Jan 24, 2023 04:04 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 11 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

إِذَا قَدَرْتَ عَلَى عَدُوِّکَ، فَاجْعَلِ الْعَفْوَ عَنْهُ شُکْراً لِلْقُدْرَهِ عَلَیْهِ

Unapomshinda adui yako, msamehe kama njia ya kumshukuru Mungu kwa kukupa nguvu za kumshinda.

Mara nyingi tunapozungumzia neema za Mwenyezi Mungu, huenda baadhi ya wakati tukadhani kuwa neema ni kile kitu kinachoonekana kwa macho na kushikika kwa mkono tu, kama zawadi tunayopokea kutoka kwa rafiki na riziki zinazoingia mikononi mwetu kila siku. Lakini ukweli ni kuwa si neema zote za Allah zinaweza kuonekana kwa macho na kushikika mkononi. Mifano iko mingi. Hivi umepata kujiuliza, mapenzi ambayo Mwenyezi Mungu ameyatia katika nyoyo za watu na kumfanya mtu apendwe, je, hii si neema ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema? Je, si ni katika neema kubwa wakati furaha inayokaa moyoni inapochukua nafasi ya huzuni? Je, neema hizi zinaonekana kwa macho na kushikika kwa mkono?

Kwa upande mwingine, sote tunajua kabisa kwamba shukrani ni muhimu kwa kila neema. Shukrani ikitolewa kwa kila neema, hupelekea kuongezeka na kudumu neema hiyo na ikiwa shukrani itakosekana, kuna uwezekano mkubwa wa neema hiyo kupungua au kutoweka kabisa. Katika hikma hii ya 11 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatukumbusha neema kubwa, ambayo lau asingelitoa ukumbusho huu, pengine wengi wetu tusingeiona kuwa ni miongoni mwa neema za Allah kwetu na matokeo yake, tusingemshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii.

Amirul-Mu’minin Ali AS anasema katika hikima hii ikwamba:

إِذَا قَدَرْتَ عَلَى عَدُوِّکَ، فَاجْعَلِ الْعَفْوَ عَنْهُ شُکْراً لِلْقُدْرَهِ عَلَیْهِ

Unapomshinda adui yako, msamehe kama njia ya kumshukuru Mungu kwa kukupa nguvu za kumshinda.

 

Yaani ikiwa mtu alitudhulumu na baada ya kupita muda akakumbwa na matatizo na sisi tukapata fursa ya kulipiza kisasi kwa mujibu wa sheria na tukawa na uwezo wa kumuadhibu kwa kitendo chake kibaya, tutambue kuwa kufanikiwa kwetu huko na kumzidi nguvu dhalimu aliyetudhulumu haki yetu,  ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Neema kubwa hii inalifanya ni jambo la wajibu kwetu kumshukuru Allah. Shukrani inayolingana na neema kama hiyo, ni kumsamehe dhalimu huyo. Kama ambavyo shukrani ya elimu ni kuwapa wengine elimu hiyo, shukrani ya utajiri ni kuwanufaisha wengine kwa utajiri huo na ni kuwasaidia wanyonge na waliodhulumiwa, ni vivyo hivyo, shukrani ya kumshinda nguvu dhalimu ni kumsamehe.

Tukitazama maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na Maimamu watoharifu AS, tutaona ushahidi mwingi wa suala hili. Wakati wa ukombozi wa mji wa Makkah, Mtume Muhammad (SAW) alipowashinda maadui zake waliomtesa kwa miaka mingi na kuwaua marafiki na jamaa zake, alisema: Leo; Ni siku ya msamaha na kuhurumiana.

Jambo muhimu hapa ni kwamba kugeuza kisasi kuwa msamaha kuna athari kubwa na ya thamani isiyo na kifani kwa jamii. Ikiwa kila dhulma na kila mauaji yatalipiziwa kisasi hata mauaji yasiyo ya kukusudia, huweza kuenea chuki na uhasama katika jamii, wakati msamaha huangamiza uadui na chuki na kujenga amani na maridhiano katika jamii. Kwa hiyo, pamoja na kuwa ni maadili mema, lakini pia msamaha ni njia nzuri ya kuendesha na kuisimamia jamii.

Tab'an ni muhimu kusema hapa kwamba amri hii inavua baadhi ya mambo. Mambo hayo ni wakati adui anapoona msamaha wako unatokana na woga na udhaifu wako. Pale adui anapotumia msamaha wako kukufanyia uadui zaidi, wakati huo msamaha kwa adui mbaya na afiriti kama huyo huwa hauna maana. Lakini msamaha unapotolewa na mtu mwenye nguvu ya kumwadhibu aliyemkosea na mkosa naye akahisi hivyo, huwa ni katika sifa bora za kimaadili.