Jun 17, 2016 06:33 UTC
  • Ijumaa 17 Juni 2016

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku dunia. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.

Miaka 440 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, yaani tarehe 17 Juni 1576, William Silent kiongozi wa harakati ya wananchi wa Holland dhidi ya Uhispania, alitangaza uhuru wa nchi hiyo. Harakati hiyo ilianza mwaka 1568 na iliandaa uwanja wa kuundwa nchi moja baada ya kuungana majimbo 8 ya Holland. Ingawa Holland ilitangazwa kuwa huru lakini wananchi wa nchi hiyo waliendelea kukandamizwa na wanajeshi wa Uhispania hadi mwaka 1609 yalipotiwa saini makubaliano ya amani kati ya viongozi wa Holland na mafalme wa Uhispania, na kutambua rasmi kujitawala kwa Holland. Nchi hiyo baada ya kujitawala taratibu ilianza kuzidhibiti na kuzikalia kwa mabavu nchi nyinginezo na ilipofika karne ya 17 Miladia Holland iliingia katika kundi la nchi zenye nguvu za Ulaya zilizozikoloni nchi nyinginezo.

Na siku kama ya leo miaka 584 iliyopita, alifariki dunia mjini Cairo Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na hadithi wa Kiislamu. Baada ya kusoma Qur'an na masomo ya awali ya kidini Ibrahim Karaki alianza kufanya safari mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Kitabu cha I'rabul-Mufasil ni moja ya athari zilizoachwa na msomi huyo.

Tags