Nov 10, 2022 15:08 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (36)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 36 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia nafasi ya akili katika Akhlaqi za Kiislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika sehemu ya 35 ya kipindi hiki tulizungumzia uhuru wa fikra katika mfumo wa kiutamaduni wa Uislamu na tukaeleza kwamba, Qur'ani tukufu inatufunza kuwa, tusikilize, tusome na tuhakiki mitazamo na fikra tofauti bila kusukumwa na hisia za chuki au upendeleo kwa fikra yoyote ile, kisha tufuate iliyo bora na ya mantiki zaidi.

Kama nilivyotangulia kueleza kwenye utangulizi wa kipindi chetu, mada yetu ya leo ni nafasi ya akili katika Akhlaqi za Kiislamu.  Katika aya ya pili ya Suratu-Yusuf, Mwenyezi Mungu Mola Mjuzi na Mwenye hekima ameitaja falsafa na hekima ya kuteremshwa Qur'ani kuwa ni watu kuitumia neema na kipawa cha akili alichowajaalia Yeye Mola, na akasema: "Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili mpate kutia akilini".

Hakuna shaka kuwa ili kuweza kuufahamu ujumbe wenye madhumuni mapana na ya kina wa Qur'ani, unaompa uhai na kumtengenezea mtu maisha yake, kuna haja ya msingi ya kutafakari na kuitumia akili. Hivi sasa karne 14 zimepita tangu ilipoteremshwa Qur'ani; na wanazuoni na watafiti wengi wa Kitabu hicho cha mbinguni, kila mmoja wao amefanya uhakiki wa kuifasiri Qur'ani katika uga ama wa kifalsafa, kifiqhi, kijamii, kiirfani na kifasihi au wa fani ya masuala ya itikadi, yaani ilmul-kalam au Hadithi na kuacha athari za maandiko yenye thamani kubwa. Mwenendo huo ungali unaendelea mpaka zama zetu hizi, lakini kungaliko na mengi mapana na ya kina kuhusu Qur'ani ambayo bado hayajajulikana na yanahitaji kuchunguzwa na kutafakariwa kila uchao.

Ni muhimu sana kuelewa kwamba, baada ya Qur'ani, Sunna na Ijmaa au makubaliano ya mafaqihi wote, nguzo nyingine, miongoni mwa nguzo nne kuu za Ijtihadi kwa mafaqihi wabobezi wa Uislamu ni "akili"; nukta inayodhihirisha nafasi na hadhi ya kipawa hicho katika utamaduni wa kuhakiki na kutafiti elimu wa Uislamu. Lakini mbali na hayo Qur'ani inawakemea watu wasiotafakari na kuzingatia kwa kina aya za Kitabu hicho kama inavyoeleza aya ya 24 ya Suratu-Muhammad ya kwamba: "Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?" 

Kwa hiyo Qur'ani ni kitabu cha "kutumia akili", kutafakari na kufikiri; na kinawataka wafuasi wake wa kweli kuutumia mwanga wa akili ili kuweza kupambanua baina ya haki na batili na njia ya uongofu na ile ya dhalala na upotofu.

Imam Muhammad Baqir (AS), ambaye ni mwasisi na mhuishaji wa utamaduni wa Kiislamu amesema: "Wakati Mwenyezi Mungu alipoiumba akili aliiambia: Naapa kwa izza yangu na utukufu wangu kwamba sijaumba kitu chema zaidi na chenye hadhi ya juu zaidi kuliko wewe; ni kutokana na wewe ninaamrisha na ninakataza; na kwa sababu ya wewe, ninalipa thawabu au adhabu (kwa waja wangu)". Al Kafi 1/26/26.

Wakati watu walipomsifu mwenzao mmoja mbele ya Bwana Mtume SAW kwa ufanyaji wake mzuri wa ibada, mtukufu huyo aliwaambia: Itazameni akili yake. Kwa hakika watalipwa waja malipo yao Siku ya Kiyama kulingana na akili zao (zilivyokuwa).

