Jumatatu, Disemba 12, 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Mfunguo Nane Jumadil Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Disemba 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1153 iliyopita, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab, msomi mashuhuri wa lugha na nahau. Tha’labi aliyekuwa na asili ya Iran ya alizaliwa mwaka 200 Hijiria mjini Baghdad. Kutokana na kumbukumbu yake nzuri alijifunza kwa haraka elimu ya nahau, lugha ya Kiarabu, kusoma Qur’ani na hadithi mbele ya walimu wa zama hizo. Akiwa kijana mdogo tayari alikuwa amehifadhi fasihi ya lugha ya Kiarabu ambapo alilipa umuhimu suala hilo huku akifikia daraja ya juu katika uga huo. Miongoni mwa athari zilizosalia hii leo kutoka kwa Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab ni kitabu cha ‘Majaalisu Tha’lab’ ‘Kitabul-Faswiih’ na ‘Qawaidu al-Shi’r.’
Miaka 994 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mmoja wa wasomi na wanafalsafa wakubwa wa Kiislamu na Kiirani Abu Hamid Muhammad Ghazali, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumuddin," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme".
Katika siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kifaransa, Gustave Flaubert katika mji wa Rouen nchini Ufaransa. Alipenda sana taaluma na fasihi akiwa bado kijana na kwa sababu hiyo aliacha masomo ya sheria, akaondoka Paris na kwenda kuishi maeneo ya vijijini. Wakati huo ndipo alipoandika vitabu vilivyompa umashuhuri mkubwa. Japokuwa Gustave Flaubert hakuandika vitabu vingi lakini athari na vitabu vichache vya mwandishi huyo vinahesabiwa kuwa vya aina yake katika taaluma ya fasihi duniani. Vitabu mashuhuri zaidi ya Gustave Flaubert ni Madame Bovary, Sentimental Education na Three Tales. Flaubert aliaga dunia tarehe 8 Mei mwaka 1880 akiwa na umri wa miaka 59.
Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Guglielmo Marconi ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani.
Tarehe 12 Disemba 1963, yaani siku kama hii ya leo miaka 59 iliyopita, Kenya ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi. Harakati ya wananchi iliyoongozwa na Jomo Kenyata ilipambana na wakoloni hao katika vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchini humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.