sehemu ya 23 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 24 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/