Maudhui nyingine muhimu yenye umuhimu mkubwa na ambayo imezingatiwa katika utamaduni wa Kiislamu tu peke yake ni tafsiri na maana ya akili.

Kwa mtazamo wa kiujumla, wanadamu wote wamejaaliwa kuwa na kipawa cha akili; na kwa mtazamo huo, wote wana hali moja na sawa. Lakini katika mtazamo wa kimsingi wa Uislamu, akili ina maana maalumu inayoipambanua na akili ya kawaida waliyonayo watu wote. Alipoulizwa suali kwamba akili ni kitu gani? Imam Jaafar Sadiq (AS) alisema: "Akili ni kitu ambacho, kwa sababu yake Mwenyezi Mungu Mrehemevu anaabudiwa na kutiiwa (na matokeo yake) ni kupata Pepo ya Mwenyezi Mungu. Al Kafi 1/11/3

Kwa muktadha huo, akili yoyote inayomfanya mtu ajiweke mbali na kumwabudu na kumtii Mwenyezi Mungu, huwa haina hadhi wala thamani kwa mtazamo wa usuli na misingi ya Kiislamu. Na ndio maana wakati mpokezi wa Hadithi tuliyosoma alipomuuliza Imam Jaafar Sadiq (AS) kwamba, kwa mujibu wa tafsiri uliyotoa kuhusu akili, kile alichokuwa nacho Muawiya kilikuwa ni nini? Mtukufu huyo alijibu: Zile ni hadaa na uafriti uliofanana na akili, lakini sio akili".

Ikiwa akili timamu ya mtu itajifungamanisha na Mwenyezi Mungu, matunda yatakayoota kutoka kwenye mti wa akili hiyo ni sifa njema za kiakhlaqi za watu wa peponi, ambazo marashi na manukato yake yatazifariji na kuziburudisha nyoyo na nafsi za waja.

Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye alikuwa ruwaza na mfano wa kuigwa katika akhlaqi zote za kiutamaduni za Uislamu amelitolea ufafanuzi hilo kwa kusema: "Katika ishara za mtu mwenye akili na busara ni kuwa mstahamilivu na mwenye subira mbele ya tabia za kijahili za watu wajinga. Humsamehe aliyemdhulumu. Huwa mnyenyekevu mbele ya waliochini ya mamlaka yake. Huwa wa mbele katika kuwafanyia wema wanyonge. Kila anapotaka kusema hufikiri kwanza; kama analotaka kusema lina faida hunena na kama si neno jema hunyamaza ili aepukane na dhara yake. Kila akabiliwapo na fitna na balaa humwomba Mwenyezi Mungu amlinde na shari yake. Huudhibiti mkono na ulimi wake; na kila aionapo fadhila yoyote ya kheri huijali thamani yake. Haya na staha huonekana muda wote katika mwenendo wake na haionekani kwake pupa na uchu".

Bwana Mtume SAW akamalizia kwa kusema: "Hizi ni sifa na hulka kumi zenye thamani, ambazo mtu mwenye akili na busara hupambika nazo". Tuhaful-Uqul- 28

Kwa hivyo ikiwa akili haitapambwa na thamani aali na tukufu za kiakhlaqi, za kuipa muelekeo na kuionyesha lengo sahihi, itaghilibiwa na kutekwa na hawaa na matamanio ya nafsi na wasiwasi wa shetani na kumfanya mtu awe mpenda jaha, mpaparikia dunia, mtekwa na anasa na mapambo yake; na baya zaidi na lenye madhara makubwa zaidi ya yote hayo, kugubikwa na mghafala wa kumsahau Mwenyezi Mungu ndani ya nafsi yake na hivyo kuzimikiwa na mwanga wa akili wa kumuelekeza kwenye njia sahihi na ya sawa. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya 36 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 37 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/