Nov 19, 2022 02:27 UTC
  • Jumamosi, 19 Novemba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 19 Novemba 2022 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar mashuhuri kwa jina la Hatami au Baghdadi mtambuzi wa lugha, mwanaisimu na msomi wa Kiislamu aliaga dunia. Alisoma elimu ya fasihi na utambuzi wa lugha kwa walimu mahiri wa zama zake. Baadaye Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar alianza kufundisha katika uga huo mjini Baghdad. Darsa na vikao vyake vya masomo vilikuwa na kiwango cha hali ya juu. Ameandika pia kitabu kinachojulikana kwa jina la Hatamiyeh ambacho kinaelezea nakisi na mapungufu ya mashairi ya malenga na washairi wa zama zake. ***

Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar mashuhuri kwa jina la Hatami au Baghdadi

 

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, alifariki dunia Franz Schubert mtunzi wa nyimbo maarufu wa nchini Austria. Schubert alizaliwa mwaka 1797 katika familia masikini. Tangu akiwa kijana mdogo alipendelea sana nyimbo huku akiwa na kipawa kikubwa katika uwanja huo na hivyo kuamua kusomea taaluma hiyo. Alianza kubuni nyimbo akiwa kijana na katika umri wake wote aliimba zaidi ya nyimbo 600. Hata hivyo licha ya kuimba nyimbo nyingi hususan mziki wa asili, bado hakuweza kujinasua kutoka kwenye umasikini. Hii ni kwa kuwa nyimbo zake hazikupokelewa kwa wingi na jamii ya wakati wake. Ni baada ya kufariki dunia ndipo nyimbo zake zikapewa umuhimu mkubwa katika jamii. ***

Franz Schubert

 

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko Allahabad nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa. ***

Indira Gandhi

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari katika Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Sadat ambayo pia ilizusha machafuko na ghasia nchini Misri kwenyewe. Hatimaye mwaka 1981 Khalid Islambuli aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri alimpiga risasi na kumuua Sadat akipinga hatua yake ya kutia saini mkataba muovu wa Camp David. ***

Anwar Sadat

 

Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam lililokuwa likiongozwa na gaidi Msaudi Arabia, Majid al Majid ambalo ni miongoni mwa matawi ya kundi la kigaidi la al Qaida, lilishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran mjini Beirut huko Lebanon kwa kutumia magaidi wawili waliojilipua kwa mabomu. Katika mashambulizi hayo mawili ya kigaidi watu 23, akiwemo Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari aliyekuwa Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran nchini Lebanon na mke wa mmoja kati ya wanadiplomasia wa Iran, waliuawa shahidi na watu wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa. Walinzi wanne wa ubalozi wa Iran mjini Beirut pia waliuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Majid al Majid alitiwa nguvuni lakini aliuawa kwa njia ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi mjini Beirut kabla ya kutoa taarifa yoyote na maiti yake ikakabidhiwa kwa maafisa wa utawala wa Saudi Arabia. ***

Shambulio la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Beirut