Nov 10, 2022 17:07 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (40)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 40 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia nukta nyingine za kiuchumi za Akhlaqi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika kipindi kilichopita tulitoa ufafanuzi mfupi kuhusu mfumo wa kiuchumi wa Uislamu, ambao mhimili wake mkuu ni imani juu ya Mwenyezi Mungu. Msingi mwingine muhimu na wenye nafasi maalumu katika mfumo wa kiuchumi wa Uislamu ni "kuamini Maadi" yaani kufufuliwa kwa viumbe; imani ambayo inaipa mlingano na ukadirifu mipango na njia za utekelezaji za kiuchumi. Kwa upande mmoja, Uislamu unaihimiza na kuishajiisha jamii ya wanadamu ifanye bidii na juhudi za kujituma katika nyuga zote za kiuchumi na kuwataka watu wasifanye ajizi ya kuchukua kila hatua kuhakikisha wanajitosheleza na kujitegemea kiuchumi; na kwa upande mwingine unawataka, mbali na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, wasighafilike pia na kuikumbuka siku ya kufufuliwa; na wawe na yakini kwamba, watakaposimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu lazima wataulizwa na kutakiwa wajibu mali na kila walichokuwa nacho walikipataje na kwa kupitia njia gani. Lakini pia walikitumia vipi na kwa nia ipi. Kuwa na mtazamo huu kunamfanya mtu mwenye imani juu ya Mwenyezi Mungu na itikadi ya kufufuliwa asikengeuke njia ya sawa ya kadiri na wastani; na kwa hivyo katika jitihada zote anazofanya kwenye shughuli zake za kiuchumi, hujichunga ili kuhakikisha hajiharibii maisha yake ya akhera katika ulimwengu wa baada ya kifo.

Imam Hassan al Mujtaba (AS) ameizungumzia nukta hii kwa kusema:"fanya juhudi kwa ajili ya dunia yako kama kwamba utaishi milele na ishughulikie akhera yako kama kwamba utakufa kesho."Wasaail juzuu ya 2, Uk. 535

Qur'ani tukufu inatupa mtazamo wa kiujumla kuhusu Waislamu kwa kuwatambulisha kuwa ni watu wa umma wa kadiri na wastani wa mambo, kama inavyoeleza aya ya 143 ya Suratul-Baqarah ya kwamba: "Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu."

Bwana Mtume SAW, ambaye mwenendo na sira yake ilichukua ilhamu kutoka kwenye chemchemi ya Qur'ani alikuwa akifuata njia ya kadiri na wastani, ya baina ya wakumbatiaji dunia na wanaofikiria akhera pekee. Kwa upande mmoja alikuwa akiihimiza na kuishajiisha jamii kuchapa kazi na kufanya juhudi katika nyuga zote za uzalishaji, biashara na kilimo na kunufaika na suhula za kimaada; na kwa upande mwingine alikuwa akiimarisha katika nyoyo za waumini misingi ya imani juu ya Mwenyezi Mungu na ufufuo ili kuhuisha thamani tukufu za kiakhlaqi, kiutu na kimaanawi, sambamba na kukabiliana na kila aina ya upotofu unaokengeuka mkondo wa kadiri na wastani.

Inasimuliwa kwamba kundi moja la masahaba wa Bwana Mtume SAW waliamua kujijenga na kujitakasa nafsi zao kiroho kwa kufunga mchana, kusimama usiku kwa Sala na kuepuka kuchanganyika na wake zao. Ummu Salama, mke wa Bwana Mtume SAW aliisikia habari hiyo na akamfikishia Bwana Mtume. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaendea masahaba zake hao na kuwauliza: "Ni kweli mumejitenga na wake zenu? Mimi ambaye ni Mtume wenu sina mwenendo huo. Siachi kujishughulisha na kufanya kazi. Mchana nachanganyika na watu katika jamii, ninakula kama wanavyokula watu wengine na ninapumzika. Basi yeyote asiyefuata suna na mwenendo wangu, huyo hatokani na mimi." Wasaail 2/5

Lakini kinyume, na mkabala na kundi hilo la masahaba waliotaka kuishi maisha ya utawa na ambao walilaumiwa na kukemewa na Bwana Mtume SAW, kuna kundi jengine la watu walio na mwenendo mbadala na huo, ambao wameghariki na kuzama kwenye dimbwi la kupenda vitu vya kidunia, mpaka Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyeuumba ulimwengu kwa msingi wa kadiri na wastani, akamwamuru Mtume wake huyo mteule kwa kumwambia kama aya ya 103, 104 na 105 za Suratul-Kahf zinavyosema: "Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao? Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri. Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu."

Katika makamilisho ya maudhui hii tunafikia hitimisho kwamba, katika utamaduni wa "Akhlaqi za Kiuchumi za Uislamu" tunatakiwa daima tushike njia ya kadiri na wastani; kwa maana kwamba, tusiache kufanya juhudi na kujishughulisha na harakati za kiuchumi tukajikosesha kuishi maisha ya heshima na sharafu. Na wakati huohuo, tusighafilike na ulimwengu wa baada ya kifo, kwa kughariki kwenye dimbwi la raha na anasa za kupita za dunia kama kwamba baada ya dunia hii, hakutakuwepo na akhera wala malipo.

Bwana Mtume SAW, ambaye ndiye ruwaza na mfano bora wa kuigwa, ametuusia na kututahadharisha na kukengeuka njia na mwenendo wa kadiri na wastani aliposema: "Si miongoni mwetu sisi, yule anayeiacha dunia yake kwa kisingizio cha kushika dini, au akaiacha dini yake kwa sababu ya (manufaa ya kupita) dunia." Tuhaful-Uqul.

Kwa hivyo kwa mtazamo wa Uislamu wa asili, inapasa tunapofanya jitihada na bidii za kujistawisha kiuchumi, tuhakikishe wakati huohuo tunafanya hima na juhudi za kujiandalia mustakabali wetu wa milele katika ulimwengu mwingine, ili kwa kufanya hivyo, tuistawishe na kuinawirisha dunia yetu hii ya kupita na vilevile kuiandaa kwa matumaini akhera yetu ya milele. Bwana Mtume SAW amewasifu watu wenye sifa na mwenendo huo aliposema: "Kati ya watu wote, mwenye hadhi na daraja ya juu zaidi, ni mtu muumini aliye na hima katika mambo yake ya dunia na akhera."

Mpendwa msikilizaji, kama tutazishika barabara akhlaqi za kiuchumi za Uislamu kwa kufuata mtazamo na muelekeo huu, tutaweza kunufaika kwa namna bora na dunia ya vitu vya kimaada kwa faida ya akhera yetu.

Imam Ali (AS) alimtaalamisha mtu mmoja aliyekuwa akiisema vibaya dunia kwa kumwambia: "dunia ni mahali pa tijara na biashara kwa mawalii na vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Dunia ni mahali pa ibada na sujudio la watu wanaompenda Mwenyezi Mungu." Hekima ya 131-Nahjul-Balagha.

Kwa hivyo, kwa kutumia mbawa mbili za imani juu ya Mwenyezi Mungu na kuitakidi kuwepo kwa ufufuo tutaweza kuwa na maisha ya raha na utulivu ya hapa duniani na tutaweza pia katika ulimwengu wa baada ya kifo, kuwa na hadhi ya juu kimaanawi na kuneemeka na raha na starahe za milele na zisizo na mwisho. Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya 40 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 41 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

 

 

Tags